BERLIN, UJERMANI
KANSELA Angela Merkel, ametoa wito wa kutafakari upya mtazamo wa Serikali ya Ujerumani kwa Uturuki baada ya taifa hilo kuwakamata raia wao wawili zaidi.
Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umelegelega tangu jaribio lililoshindwa la mapinduzi mwaka 2016.
“Hakuna msingi wa kisheria wa kukamatwa kwao,” alisema Merkel akielezea kuhusu Wajerumani hao waliokamatwa Alhamisi iliyopita nchini Uturuki.
Kukamatwa kwao kunafikisha idadi ya raia wa Ujerumani waliokamatwa nchini humo kwa sababu za kisiasa kuwa 12.
“Hii ndiyo sababu tunahitaji kuchukua hatua muhimu hapa,” alisema na kuongeza kwamba Serikali yake inapaswa kutafakari upya uhusiano wake na Uturuki.
Merkel alisema Ujerumani tayari imeendeleza kwa kiasi kikubwa uhusiano wake na Uturuki, lakini hatua hii mpya ina maana huenda ni muhimu kutafakari upya zaidi.
“Madai yetu kwa Uturuki yako wazi kabisa,” alisema msemaji wa Serikali ya Ujerumani, Steffen Seibert.
“Tunatarajia Uturuki itawaachia huru raia wa Ujerumani ambao wamekamatwa kwa misingi isiyokuwa ya kisheria.”
Mahusiano baina ya washirika hao wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO yamevurugika tangu Serikali ya Ujerumani ilipoikosoa Uturuki kuhusu ukandamizaji uliofuatia jaribio la mwaka jana la mapinduzi lililoshindwa.
Mwisho