30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

MDEE: MSIOGOPE KUTETEA WATOTO WA KIKE

Na JANETH MUSHI -ARUSHA

VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wametakiwa kusimama bila kuogopa kutetea haki za watoto wa kike hata ikibidi kutofautiana na watawala kwa sababu Mungu atawabariki.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, alipozungumza katika Kituo cha kulea watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Samaritan Village, walipoenda kutoa msaada wa vyakula ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa chama hicho.

Mdee alisema wakati chama kinajipanga kuandaa maadhimisho hayo, wao wameamua kuanza kusherehekea miaka hiyo muhimu ya mapambano ya demokrasia kwa kufanya shughuli mbalimbali ikiwamo za kijamii.

Mdee ambaye pia ni Mbunge wa Kawe, alisema viongozi wana wajibu wa kuhakikisha wanatetea makundi mbalimbali ikiwamo watoto wa kike bila woga hata kama wanakabiliana na vikwazo vinavyotaka kuwazuia kutetea watoto kutimiza ndoto zao.

“Nyie mmeshuhudia hivi karibuni kwamba yanatoka matamko ambayo yanaweza yakafifisha ama kuua ndoto za watoto, kiongozi mkubwa wa Serikali anasema mtoto wa kike akipata mimba shule marufuku.

“Watoto wasipolindwa yakatokea mabaya dhidi yao sisi tunaotakiwa kuwalinda tukisema ndoto zao zimekufa tutakuwa hatulitendei haki Taifa, ndiyo maana nasema sisi kama viongozi kwa ngazi yoyote ile hata kama kiongozi wa nchi akisema mtoto hatakiwi kupata nafasi wewe simamia mtoto Mungu atakulinda.

“Lakini hebu tujiulize, hawa watoto wa kike ambao kituo chenu kimewachukua kisingewachukua huko mtaani kwa utoto  wao watu wangapi wangewafanyia vitendo vya kikatili, wangeanza kudhalilishwa kijinsia tunajua aina ya jamii ilivyo na watu wakatili,” alisema.

Mdee alisema viongozi ambao wana wajibu wa kulinda watoto wasipotekeleza wajibu huo watakuwa hawalitendei Taifa haki na kuwa licha ya kuwekwa mahabusu kwa siku kadhaa hataacha kuzungumza kuhusu haki za watoto.

“Niseme tu mimi sitaacha kusema maana kuna watu wengine wanafikiria ukiwekwa ndani siku mbili au tatu unaogopa, unaenda unawekwa ndani unakula pozi kidogo unarudi unasubiri mambo yatulie ili wazazi nao wasipaniki, ukienda ndani sana wanachanganyikiwa, unaenda unalianzisha tena kwa sababu tusiposema sisi atasema nani,” alihoji.

Awali, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Josephat Mmanyi, alisema hadi sasa kituo hicho kina watoto 50 wenye umri kuanzia mwaka mmoja hadi miaka 21 ambao wengi wao wanasoma shule mbalimbali za msingi na sekondari za jijini hapa.

“Tunawashukuru kwa kuja kututembelea na msaada mliotupa, tunawashukuru sana ila kwa ajili ya kumbukumbu ya Mdee kuja kituoni kwetu tutamwomba apande mti ambao tutaupa jina lake,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Arusha, Secilia Ndossi, alisema jamii kwa kushirikiana ina wajibu wa kuwahudumia watoto ikiwamo wanaotelekezwa na familia zao ikiwa ni pamoja na kuvisaidia vituo vinavyolea watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.

“Hawa watoto ni wetu, ni taifa la kesho, wanahitaji upendo wetu kama wazazi ndiyo maana sisi kama Bawacha tumeamua kutoa hiki kidogo kama sadaka, hasa ikizingatiwa leo ni sikukuu, lakini tumeona ni vema tukaja kushiriki pamoja nanyi,” alisema Ndossi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles