24.5 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO, MAPITO YA VIONGOZI AFRIKA 2017


NA MARKUS MPANGALA -

LEO tunaufunga rasmi mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka 2018.

Kama ilivyo miaka mingine iliyopita mwaka 2017 uligubikwa na matukio lukuki yaliyozitikisa duru za kisiasa katika nchi za Afrika.

Katika matukio hayo ambayo kimsingi yanagusia pia masuala ya kidiplomasia, watu kadhaa walipoteza maisha huku viongozi mbalimbali wakitikiswa kisiasa.

Miongoni mwa matukio hayo tukianzia Afrika Kaskazini nchini Libya, kulikuwapo na biashara haramu ya utumwa.

Morocco kurudishwa kwenye Umoja wa Afrika na baadaye kivumbi cha kuwania urais ndani ya chama cha African National Congress (ANC) kati ya Cyril Ramaphosa na Dk.Nkosozana Dlamini-Zuma.

Aidha, hofu ilitanda kuhusu afya ya Rais wa Nigeria Mohammadu Buhari.

Nchi ya Burundi kujitoa uanachama wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Uchaguzi nchini Kenya ulivyoibua utata hadi matokeo ya urais kufutwa.

Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni hakubaki nyuma katika kuukamilisha mwaka 2017, baada ya kuibuliwa kwa mpango wake wa kuichezea Katiba ya nchi hiyo kubadilisha kipengele cha umri wa urais.

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe aling’oka madarakani.

Kwa matukio zaidi ya mwaka 2017 Endelea kusoma makala haya…

Siku 50 zilipita kwa wananchi wa Nigeria bila kufahamu nini kinaendelea juu ya Rais wao Mohammadu Buhari aliyekuwa amelazwa nchini Uingereza kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Ndege ya Rais Buhari kwa kipindi chote alichokuwapo nchini Uingereza ilikuwa imeegeshwa katika Uwanja wa Ndege wa Stansted, mjini London, Uingereza na kuibua hofu kwa wananchi.  Maandamano yaliibuka kwa kile kilichodaiwa kuwa ni shinikizo la kutaka serikali itoe taarifa kuhusu kilichomkumba Rais wao.

Baada ya maandamano hayo ofisi ya rais nchini humo, ilitoa taarifa na kukiri kuwa ndege rasmi ya Rais Buhari ilikuwa imeegeshwa katika uwanja huo kwa muda wote.

Awali kulikuwapo na taarifa kuwa Pauni 4,000 zilikuwa zinalipwa kwa siku kama ada ya kuegesha ndege hiyo, hivyo kwa muda wote huo iligharimu pauni 200,000.

Hata hivyo msemaji wa Rais Garba Shehu, alikanusha taarifa hiyo na kueleza kuwa gharama za kuegesha ndege hiyo hazikuzidi pauni 1,000.

Buhari mwenye umri wa miaka 74 aliondoka nchini Nigeria Januari 19 mwaka huu, kwenda Uingereza kwa safari ya matibabu.

Katika kipindi chote alichokuwa nje ya nchi, Nigeria ilikuwa ikiongozwa na Makamu wake Yemi Osinbajo.

 

Upepo wa kisiasa ulimtikisa Rais wa Gambia Yahya Jammeh. Jabali hilo la kisiasa ameongoza nchi hiyo ndogo ya kwa upande wa Afrika Magharibi kwa mikono ya chuma kwa miaka 22, hadi alipopoteza nafasi hiyo kwenye uchaguzi wa rais mwaka 2016 kupitia mshindani wake Adama Barrow. Awali Jammeh alikubali matokeo kabla ya kubadilisha uamuzi hivyo kung’ang’ania madarakani.

Hata hivyo vikosi vya ECOWAS vilitumwa Gambia kumshawishi Jammeh kukubali kushindwa na ajiuzulu. Januari 2017 aliondoka na kwenda uhamishoni Guinea ya Ikweta, baada ya kuivuruga hali ya fedha ya nchi hiyo.

RAIS wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak aliyekuwa amepewa kifungo cha maisha jela kwa kuchochea mauaji ya raia wakati wa maandamano ya kumwondoa madarakani mwaka 2011, ameachiliwa huru mwaka huu.

Mubarak alizuiliwa katika hospitali ya kijeshi mjini Cairo, wakili wake aliviambia vyombo vya habari kuwa ameruhusiwa kurudi nyumbani kwake mjini humo.

