24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, April 14, 2024

Contact us: [email protected]

SI SAHIHI KUWABAGUA WATOTO


Na Arodia Peter -

SIFA mojawapo kuu ya kuwa mzazi bora ni kutoa malezi bora kwa watoto wote  katika nyanja zote bila ubaguzi.

Baadhi ya wazazi wanadhani kuwa malezi bora kwa mtoto ni  kumpatia huduma muhimu kama malazi, chakula na mavazi pekee.

Ili mzazi ukamilishe dhana ya kuwajibika kikamilifu kwa watoto, ni lazima huduma muhimu zitolewe pamoja na ushiriki wa kimatendo.

Ifahamike kuwa mzazi ndiye kiunganishi kikuu kati yake na mtoto/watoto kuanzia mtoto anapokuwa mdogo hadi ukubwani.

Wapo baadhi ya watoto ni watukutu na wengine wasikivu. Miongoni mwa familia zetu kuna watoto waliopatikana ndani ya ndoa na wengine nje.

Licha ya mgawanyiko huo na tabia za watoto, si vema mzazi kutumia nafasi hiyo kuwabagua watoto.

Baadhi ya wanaume wenye watoto nje ya ndoa, wengi wao ushiriki wa kimatendo ni mdogo au hakuna kabisa.

Miongoni mwa kundi hilo wapo wanaodhani kuwa stahiki za mtoto ni chakula, malazi na mavazi, bila kufahamu kuwa malezi ni kuwa karibu zaidi na mtoto haijalishi ni wa ndani au nje ya ndoa.

Wazazi wenye tabia hiyo hata kwenye mazungumzo yao aghalabu sana kumzungumza mtoto ambaye nafsini mwake amemtenga.

Si tu kwa watoto wa nje ya ndoa, wapo baadhi ya wazazi wamegawana watoto; wapo mtoto/watoto wa baba na wa mama.

Zipo familia bila kuambiwa utagundua wazi kuwa kuna watoto wanalelewa katika misingi ya kibaguzi.

Mfano mzazi anataka kuwapa watoto zawadi badala ya kuwaita wote awagawie, anampa yule anayempenda zaidi achague anayoipenda kisha wanafuata wengine au mwingine.

Kitendo hicho kinawafanya watoto kuathirika kisaikolojia na kwa sababu anayefanya hivyo ni mzazi, inawawia vigumu kueleza machungu waliyonayo.

Mbali ya kuathirika kisaikolojia, mtoto anayetengwa huingia chuki kati yake na wenzake au na mzazi husika.

Jambo hilo ni hatari kwa ustawi wa mtoto/watoto na familia kwa ujumla.

Wazazi wanapaswa kuwa makini katika kujenga misingi bora ya malezi kwa watoto  kuanzia wanapokuwa wadogo.

Watoto wapewe malezi yenye kuzingatia usawa ili kuwajengea upendo na mshikamano katika makuzi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles