25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MDOLWA: NILIJIFUNGIA NDANI KUWAKWEPA WATAKA RUSHWA


Na EVANS MAGEGE -

Edmund Mdolwa mbali ya jina lake kufahamika vyema kwenye nafasi za utendaji serikalini na taasisi binafsi za ndani na nje siku za nyuma, jina hilo limerejea kwa kishindo katika ulingo wa siasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi –CCM.

Hivi sasa Dk. Mdolwa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa chama ngazi ya Taifa baada ya kurithi kwa mtangulizi wake Abdallah Bulembo.

Nyakati mbalimbali za chaguzi jina lake lilipata kusikika hususan wakati wa michakato ya ubunge katika Jimbo la Korogwe vijijini.

Gazeti hili limepata wasaa wa kufanya naye mahojiano maalumu nyumbani kwake Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

Pamoja na mambo mengine ameelezea uamuzi wake wa kujifungia ndani ili kukwepa vishawishi vya kutoa rushwa wakati wa kampeni za kuwania nafasi hiyo aliyoitwa hivi karibuni.

Endelea kufuatilia mahojiano haya…

MTANZANIA Jumapili: Umepata dhamana ya kuongoza Jumuiya ya Wazazi ambayo ni moja ya nguzo muhimu za CCM na umepokea kijiti hicho kutoka kwa mtangulizi wako, Abdallah Bulembo, umejifunza nini kutoka kwake?

Dk. Mndolwa:Kwanza niseme kwa uwazi kuwa ni heshima kubwa sana kwa wanajumuiya kunipa dhamana ya kuongoza taasisi hii kubwa na nyeti pia ni taasisi ambayo ni mtoto wa kwanza wa  TANU kabla ya kuwa CCM.

Taasisi hii ni muhimu sana kwa maendeleo ya chama na nchi kwa ujumla. Kwa hiyo kama ulivyoniuliza nimejifunza nini kutoka kwa Bulembo.

Kwanza tuanze pale mwanzoni alipopewa Bulembo maana na mimi nilikuwa kwenye kamati yake ya utekelezaji.

Bulembo alipochukuwa madaraka haya, Mwenyekiti mstaafu, Jakaya Kikwete alimwambia kuwa taasisi hii ilikuwa ifutwe na kwamba ajenda ya kufutwa ipo, wewe tuambie tunasababu gani ya kuendelea na jumuiya hii?. Kwa hiyo Bulembo alichukuwa taasisi ikiwa mufilisi, ikiwa ICU, hoi bin taabani kwa kila kitu.

Ameniachia mahali pazuri sana, ameniachia vifedha kidogo benki ambavyo  tunaweza kuvitumia kutoa kero za hapa na pale.

Tuna mwendelezo wa shughuli zetu za kimaadili ndani ya jumuiya, tumerudisha treni mahala pake, hapa ndipo alipotuacha.

Ukiniuliza nimejifunza nini kutoka kwake, kwanza kutokata tamaa kama kuna matatizo makubwa. Nisikate tamaa kwa sababu unaweza kuhuisha, unajua Bulembo ana nguvu kubwa sana ya ushawishi.

Bulembo ni Bulldozer, akiamini chake kitakwenda tu, atakisimamia na haogopi hivyo vyote nimejifunza kwake.

Pia, nimejifunza kwake kuwa ni mtu mzuri  na mwema na anapenda kusamehe na haya nimejifunza ndani ya miaka mitano ambayo nimekuwa naye karibu, kwa sababu kuna watu walivurugavuruga na wengine tukawatoa kwenye baraza lakini baadaye walivyoomba msamaha akawasamehe.

Kwa hiyo nina changamoto kubwa kwa sababu mwenzangu ameishaniweka kwenye reli, treni sasa halipo chini, sasa tutaliendeshaje hii ndiyo changamoto kubwa niliyonayo lakini nimejifunza mambo mengi sana kutoka kwake.

MTANZANIA Jumapili: Nini kilikusukuma kuwania nafasi hiyo ya juu kisiasa?

Dk.Mndolwa:Unajua kila kiongozi anayewania nafasi ana sababu zake, sababu yangu kwanza naielewa jumuiya vizuri sana, naelewa changamoto zake, naelewa tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi.

Naelewa mchango wa jumuiya kwenye chama na nchi yetu. Kwa hiyo nimeingia kwa sababu nina hakika nina mchango muhimu wa kuleta maendeleo kwenye jumuiya hii na chama kwa ujumla.

Mimi ni mstaafu, nimestaafu nikiwa na miaka 60 na sasa nina miaka 68. Katika taaluma yangu ya uhasibu na utawala wa fedha na uchumi nimeishafikia mwisho na kilichobaki kutoka kwangu ni kurudisha shukrani kwenye jamii, chama na nchi yangu.

Wasambaa tunaita “kuuza kome” yaani narudisha shukrani nyumbani na nina hakika ndani ya miaka mitano nitaweza kuweka misingi  kwanza ya kuendeleza tulichoachiwa.

Pili kuboresha jumuiya yetu ifike mahali ambapo watu wasizungumze tu kwamba jumuiya haitafutwa bali wazungumze kwamba igeni kutoka kwa jumuiya yetu, hiyo ndiyo nia yangu kuwa tuifikishe jumuiya mahali ambapo itakuwa ni jumuiya ya kuigwa, tutegemewe sisi na CCM kwa mambo yote ya kisiasa, kiuchumi na kila kitu.

MTANZANIA Jumapili: Unadhani  Jumuiya ya Wazazi ina umuhimu wowote kwa siasa za sasa zinavyoendeshwa nchini?

Dk. Mndolwa: Tuna umuhimu mkubwa sana. Unajua sisi katika jamii yote tupo kila mahali, kutoka juu mpaka chini, kutoka Dar es Salaam mpaka ngazi ya kitongoji cha mwisho unachokijua wewe.

Na hao wote wanahitaji mwongozo wa kuelekezwa  maendeleo, wanahitaji kero zao zitatuliwe.

Kwa sababu tupo kila mahali kwa wananchi wa Tanzania, ninaweza kusema tunahitajika sana. Sisemi tupo wenyewe, UVCCM nao wako kila mahali, UWT nao wako  kila mahali na chama chote kipo katika jamii lakini kumbuka sisi ni wazazi ambao tunajumuisha wote hawa.

Utaona mfumo wa UVCCM una ubaguzi fulani kwa maana ukifikisha miaka 36 na kuendelea huwezi kuwa ndani ya jumuiya hiyo.

Najua wamo wenye zaidi ya umri huo lakini hawawezi kufika mahali kwa sababu kuna sehemu kubwa ya wananchi ambayo wao hawawezi kuwa ndani UVCCM, UWT pia usipokuwa mwanamke maana yake wewe hauwezi kuwa UWT, sisi awe UVCCM akisema kuanzia miaka 36 anaweza kuja kwetu hata kama hajafikisha umri huo, wanawake pia wanaruhusiwa kuja kwa hivyo tuna umuhimu mkubwa sana .

Tupo sehemu ambayo haiwezekani tuachwe la msingi ni kujionyesha tu kwamba sisi tuna umuhimu na hiyo ndiyo kazi yetu kubwa.

MTANZANIA Jumapili: Siasa za mtandao ndani ya CCM zinatajwa kuchukuwa nafasi kubwa na kwa muda mrefu kuanzia uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi nchini(1995) na zinatajwa pia kuwa ndizo zilizaa Rais wa nchi hii wa awamu ya nne. Kwa mtazamo wako siasa za mtandao wa urais zilikufundisha nini na unazitathimini vipi, Je zinaweza kujenga au kuimarisha maisha ya baadaye ya chama?

Dk. Mndolwa: Siasa za mtandao zilimsaidia aliyeziweka wakati ule kushinda. Kwanza kilikuwa ni kitu kipya kwa hivyo mtandao ule kwa maana ya wale watu waliohusika kuuendesha uliwasaidia.

Unajua kama shilingi ina pande mbili na kila kitu kina faida zake na hasara zake. Siasa za mtandao zilikuwa ni kundi, pamoja na kufanya siasa lakini lile ni kundi na katika chaguzi zote inafahamika chaguzi ni makundi kushindana.

Huwezi kusema unafanyika uchaguzi kusiwe na makundi, unaweza ukawa na kundi lako ambalo umelishawishi kuwa wewe ndio bora lakini utaona chama chetu kina haribiwa na makundi huo ndiyo upande wa pili wa shilingi.

Ukiendeleza makundi baada ya uchaguzi ndio tatizo linapoanzia, ile filosofia ya kuendeleza makundi kwa kusema sisi ni watu wa fulani ndiyo inatuumiza.

Utaona viongozi kila siku wanasema vunjeni makundi  lakini siasa ya mtandao ni kundi ambalo kulivunja ilikuwa ni matatizo, hata huyo liliyemsaidia ilikuwa tatizo kwake.

Kwa mfano mimi kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, kuna walionipigia kura na wengine hawakunipigia lakini wote ni wangu.Sasa lile kundi langu likiendeleza wale wengine watafanyaje? Kwa hiyo hilo ndio tatizo la mtandao, watu wanataka wanayoyataka, ukiwanyima wanakulaumu, unakuta wengine wanataka kuwa ma-DC, RC na unapowanyima kwa maelezo ya kwamba hawana vigezo wanakulaumu na hapo unakuwa hasi kwao.

Mtandao kwa maana ya kundi kama makundi mengine na siasa yetu ya chama hautakiwi, tunataka tubakiwe na kundi moja tu linaloitwa CCM. Kulipata kundi linaloitwa CCM baada ya uchaguzi ni vigumu lakini ni lazima lipatikane.

Popote pale ambapo wapinzani wameshinda ni kwa sababu CCM wameshindwa kuvunja makundi yao. Kwa swali hili la mtandao majibu yake ni hayo kwamba limemsaidia aliyelianzisha wakati ule lakini baada ya hapo kulivunja imekuwa ni shida kwa hiyo limeanza kula kwetu sasa, watu wanazira sasa, katika kuzira huko wapinzani wanapata nguvu.Kwa hivyo siasa ya makundi iishe baada ya uchaguzi.

MTANZANIA Jumapili: Katika harakati zako za kisiasa ndani ya CCM, unadhani siasa za mtandao zimewahi kukuumiza?

Dk. Mndolwa:Hilo ni swali gumu sana kwa sababu kwanza hunijui nilikuwa kwenye mtandao au sikuwa kwenye mtandao.

Lakini kama ulivyosema kama siasa ya mtandao imeumiza CCM, hii ni kweli nakwambia na siasa ya makundi yoyote lazima ikiumize chama husika.

Hata Chadema wakiwa na makundi lazima waparaganyike ndio maana kuna kuwa na matatizo, makundi yao wanayaendeleza  ndiyo maana nao wanaumia.

MTANZANIA Jumapili: Kuna ukweli wowote kuwa siasa za mtandao ni rafiki wa vitendo vya rushwa?

Dk. Mndolwa: Mtandao kama nilivyosema awali ni kundi, rushwa ni kitu kingine kabisa, huwezi kusema kwamba mapadri wote ni wacha mungu kiasi  kwamba hawatendi dhambi.

Rushwa ni hulka ya mtu, mtu aliye ndani ya mtandao anaweza asipende vitendo vya rushwa na mtu asieyekuwa ndani ya mtandao akawa anapenda rushwa.

Kwa hiyo rushwa ni kitu kingine tofauti kabisa, lakini unaweza ukasema kuwa mtandao ni rushwa mojawapo kwa sababu kuwa na kundi ni kumshawishi mtu aungane na wewe sasa inategemea unamshawishi kwa njia ipi, ya mdomo tu au ya fedha?. Kwa hivyo hisia ya rushwa katika njia ya kumshawishi mtu kuungana na kundi na kama unamshawishi mtu kwa njia ya fedha hapo ndipo unaleta tatizo jingine la rushwa.

Unajua siasa ya kupigiwa kura inategemea nguvu ya hoja na hiyo nguvu ya hoja ndiyo tumeiona kwenye uchaguzi wa mwaka huu ndani ya CCM, binafsi nimeshinda lakini nilitumia nguvu ya hoja zaidi. Na watu waliotafuta ushawishi kwa kutoa fedha  katika uchaguzi huu wameumia.

Kwa hiyo rushwa ni kitu tofauti lakini watu wanaitumia kushawishi ingawa unaweza kutumia ushawishi wa nguvu ya hoja kuungwa mkono na kupigiwa kura.

MTANZANIA Jumapili: Umepata kuwa mmoja kati ya wasaidizi wa Bulembo, ni kitu gani ulikuwa hupendezewi nacho ndani ya jumuiya kupitia uongozi wake?

Dk. Mndolwa: Vitu vizuri vyote havikosi kasoro, hakuna kitu kizuri chochote ambacho hakipaswi kuboreshwa, hata mke mzuri ukimuoa utakuta kuna vitu ambavyo inabidi umboreshe.

Kwa hiyo kuna vitu vingi vya kuboresha hapa. Naweza kusema sisi katika uongozi wa Bulembo tulikuwa na malengo mengi lakini hatukuyakamilisha yote na haiwezekani ukamilishe malengo yote.

Unajua hii ina kwenda kwenye filosofia ya taasisi kuna kitu kinaitwa, vision na mission. Katika mission tunasema nataka tuwe kitu fulani lakini hamuwezi kufikia hapo.

Kwa hiyo kwa kifupi tulikuwa na malengo mengi na ninaweza kusema tumekamilisha malengo kwa asilimia 85, zile asilimia 15 ndizo mimi naanzia hapo. Kwa hiyo nina ajenda kamili kabisa kwamba asilimia 15 ile hatukuikamilisha lazima niikamilishe.

Wakati wa Bulembo kulikuwa na ajenda ya kufutwa au kutofutwa, ile ajenda imekwisha sasa hivi kuna ajenda mpya inahusiana na hiyo ambayo inaitwa kujitegemea.

Hii ni ajenda kubwa sana, pia kuna ajenda nyingine nyingi  kwa maana kuna ajenda mama, ajenda mtoto zote zina umuhimu ajenda kubwa ni kujitegemea.

MTANZANIA Jumapili: Nini siri ya ushindi wako na kwanini wasiwe wengine?

Dk.Mndolwa:Nimeshinda kwa sababu, kwanza mimi ninavyoona na nilivyosikia kwenye redio Kariakoo zinaitwa hivyo , kwamba  Mndolwa kwenye jumuiya anafahamu tunatoka wapi na tunakwenda wapi.

Katika wenzangu wote nilioshindana nao ni mimi peke yangu ambaye nina ‘institution memory’ ya jumuiya ni kama wanajeshi wakienda vitani, si kwamba wakifika pale wanaanza kujifunza bunduki, risasi inawekwaje, pori nalo liko wapi tunajifichaje, hapana ninajua pa kwenda.

Nadani hiyo ni dhana mojawapo ambayo imenisaidia kwamba nina uzoefu kuliko wenzangu niliopambana nao.

Pili, nadhani sifa zangu mwenyewe kama ukizichunguza.  Hata hivyo swali hili ingekuwa vizuri kumuuliza mpigakura wangu mimi najiona hivyo, ujue kuna miono mitatu.

Ninaweza kujiona mwenyewe, jamii inavyoniona na Mungu anavyoniona. Sasa hapa nasema mimi kwa jinsi ninavyojiona na si kufikiria wenzangu wananionaje, kwamba uzoefu na ujuzi wangu. Watu wengine wameweza kusema kwamba nimependelewa, lakini kama ukimpendelea mtu kwa sababu ya uzoefu na ujuzi wake si vibaya kwa sababu ukinipigia kura maana yake umenipendelea kuliko mwingine.

Kwa hiyo si dhambi kupendelewa kwa mantiki hiyo nadhani ujuzi na uzoefu wangu ndio umenisaidia kushinda kwa sababu nimekuwa kiongozi katika jumuiya, katika chama kwa miaka mingi.

Nimeanza chini, nimeanza ngazi ya wilaya kuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya, mjumbe wa kamati ya siasa, mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya kwa miaka zaidi ya 15, nikaja katika ngazi ya mkoa, nimekuwa mwenyekiti wa wazazi mkoa, nimekuwa mjumbe wa kamati ya siasa ya wazazi , nimekuwa muweka hazina wa chama kwa muda wa muhula mmoja ngazi ya Taifa, nimekuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya Taifa, nimekuwa mjumbe wa Nec lakini wenzangu wengine wote hawakuwa na sifa hizo.

Kwa hiyo wanajumuiya wakati wanapiga kura waliliona hili, hawakuona kwa nafasi hii kumpa mtu wa kujifunza. Sababu naweza kusema ni taaluma yangu. Mimi ni mchumi, shahada yangu ya kwanza ni mhasibu, shahadha ya udhamiri ni ya masuala ya kibenki na udhamivu wangu ni kwenye maswala ya fedha hivyo nauzoefu wa kuendesha taasisi mpaka umri wangu wa kustaafu ulipofika.

Ninapenda kusema kwamba wenzangu wote niliopambana nao wanafaa kwa sababu wamechujwa, wamepita michujo yote na yeyote kati yetu angefaa kuendesha hii jumuiya lakini unajua watu wanaofaulu mtihani  unaweza kuwaambia kiwango cha ufaulu  ni kutoka 50 mpaka 100, sasa kama mimi nimepata 95 kwanini nisichukuliwe  achukuliwe wa 50?.

MTANZANIA Jumapili: Rushwa mara nyingi inatajwa kutawala kwa kiasi kikubwa hasa unapofikia wakati wa chaguzi za ndani za CCM, vipi kwa upande wa jumuiya yenu uchaguzi wa mwaka huu hali ya rushwa ilikuwaje?

Dk. Mndolwa:Kwanza nasema rushwa ni kitu ambacho mimi nimekiandikia mambo mengi sana hasa kwenye ngazi ya kimataifa nimeandika mambo mengi yanayokosoa  na kueleza madhara ya rushwa.

Kwa hiyo rushwa ni kitu ambacho unaweza kusema ni seli ndogo yenye uwezo mkubwa wa kuharibu mwili wote na kuua. Kansa ni seli  ndogo sana, ujue binadamu  ana seli karibu trilioni11 lakini seli moja kati ya hizo inaweza kukuua kwa sababu inaweza kuziambukiza seli zote  na mfano huo ndio rushwa.

Kidhati naichukia rushwa  na ninajua ndiyo itatuumiza kama tusipoikataa. Kwa hiyo kama ulivyouliza swali, nataka kusema katika awamu zote za nyuma katika chaguzi zetu na si kwa jumuiya peke yake bali siasa za nchi yote kulikuwa na rushwa iliyoanza kidogo kidogo.

Nimeanza siasa za kuwania uongozi mwaka 1995 na wakati huo sikutaka kuwania ubunge, ila dhamira yangu ilikuwa ni kumpata mbunge huko Korogwe vijijini ana ubora wa kutosha na atatupeleka mbele.

Nakumbuka rushwa ya wakati huo kama unaweza kuitafsiri ni rushwa ilikuwa  ni soda na kreti lilikuwa linauzwa Sh.4,500 unaita wazee tunazungumza. Sasa kama unaweza kuita hiyo ni rushwa sawa sasa rushwa ya siku hizi, rushwa ya mwaka 2015 ilikuwaje, watu wote wanajua jinsi ilivyokuwa kubwa.

Halafu hakuna mtu aliyetarajia Magufulia (Rais) angeshinda, hakuna hata mmoja hata mimi sikutegemea kwa sababu kulikuwa na ushindani wa rushwa ya hali ya juu, wanaotia nia walikuwa ni watu wenye hela lakini kwa bahati nzuri  Mungu  naye ndiye anayechagua kiongozi.

Ilikuwa kwamba wakubwa wanapigana upande wa kulia  na kushoto, Mungu naye akamwongoza huyu Daudi akaenda kupigana na Magoriati, kapenya mpaka akashinda na kwa mujibu wake yeye  anasema hakutumia shilingi hata moja.

Kwa hivyo kwa uchaguzi wetu wa jumuiya nilichokifanya  Dodoma, sikuzunguka hata siku moja kwenda kuomba kura usiku kwa sababu nilijua kuwa sitatoa rushwa lakini hiyo haikutosha  kuonekana kutotoa rushwa. Lakini ukizunguka utaombwa hela na ukiombwa hela utatoa tu,sasa nikajiuliza kutoa hela tatizo na usipotoa tatizo kwa hiyo sikuona umuhimu wa kuzunguka usiku.

Kwa hiyo nilikuwa na kaa ndani ikifika jioni naenda pale CCM makao makuu naomba  kura ikifika saa 12 jioni narudi kujificha na kesho nafanya hivyo hivyo. Kwa msingi huo sikuona vitendo vya rushwa, kwangu mimi uliza watu wanajua vizuri sikutoa senti hata moja na nimelaumiwa sana na watu na zile kura nilizozipata labda zingeongezeka kama ningeenda kuomba kura lakini hatari ambayo ningechukuwa kwa kuomba kura kwa rushwa ilikuwa ni kubwa sana. Kwa hiyo nilikuwa najificha, watu hawakufahamu naishi sehemu gani, wakinipigia simu mimi namuomba kura akiniuliza sababu za mimi kutokwenda kupiga kampeni namwongopea kwa kweli Mungu anisamehe kwa sababu za uongo niliowaongopea walionipigia simu.

Nataka nikwambie kwamba huko nyuma nimegombea ubunge lakini sikushinda kwa sababu sikutoa rushwa.

Sasa watu wa Korogwe vijijini wanasema jiwe waliloliacha waashi sasa hivi limekuwa jiwe la msingi, mimi sasa ni mjumbe wa kamati kuu, kwa hiyo kwa uchaguzi huu ni mara ya kwanza nimepata wakati sikutoa rushwa. Kwa hiyo nashukuru sana awamu hii kuonyesha kwa vitendo kupambana na rushwa na tukiendelea hivi kwa kumsaidia Rais wetu kwenye ajenda hii ya kukemea rushwa nchi hii itafika mbali.

MTANZANIA Jumapili: Una kipya gani ndani ya uongozi wako?

Dk. Mndolwa: Kwa kauli moja ninaweza kusema kwamba katika uongozi wangu nitamagufulisha jumuiya ya wazazi. Hii ni ajenda kubwa sana ambayo nakwenda kuiendesha ndani ya jumuiya yetu.

MTANZANIA Jumapili: Mali za Jumuiya  ya Wazazi wa CCM zinadaiwa kuyeyuka ama kupotea, pia faida ya mali zilizopo inatajwa kuwa ni kidogo na sehemu kubwa ya faida hiyo inaishia mikononi mwa watu binafsi, unadhani hali hiyo imetokana na nini?

Dk. Mndolwa: Mimi ni mwalimu wa utawala bora, ukiulizwa swali kuwa taasisi imekwenda kombo kwa kiasi gani unaweza kusema kwamba utawara bora kidogo umeteteleka.

Na jibu linaweza kuwa sahihi.Katika utamaduni wetu wa jumuiya huko tunakotoka, shule zetu ambayo ndio mali kubwa tuliyonayo, kwa mtazamo halisia zilikuwa shule za wazazi lakini undani wake zilikuwa ni shule za walimu.

Walimu wakuu ndio waliokuwa wanaendesha shule hizo na ilifikia hatua hiyo kwa sababu ya utamaduni.Taasisi ikiwa na utamaduni mbovu lazima utamaduni huo uiumize taasisi lakini kama ina utamaduni mzuri lazima taasisi iinuke.

Utamaduni wetu huko nyuma viongozi wetu wetu wanapita shuleni huko, mara wanachukua milioni mbili hapa shule ile anachukua milioni tatu, mwalimu naye akiona hivyo naye anachukuwa zaidi  na ukimuuliza anasema zote zimachukuliwa na bwana mkubwa, sasa hapakuwa uwajibikaji  kwa hivyo unakuta mwalimu akishamaliza mwaka mahesabu yake hayaonyeshi kama kuna gawio  na kadhalika, kwa hiyo zilikuwa ni shule za walimu wakuu.

Nataka nikwambie, shule hizi kuonekana ni za jumuiya alianza Bulembo, binafsi nilichaguliwa na Bulembo katika kamati yake ya utekelezaji kuwa mwenyekiti wa kamati ya elimu, nikazungukia shule si zote lakini nyingi nikajionea matatizo makubwa.

Nikupe mfano mmoja kuna mwalimu kule Mbeya sitaki kumtaja jina, ameacha kazi kwenye shule yetu lakini amefungua shule zake mbili, sasa jiulize fedha kapata wapi.

Kwa hiyo kama ulivyouliza ni kweli mali zetu nyingi zimeibiwa, na Bulembo kajitahidi kurudisha treni kwenye reli kwa hiyo mimi najukumbu kusukumba mbele malengo yetu.

Si shule tu, pia tuna viwanja nako kuna changamoto kubwa, nakumbuka Bulembo alipoingia kulikuwa na hati miliki 18 na sasa hivi  tuna hati miliki 56 na bado katika changamoto zangu nilizonazo ni kupata hati miliki, piga uwa galagaza lazima tupate hati miliki za viwanja vyetu.Pia tunaamiwa kuwa tuna maeneo ambayo naambiwa yana mali chini ya ardhi. Hivyo nia yangu ni kuhakikisha tunayapatia maeneo yetu hati miliki kwa sababu ukishakuwa na hati miliki maana yake una fedha mfukoni.

MTANZANIA Jumapili: Rais Magufuli ameiagiza jumuiya kusimamia maadili hasa kuhusu mavazi akielekeza kwa wanaovaa nusu utupu umejipanga kutimiza agizo hilo na unalianzia upande gani?

Dk. Mndolwa: Kuanzia Februari mwakani tunaanzisha ajenda ya maadili katika shule zetu.Januari mwishoni tutakuwa na semina ya walimu wa shule zetu kuzungumzia maadili pekee.

Ni tumaini letu walimu wakitoka watakwenda kusimamia na kutekeleza walichojifunza na upande wetu viongozi tutakuwa tunawatathimini kila baada ya miezi mitatu.

Pia tutakuwa na mpango wa kufundisha viongozi na sisi viongozi tutakwenda kufundishwa Ihema kilipo chuo chetu cha chama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles