24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

RUSHWA YA NGONO, UKEKETAJI KUPATIWA DAWA 2018


Na JOHANES RESPICHIUS, DAR ES SALAAM -

WANAHARAKATI ngazi ya jamii kutoka Kituo cha Taarifa na Maarifa Kipunguni, Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, wamezindua kampeni ya kupinga rushwa ya ngono na ukeketaji kwa mwaka 2018.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo imefadhiliwa na Shirika la Women Fund Tanzania (WFT), Mwenyekiti wa Mtaa wa Amani, Dani Maragashimba, aliwataka wananchi katika mtaa wake kuhakikisha kila mmoja anasimama katika nafasi yake kukomesha vitendo vya ukeketaji na rushwa ya ngono.

Mbali na kutoa wito huo, alisema atasimama kidete pamoja na wanaharakati hao katika kupinga vitendo hivyo vya ukatili na ili kumfanya mtoto wa kike kupata furaha sawa na anayoipata mtoto wa kiume ikiwa ni pamoja na kupata elimu.

“Lengo ni hadi kufikia Desemba mwaka 2018, tusisikie kunaripotiwa vitendo vyovyote vya rushwa za ngono maofisini na mitaani ikiwa ni pamoja na ukeketaji watoto wa kike na udhalilishaji wa kijinsia,” alisema Maragashimba.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho, Seleman Bishagazi, alisema wameamua kuanzisha harakati hizo mapema kutokana na kwamba shughuli za ukeketaji hufanyika katika miaka inayogawanyika kwa mbili.

Alisema wanaamini kama wazazi na watoto watakuwa na uelewa wakutosha kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili wa kingono na ukeketaji, itasaidia kujua namna ya kukabiliana navyo pale vinapotokea kwenye jamii.

“Tunaamini mzazi akijua maana na madhara ya rushwa ya ngono, itakuwa rahisi kumwelimisha mwanawe na lengo letu ni kuona watoto wajue madhara ya jambo hili wakiwa wangali wadogo kwani hata wakienda shuleni, vyuoni na maofisini watakuwa wanajua namna ya kukabiliana na vitendo hivyo.

“Suala la ukeketaji sisi kama wanaharakati ngazi ya jamii tumekuwa tukifanya jitihada kubwa kupambana na suala hili hasa ukilinganisha kila mwaka unaogawanyika kwa mbili ndio watoto huwa wanakeketwa.

“Kesi ambazo tumekuwa tukikimbizana nazo kwa kuwakamata wazazi na mangariba wanaokeketa na kuwapeleka polisi mwisho wa siku zimekuwa zikiishia hewani kwa sababu zimekuwa zikikosa ushahidi kwani ni vigumu mtoto kwenda kuwatolea ushahidi familia yake,” alisema Bishagazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles