26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MDEE KUONGOZA KONGAMANO LA UCHUMI, SIASA

Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Halima Mdee

Na JANETH MUSHI

-ARUSHA

MWENYEKITI wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, anatarajiwa kuongoza kongamano la kujadili masuala ya kisiasa na kiuchumi katika kuleta maendeleo, litakalofanyika jijini hapa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Bawacha Mkoa wa Arusha, Irene Kimathi, alisema kongamano hilo linaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya kuanzishwa kwa Chadema.

Alisema kongamano hilo litafanyika Septemba mosi mwaka huu katika Hoteli ya kitalii ya Ne Safari, ambapo Mdee ataungana na wadau wengine wa maendeleo wakiwemo viongozi wa Chadema Mkoa wa Arusha katika kongamano hilo.

“Chadema ilianzishwa 1992 na waasisi wetu akiwemo Edwin Mtei na baadaye kilipata usajili 1993, tumefika miaka 25 hii ni Silver Jubilee, chama kimetupa dhamana Bawacha kuandaa maadhimisho haya, hivyo tutakuwa na kongamano litakalojadili mahusiano ya kisiasa na kiuchumi katika kuleta maendeleo,” alisema Irene.

Alisema maadhimisho hayo kwa Mkoa wa Arusha yanatarajiwa kufanyika kwa siku mbili, ambapo Septemba mosi wataanza na kufanya kazi za jamii ikiwemo kutembelea vituo vya watoto waishio katika mazingira hatarishi, kituo cha wazee, wodi za wazazi na kutoa misaada mbalimbali kabla ya kuanza kongamano hilo litakalofuatiwa na maonyesho ya mavazi usiku.

Alisema Septemba 2, mwaka huu wanatarajia kuwa na bonanza ambalo litafanyika katika viwanja vya Paloti, Unga Ltd na litakuwa na michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, kuruka kamba, kukimbiza kuku, mpira wa mikono na mpira wa miguu kati ya viongozi wakiwemo wabunge na madiwani.

Akizungumzia baadhi ya mafanikio chama hicho walichokipata tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, alisema idadi ya wabunge na madiwani imekuwa ikiongezeka.

Alisema mwaka 1995 walipata wabunge wanne na madiwani 42, mwaka 2000 wabunge 5 na madiwani 75, mwaka 2005 wabunge wakafika 11 madiwani 103, mwaka 2010 wabunge walikuwa 50 na madiwani 467 na mwaka 2015 wabunge wakawa 72 na madiwani 1108.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles