28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MKWELA, MSOMI ALIYEJIKITA KWENYE FANI YA UFUMAJI

Na MWANDISHI WETU

NI vigumu kuamini kwamba, msomi wa kiwango cha elimu ya uzamivu (falsafa au PhD) anaweza kuacha kazi ya kufundisha vyuo vikuu na kujikita katika masuala ya ujasiriamali mdogo kabisa ambao  unafanyika katika mazingira yasiyotarajiwa, chini ya mti na kuchanganyika na walalahoi wanuka jasho.

Daktari Hawa Mkwela ambaye ni mhitimu wa elimu ya falsafa kutoka katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha nchini Norway, ameanzisha kikundi cha akinamama cha ujasiriamali huku akianza na majirani zake akiwa na malengo ya kumkomboa mwanamke wa Kiafrika kutoka katika lindi la umasikini.

Falsafa ya mwanamama huyu jasiri ni kuwa, elimu bila matokeo ni kazi bure. “Lengo langu hasa la kuanzisha kikundi cha akinamama ni kwa ajili ya kumkomboa mwanamke ili aondokane na umasikini kutokana na kwamba wanawake wengi wamekosa fursa mbalimbali ingawa wao ndio walezi wa familia zetu,” anasema.

Dk. Hawa anasema mradi wake wa kufundisha akinamama kazi ya ufumaji utawasaidia katika kujiongezea kipato cha familia zao.

“Kazi ya ufumaji unaweza kuifanyia nyumbani hata kama utakuwa umepumzika. Ni kazi ambayo inaweza kuwakomboa wanawake wengi ambao muda mwingi wanakuwa majumbani mwao wakilea familia,” anasema.

Mradi wa ufumaji ni miongoni mwa miradi mbalimbali ambayo mwanamke huyu msomi anatarajia kuifanya chini ya shirika lake alilolianzisha mapema mwaka huu lisilo la kiserikali linaloitwa A Kid In Net (AKINI). Shirika hili pamoja na mambo mengine linajihusisha na masuala mbalimbali kama haki za watoto, elimu ya afya kwa wanawake na watoto, uwezeshaji kwa wanawake, elimu ya bima na masuala ya haki za kibinadamu.

“Tangu nianzishe mradi huu kuna faida kadha wa kadha kikundi chetu kimepata. Tumeweza kushiriki katika maonyesho mbalimbali ya hapa nchini na tunatarajia kuhudhuria maonyesho ya sabasaba ya mwaka huu ambapo tunatarajia kupeleka bidha zetu zilizotengenezwa na akinamama wa kikundi,” anasema.

Mkwela anasema akinamama wengi tangu aanzishe kikundi chake wameonesha nia ya kujiunga na watu wengi wameanza kuzitafuta bidhaa zake.

“Bidhaa zetu zimevutia watu wengi na sasa hivi tumeanza kupokea simu kutoka sehemu mbalimbali hapa Da es Salaam ambako watu wanapenda kuja kujifunza katika kikundi chetu,” anasema.

Anasema pamoja na mafanikio madogo waliyoyapata, kikundi bado kinapitia katika changamoto mbalimbali ambazo ili kiweze kufikia malengo ni muhimu kwa Serikali kuangalia namna ya kukiwezesha.

“Mimi nimeamua kufanya jambo hili. Ninapenda kuona akinamama wanaondokana na umasikini, hivyo ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba akinamama wanawezeshwa, wanawekewa mazingira rafiki ya kufanya shughuli za ujasiriamali na mazingira mazuri ya kupata mikopo,” anasema.

Dk. Hawa anasema kwa sasa anatarajia kuzindua mradi wa kuhakikisha kwamba wanawake wa kikundi chake na familia zao hasa watoto wanapata bima ya afya na anatarajia kuzindua pia elimu ya kusafisha kinywa kwa watoto wa familia wanakotoka wanakikundi.

Bidhaa zinazotengenezwa na akinamama hao ambao wamepiga kambi katika nyumba ya Dk. Hawa Mkwela katika maeneo ya Mbezi Luisi Mkoa wa Dar es Salaam, ni pamoja na mito, sketi za watoto, vilemba shingo (scarfs), mabegi, vitambaa mbalimbali  na karibu mahitaji  yote ya mwanamke vikiwemo pia mavazi ya kiume.

“Bidhaa zetu zinatengenezwa kutokana na ubunifu wa hali ya juu. Hatutumii bidhaa yoyote ya kuagiza kutoka nje. Kila kitu tunakinunua hapa hapa nchini. Na ninapenda Watanzania na Waafrika kwa ujumla kupenda bidhaa zetu na shughuli zetu, nafahamu kabisa watu wengi wameacha ufumaji kutokana na bidhaa nyingi kutoka nje. Ufumaji ni mali, ni kazi hivyo nawashauri wanawake wenzangu wajikite katika shughuli hii watapata pesa na kujiongezea kipato,” anasema.

Nchini Tanzania wanawake wengi  hasa wajasiriamali wamekuwa wakikumbana na chanagmoto mbalimbali ikiwemo mitaji, mazingira mabaya ya kufanyia shughuli zao na hasa suala la kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha likiwa ndicho kikwazo kikubwa. Lakini tunaamini kwamba kama Serikali itaboresha na kuwekeza katika kusaidia nguvu ya mwanamke na kumwezesha, basi taifa letu litapiga hatua kubwa katika masuala ya maendeleo.

Mwisho……..

Dk Hawa Kwela akimuonyesha mmoja wa akinamama ambaye ni mwanakikundi chini ya asasi isiyokuwa ya kiserikali ya  A Kid In Net (AKINI) namna ya kuanza kufuma kitambaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles