NA KULWA MZEE
DAR ES SALAAM
MENEJA wa Benki I &M Tawi la Kariakoo, Sammer Khan, ameunganishwa katika kesi ya kukwepa kodi na kutakatisha fedha inayomkabili Mfanyabiashara, Mohammed Yusufali na mwenzake.
Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka mapya 506 yakiwamo 62 ya kutakatisha, 132 ya kutoa taarifa za uongo TRA , shtaka moja la kula njama na moja la kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni 24.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita akisaidiana na Leonard Swai, alidai mshtakiwa ambaye ni Meneja wa Benki I&M , Khan anakabiliwa na mashtaka 12 ya kutakatisha fedha kinyume cha sheria.
Inadaiwa washtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Januari mwaka 2008 na mwaka 2016 katika maeneo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Wakili Mwita alidai mshtakiwa wa kwanza, Mohammed na mshtakiwa wa pili, Arifali Palewalla katika kipindi hicho, walikula njama ya kutenda kosa la kukwepa kodi.
Washtakiwa hao pia wanakabiliwa na mashtaka 293 ya kughushi nyaraka na na mashtaka 132 ya kutoa taarifa za uongo TRA.
Wakili wa Serikali, Esther Martine akisoma shtaka la 506, alidai shtaka hilo linawakabili washtakiwa wote ambao wanadaiwa kusababisha hasara ya Sh 24,303,777,426.70 kwa TRA baada ya kuwasilisha nyaraka zenye hesabu za uongo.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwa vile Jamhuri walidai upelelezi umekamilika wako katika za mwisho za kuwasilisha taarifa Mahakama Kuu kesi hiyo ihamie huko kwa ajili ya kusikilizwa.
Mahakama iliahirisha kesi hadi Februari 18 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Awali mshtakiwa Yusufali na Palewalla alikuwa akikabiliwa na mashtaka 601 yakiwamo kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Sh bilioni 14.
Jana walishtakiwa upya ambako mashtaka yalipungua na kubakia 506 na hasara waliyosababisha iliongezeka na kufikia zaidi ya Sh bilioni 24.