Aliagizwa kuachiliwa huru Machi mwaka huu baada ya Mahakama ya Rufaa kumuondolea makosa ya kuwaua waandamanaji wakati wa maandamano dhidi yake 2011.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 88 aliingia madarakani mwaka 1981 baada ya mauaji ya aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Anwar Sadat.

Amekuwa akizuiliwa katika hospitali ya kijeshi ya Maadi tangu 2013 baada ya kuhamishwa katika eneo hilo kwa dhamana kutoka jela ya Torah.

Mubarak alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya kupatikana na hatia mwaka 2012 ya mauaji ya waandamanaji waliouawa katika mikono ya vikosi vya usalama Februari mwaka 2011.

Nako nchini Zimbabwe utawala wa miaka 37 ya Rais Robert Mugabe ulikoma mwaka huu. Rais Mugabe alitangaza kujiuzulu kutokana na majadiliano yaliyochochewa na jeshi la nchi hilo, lililofanya ‘mapinduzi baridi’. Jeshi hilo lilimweka Rais Robert Mugabe katika kizuizi cha nyumbani.

Mzozo wa Zimbabwe ulichemka zaidi baada ya Mugabe akumfuta kazi makamu wake Emmerson Mnangagwa ili kumweka mke wake katika nafasi ya kuwa mrithi wake. Mugabe alijiuzulu wakati mchakato wa kumwondoa madarakani ukitarajiwa kufanyika bungeni. Mkakati wa Mugabe uligonga mwamba hatimaye Mnangagwa aliteuliwa kumrithi.

Tuhuma za rushwa kwa wanasiasa ziliendelea kumtafuna Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma na kusababisha kupigiwa kura za kutokuwa na imani naye bungeni.

Tuhuma za rushwa zilihusu kampuni za kimataifa kwa kutoa hongo ili kupata zabuni au kandarasi za serikali. Uchumi wa nchi unaathirika huku viwango vya ukosefu wa ajira vikiwa takriban asilimia 30.

Katika hatua nyingine mchuano wa kambi mbili za wagombea urais wa ndani ya Chama cha ANC cha Afrika Kusini zilikataa kuweka tofauti zao kando ili kukilinda chama hicho ambacho kilikaribia kupasuka pande mbili.

Wagombea Cyril Ramaphosa ambaye ni makamu wa Rais wa sasa nchini Afrika Kusini na  Dk.Nkosazana Dlamini-Zuma ambaye ni mjumbe wa kamati ya ANC walikuwa katika mapambano makali ya kugombea nafasi ya urais kupitia ANC huku pande zote zikikataa kuweka kando tofauti zao kwa lengo la kuleta mshikamano pamoja na kulinda masilahi ya ANC wiki moja kabla ya mkutano mkuu wa chama hicho. Hata hivyo mshindi alikuwa Ramaphosa ambaye anatarajiwa kuwa rais wa nchi hiyo baada ya Jacob Zuma kung’atuka baadaye.

Waziri Mkuu wa Israel, Benyamin Netanyahu ameendelea kuishangaza dunia baada ya kuongeza kasi ya ziara zake barani Afrika. Mwaka huu alihudhuria sherehe za kuapishwa Rais Uhuru Kenyatta.

Licha ya kuhudhuria sherehe hizo, Netanyahu hakufika uwanja wa michezo wa Moi Kasarani uliotumiwa kumwapisha Rais Kenyatta.

“Tofauti na ilivyotarajiwa, baada ya kuwasili asubuhi na kupokelewa na viongozi wa serikali, Netanyahu alipangiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais Kenyatta katika ukumbi uliopo Ikulu, ambako kungekuwa na kikao pamoja na viongozi wengine 10 wa Afrika,” liliandika gazeti la Jerusalem Post.

Taarifa zilieleza kuwa Shirika la Kijasusi la Israel Shin Bet lilitoa sababu za kiusalama kutohudhuria sherehe hizo katika uwanja wa Moi Kasarani, badala yake alishauriwa kuungana naye kwa dhifa iliyoandaliwa Ikulu pekee.

Netanyahu alikutana na kufanya mazungumzo na marais 10 wa nchi mbalimbali barani Afrika, Salva Kiir (Sudan Kusini), Edgar Lungu (Zambia), Paul Kagame (Rwanda), Ismail Omar Guelleh (Djibouti) Ian Khama (Botswana), Hailemariam Desalegn (Waziri Mkuu wa Ethiopian), Yoweri Museveni (Uganda), na Ali Bongo (Gabon.

