OUAGADOUGOU, BURKINA FASO
KANSELA wa Ujerumani, Angela Merkel ameonya kuhusu hatari ya kuongezeka ugaidi katika eneo la Afrika Magharibi na kuyataka mataifa ya Ulaya kuchukua hatua dhidi ya hali hiyo.
Kansela Merkel ameyasema hayo katika siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tatu katika eneo hilo la Sahel, ambapo juzi aliwasili hapa akitarajia kuzitembelea Mali na Niger.
Mapambano dhidi ya ugaidi ni suala la kimataifa, alisema baada ya kukutana na viongozi wa mataifa ya Burkina Faso, Mali, Mauritania, Niger na Chad marufu kama G5.
Alisema tatizo lingine ni kuwa Marekani inajaribu kuzuia kupatikana mamlaka ya vikosi vya mataifa ya Sahel katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Aliahidi kuwa Ujerumani itazipatia nchi hizo kiasi ya euro milioni 60 kwa ajili ya jeshi la pamoja kukabiliana na ugaidi
Aidha Rais wa Burkina Faso, Roch Marc Kabore, ametaka kuchukuliwe hatua za kutatua suala la mzozo wa Libya.
Alisema vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi hiyo vinaathiri eneo lote la Afrika Magharibi.
Tatizo hilo ni lazima lipatiwe suluhisho, amesema na kuongeza kwamba bila hivyo haitawezekana kupiga hatua.