Na Walter Mguluchuma, Katavi
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mpanda imewahukumu watu wanne kifungo cha jumla ya miaka 60 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na vipande 25 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 46 vikiwa na thamani ya Sh 371,600,000.
Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mpanda, Chiganga Ntengwa, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na  upande wa mashtaka.
Washtakiwa waliohukumiwa kifungo hicho ni mkazi wa Kijiji cha Ivungwe, Justine Baruti (39), wakazi wa Kijiji cha  Kalela kilichopo Kasulu mkoani Kigoma, Boniphace Hoza (40), Elias Hoza (46) na  mkazi wa Kijiji cha Ndurumo, Credo Gervas (45).
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkoa wa Katavi, Wakyo Simoni, ulikuwa na mashahidi 15 na washtakiwa walikuwa wakitetewa na Wakili Elias Kifunda na washtakiwa hawakuwa na mashahidi wowote zaidi yao.
Awali, Simoni alidai mahakamani hapo kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo Desemba 24, 2014 katika Stendi Kuu ya Mabasi ya mikoani iliyopo Mtaa wa Mji Mwema uliopo Manispaa ya Mpanda.
Simoni alidai kuwa siku ya tukio hilo, askari wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi na Jeshi la Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa washtakiwa hao  wamepanga kusafirisha meno ya tembo kutoka Mpanda na kuyapeleka Kigoma kwa kutumia basi la Kampuni ya Adventure Connection.