Wengine ni wawakilishi wa Umoja wa Afrika, Pierre Buyoya na Rupiah Banda, Balozi Maalumu kutoka Eritrea na Zambia,  Waziri Mkuu wa zamani wa Senegal, Aminata Toure, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina, na India, na Spika wa Bunge la Algeria.

Balozi Amina Mohammed wa Kenya alikuwa miongoni mwa wagombea nafasi ya Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, akichuana na wengine Moussa Faki Mahamat (Chad), Dk. Pelonomi Venson-Moitoi (Botswana), Agapito Mba Mokuy (Guinea ya Ikweta), na Profesa Abdoulaye Bathily (Senegal).

Katika uchaguzi huo mshindi ni Moussa Faki Mahamat raia wa Chad. Hata hivyo uchaguzi huo ulisababisha malumbano kati ya Kenya, Uganda na Tanzania. Kenya ililalamika kusalitiwa na majirani ambao walikanusha haraka madai hayo.

Faki hakuwa mwanasiasa mpya katika masuala ya Umoja wa Afrika, amewahi kuhudumu kama mwenyekiti wa baraza la bodi ya umoja huo ya uchumi, jamii na utamaduni kati ya mwaka wa 2007 na 2008.

Katika kinyang’anyiro cha ukuu wa Tume ya Umoja wa Afrika alipata kura 38 kwenye duru ya saba ya uchaguzi uliofanyika Januari 30, mwaka huu, na kutangazwa mshindi baada ya kupata theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa. Ili kutangazwa mshindi mgombea anatakiwa kufikisha kura 36.

Faki ni mwenyekiti wa tano wa Tume ya Umoja wa Afrika, na wa pili kutoka nchi za Afrika ya Kati baada ya Jean Ping wa Gabon aliyeongoza kati ya mwaka 2008 na  2012.

Uchaguzi nchini Kenya nao uliingia mizengwe na kulazimika Mahakama ya Juu zaidi nchini Kenya, kufuta matokeo yaliyompa ushindi wa asilimia 54 Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa awali uliofanyika Agosti 8 mwaka huu.Kesi ilifunguliwa na Raila Odinga aliyekuwa mgombea wa NASA.

Uamuzi wa mahakama hiyo ulisomwa Septemba 1, na majaji 6, hata hivyo majaji wanne walikubaliana na hoja zilizowasilishwa na walalamikaji wakati majaji wawili walikubali hoja za Tume ya Uchaguzi, Chama cha Jubilee na wanasheria wa Uhuru Kenyatta.

Mahakama  hiyo ilisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliendesha uchaguzi usiokuwa wa haki na zoezi la kukusanya matokeo halikufanywa kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo.

Jaji Mkuu David Maraga, Makamu wake, Philomena Mwilu, Jaji Smokin Wanjala, Isaac Lenaola waliafiki pingamizi lililowasilishwa na muungano wa upinzani kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na haki kwa mujibu wa Katiba. Jaji Njoki Ndung’u na Jackton Ojwang’ walipiga kura ya hapana dhidi ya pingamizi la NASA.

Majaji wanne walisema Tume ya Huru ya Uchaguzi na Mipaka imeshindwa kuthibitisha matokeo ya uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Uamuzi wa Mahakama ya Kenya ulitajwa kama uamuzi wa kijasiri na IEBC iliagizwa kuandaa uchaguzi mpya bila kuchelewa kama sheria inavyotaka.

Nchini Rwanda wananchi walitumia sanduku la kura na kumrejesha Rais Paul Kagame madarakani uchaguzi ulifanyika Agosti 4, mwaka huu.

Kagame anasifika kwa kuibadilisha Rwanda kutoka nchi isiyokuwa na bandari na kuwa nchi yenye uchumi mzuri, biashara, ajira na kupunguza umasikini.

Licha ya umahiri alionao Kagame analaumiwa kuwa ni kiongozi anayebana uhuru wa vyombo vya habari, pamoja na kutuhumiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya mauaji ya waliokuwa wapinzani wake kisiasa.

Matokeo ya uchaguzi ya mwaka huu yalipotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini Rwanda, yalionyesha Paul Kagame alishinda kwa asilimia 98. Kagame aligombea muhula wa tatu baada ya mabadiliko ya Kikatiba ya mwaka 2015.

Mabadiliko hayo yalilenga kumruhusu kugombea muhula wa tatu na vipindi vingine viwili vya miaka mitano. Hii ina maana Kagame ataruhusiwa kuwa madarakani hadi mwaka 2034.

Agosti mwaka huu wananchi wa Angola walipigakura za kumchagua rais wao baada ya Rais Jose Eduardo dos Santos kustaafu. Desemba mwaka 2016 Rais Santos alitangaza kuachia ngazi na kwamba hatagombea kwenye uchaguzi wa mwaka huu.

Matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa Agosti 25, mwaka huu yalionyesha kuwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Usalama, João Lourenco alishinda kiti cha urais.

Angola bado ipo chini ya mfumo wa chama kimoja cha siasa na imetawaliwa kwa muda mrefu na familia ya Santos. Uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa wa nne tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1975 kutoka kwa wakoloni Ureno.

Kushamiri biashara ya utumwa dhidi ya watu weusi nchini Libya nako kuliibuka na kuibua tafrani.

Jumuiya ya Kimataifa ililaani vikali vitendo na kusababisha Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Ulaya kuamua kwa kauli moja kuwa sakata la baadhi ya Waafrika kuuzwa kama watumwa linapaswa kutafutwa ufumbuzi kutokana na hali mbaya ya wakimbizi na ongezeko la wahamiaji wa Afrika kwenda barani Ulaya.

Mkutano wa tano wa viongozi wa Afrika na Ulaya ulifanyika mjini Abidjan nchini Ivory Coast, ambao waliamua kuwa suala la wakimbizi na wahamiaji wa Kiafrika linapaswa kupatiwa ufumbuzi wa kimsingi ikiwa ni pamoja na kupatikana suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Libya.

Pande hizo mbili zimetilia mkazo wa kuboreshwa hali ya wakimbizi nchini Libya na kuwasaidia kurejea makwao. Itakumbukwa kuwa mwaka huu zilisambazwa picha na video kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha raia wa nchi za Afrika wanaohamia kuelekea Ulaya wakiuzwa kama watumwa nchini Libya.

Miongoni matukio mengine ni suala la Serikali ya Burundi kugomea kutoa ushirikiano kwa wachunguzi wa uhalifu wa kivita kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai -ICC. Vitendo vya uhalifu dhidi ya ubinadamu vilidaiwa kufanywa na vikosi tiifu kwa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza dhidi ya wapinzani wa kisiasa vilichochea mahakama hiyo kuanzisha uchunguzi uliotekelezwa kati ya Aprili 2015 hadi Oktoba 2017.

Hata hivyo wataalamu walisema itakuwa vigumu mwendesha mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda kukusanya ushahidi pasipo kupata ushirikiano wa serikali ya Burundi ambayo mwaka huu ilikuwa ya kwanza kutangaza kujiondoa katika uanachama wa mahakama hiyo yenye makao yake makuu mjini The Heague nchini Uholanzi.

Duru za siasa ziliangazia katika Taifa la Morocco ambalo kwa kipindi cha miaka 33 lilikosekana katika uanachama wa Umoja wa Afrika,  baada ya viongozi kukubaliana na maombi yake licha ya kuendelea kuikalia Sahara Magharibi.

Wanachama wa AU walikubaliana kuwa suala la hadhi ya Sahara Magharibi inatakiwa kujadiliwa baadaye, lakini wakaipa nafasi Morocco kuunga nao. Morocco imekuwa nchi ya 55 kuwa mwanachama wa Umoja wa Afrika. Taifa hilo lilijitoa kwenye Umoja huo mwaka 1984 baada ya malumbano makali kutokana na kuendelea kuikalia Sahara Magharibui ambayo inatafuta uhuru wake.

Wakati tunaufunga mwaka nyota wa zamani wa soka George Weah anaingia rasmi katika kundi la marais wa Afrika akiiwakilisha Nchi ya Liberia.

Weah alimshinda mpinzani wake Joseph Boakai kwa kuongoza kwa asilimia 61.5 ya kati ya kura asilimia 98.1.

Weah ni mwanasoka maarufu aliyepata kucheza kwenye klabu za soka za juu Ulaya zikiwamo  Paris St-Germain (PSG) na AC Milan, kabla ya kumaliza taaluma yake nchini Uingereza kwa kuzichezea klabu za Chelsea na Manchester City kwa muda mfupi.

Weah ni Mwafrika pekee aliyewahi kutwaa taji la mchezaji bora duniani na tuzo ya Ballon D’Or.

Makala haya yameandaliwa kwa msaada wa mashirika ya habari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles