Na Pendo Fundisha-
Mbeya
HAKUNA asiyefahamu jitihada na mikakati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kukuza uchumi kwa kuboresha miundombinu ya barabara, umeme pamoja na usafiri wa njia ya anga na majini.
Tumeshuhudia baadhi za sekta zikikamilisha au kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo, kama vile sekta ya umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (REA) awamu ya tatu pamoja na kukamilika kwa baadhi ya barabara zikiwa katika kiwango cha lami, vumbi na changarawe sehemu mbalimbali.
Ukiangalia katika sekta ya anga, Serikali imenunua ndege na kuendelea kuagiza nyingine, lengo likiwa ni kumfikishia na kumrahisishia mwananchi huduma ya usafiri.
Lakini Serikali imeenda mbali zaidi kwa kuboresha miundombinu ya reli pamoja na miundombinu ya bandari na sababu kubwa ni kujaribu kumfikishia mwananchi maendeleo kwa kuzigusa nyanja zote muhimu za kiuchumi.
Hata hivyo, Oktoba mwaka huu, Serikali ya Mkoa wa Mbeya inatarajia kukabidhiwa meli tatu, mbili zikiwa za mizigo na moja ya abiria kupitia kituo cha Bandari ya Itungi kilichopo wilayani Kyela, ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 90.
Meli hizo zinatajwa kutumia kiasi cha Sh bilioni 20 na mtengenezaji wa meli hizo ni Kampuni ya M/s Songoro Marine Transport Ltd.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, anazitaja meli mbili kubwa za mizigo kuwa ni MV Njombe na MV Ruvuma, zikiwa na uwezo kwa kila moja kubeba tani 1000.
Anasema kuhusu meli ya abiria inayotengenezwa katika Bandari ya Itungi ni ya kisasa na itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 200 na shehena ya tani 200 pamoja na magari kwa wakati mmoja.
Kuhusu miundombinu, Makalla anasema ujenzi wa gati la kuegeshea meli katika Bandari ya Kiwira na Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Bandari hiyo umekamilika.
Anasema katika kuhakikisha Serikali inaboresha huduma za kibandari katika Ziwa Nyasa, tayari ukarabati wa pantoni tano kupitia mradi wa chelezo umefanyika katika Bandari ya Itungi na katika Ziwa Nyasa ili zitumike kuboresha huduma kwa abiria na mizigo.
Akizungumzia faida za ujenzi wa meli hizo katika Ziwa Nyasa, Mkuu huyo anasema ujio wa meli hizo kutafungua fursa kubwa ya kukuza na kuboresha shughuli za kiuchumi, kibiashara na kijamii katika ukanda wa Ziwa Nyasa hasa katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Ruvuma na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia.
“Hii inatokana na ukweli kwamba wateja wengi wameonesha utayari mkubwa katika kutumia usafiri wa njia ya maji mara vyombo hivyo vitakapokamilika,” anasema.
Akizungumzia suala la kuongezeka kwa ajira, anasema kukamilika kwa mradi huo kutatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja na kwamba miradi hiyo pia ni kichocheo kizuri cha kufunguka kwa Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara, hivyo kuzifanya bandari za Mtwara na Mbamba Bay kuhudumia soko la Malawi na kupunguza ushindani wa bandari za Msumbiji.
Hata hivyo, anasema jumla ya bandari 15 zinafanya kazi katika Ziwa Nyasa ambazo ni Itungi, Kiwira na Matema zilizopo Kyela, Ndumbi, Lundu, Mkili, Njambe, Liuli na Mbamba Bay zilizopo Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Lumbila, Ifungu, Nsisi, Makonde, Lupingu na Manda zilizopo Ludewa mkoani Njombe.
Aina ya mizigo inayohudumiwa katika bandari za ziwa Nyasa ni makaa ya mawe, mbolea, saruji, mbao, mihogo, mahindi, dagaa, samaki, bati na mizigo mingine mchanganyiko.
Bandari hii inalenga kuwa lango la kuhudumia shehena kutoka na kwenda mikoa ya Mbeya, Njombe na Ruvuma na nchi jirani za Malawi, Zambia na Msumbiji.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kita, anasema ujenzi wa meli hizo unaenda sambamba na ujenzi wa vipande viwili vya barabara vinavyoelekea Bandari ya Itungi na ile ya Kiwira na kwamba Serikali inatarajia kutumia Sh bilioni 3.0.
Anasema lengo la Serikali la kuboresha vipande hivyo vya barabara ni kuhakikisha inawarahisishia wananchi huduma ya usafiri kwa njia ya maji pindi meli hizo zitakapoanza kufanya kazi.
“Ujenzi wa meli hizi tatu ambazo mbili ni za mizigo na moja ya abiria, hautakuwa na maana kama miundombinu ya barabara itakuwa mibovu, ndio sababu Serikali imetenga kiasi cha Sh bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo,” anasema.
Makalla anasema wajibu wao kama Serikali ya Wilaya ni kuhakikisha wanazisimamia fedha hizo zitoke kwa wakati ili kuwapunguzia wananchi adha kubwa wanayoipata wakati wa kusafiri na kusafirisha mizigo yao.
Naye Kaimu Meneja wa Kituo cha Bandari ya Itungi, Ajuaye Msese, anasema jitihada za Serikali katika kuwafikishia wananchi wa pembezoni huduma zitafanikiwa kama baadhi ya changamoto zitatuliwa kwa wakati.
Anasema licha ya Serikali kuhakikisha inaboresha miundombinu ya usafiri kwa njia ya maji kwa kutengeneza meli tatu, huenda jitihada hizo zisizae matunda kutokana na kitendo cha mchanga na udongo kuingia kwa wingi ndani ya bandari hiyo.
“Kituo kimejitahidi kudhibiti uingiaji wa mchanga na udongo kwa kiasi kikubwa kwa kutengeneza ukuta kwa kutumia miti ya asili na majani ambayo kwa kiasi fulani imezuia, lakini pamoja na kudhibiti kwa njia hiyo bado kuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mto Kiwira ambazo zinachangia kuleta udongo na mchanga, hivyo suala la udhibiti linakuwa changamoto kubwa,” anasema.
Anasema kituo hicho kimeendelea na zoezi hilo lakini kwa hali ilipofikia wanaomba mamlaka ya Serikali iangalie ni jinsi gani inaweza kusaidia kudhibiti kwa pamoja kama siku za nyuma kabla ya athari kubwa kutokea.
Msese anaiomba Serikali kuongeza kasi ya ukamilishaji wa miundombinu ya barabara hasa zile zinazoingia katika kituo cha Bandari ya Itungi na Kiwira, lengo likiwa ni kuwasaidia wananchi kwenye suala zima la usafiri.
“Hakuna mawasiliano katika Bandari ya Kiwira na shughuli za kiuchumi zimesimama kutokana na mto Kiwira kufurika na kumwaga maji mara kwa mara hasa nyakati za mvua, hivyo tunaiomba Serikali iharakishe ujenzi wa barabara mbadala,” anasema.
Akitoa maoni kuhusu upatikanaji wa meli hizo, mdau wa maendeleo wilayani Kyela, Sebastian Huruma, anasema Serikali imeanza kufanya kwa vitendo katika ukuzaji wa uchumi kwa kutengeneza meli hizo tatu, ikiwa na kuboresha miundombinu hiyo ya barabara.
“Kama haya yatafanyika milango ya fursa itafunguka, wananchi watafanya biashara na vipato vyao vitaongezeka kwani gharama ya uendeshaji, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Mdau huyo anasema viwanda vya uzalishaji pamoja na makampuni ya usambazaji yamekuwa yakitumia usafiri wa magari kusafirisha bidhaa pamoja na malighafi mbalimbali hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na kwamba wamekuwa wakitumia gharama kubwa katika upande wa mafuta.
“Tukiachana na utumiaji mkubwa wa fedha pia usafirishaji huo umekuwa ukichukua muda mwingi lakini endapo meli hizi zitakamilika na kuanza kufanya kazi, kampuni zitapunguza gharama pamoja na kufanikiwa kuwafikishia wananchi mahitaji yao kwa wakati mwafaka,” anasema Mwaruma.
Anasema safari iliyokuwa ikitumia siku nne kwa kutumia gari, kwa meli itakuwa ikitumia siku moja tu hivyo Serikali imefanya jambo la maana na kwamba inahitaji kupongezwa.
Hata hivyo, anasema mahitaji ya meli hizo kwa Watanzania na raia wa Malawi ni makubwa, hivyo ni vema zoezi hilo likakamilika kwa muda mwafaka.