AMINA OMARI-TANG
BARAZA la Habari Tanzania(MCT) kwa kushirikiana na wahariri na wadau wa habari nchini linaandaa mpango kazi wa uhuru wa habari na mikakati ya kumaliza changamoto za usalama kwa waandishi wa habari nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la hilo, Kajubi Mukajanga wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa ushauriano kati yaMCT, wahariri na wadau wa habari nchini, Tanga jana.
Alisema mpango huo ndiyo utakaoweza kuwa suluhisho au ufumbuzi wa changamoto za usalama wa waandishi na kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini.
Kajubi alisema anamini mikakati hiyo ya pamoja itaweza kuweka dira ndani ya vyumba vya habari katika kuhakikisha wanasimama katika misingi yao ya haki katika kutimiza wajibu wao wa kuhabarisha umma kwa uhuru bila ya vikwazo vyovyote.
“Taifa linalozungumza ni lazima litazame wale wanaozungumza kama wana uwezo wa kuzungumza kwa kuhakikisha uhuru wa uhariri na usalama wa waandishi unakuwa bora zaidi,” alisema Mukajanga.
Makamu wa Rais wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Jane Mihanji alisema waandishi ambao wapo huru wanaweza kutekeleza majukumu yao bila ya hofu yoyote.
“Tunatamani siku moja waandishi nchini tuweze kufanya kazi kwa uhuru bila kuwa na woga wa kutishiwa maisha yetu wala kubanwa na mamlaka za juu katika kutekeleza majukumu yetu,” alisema.
Aaliyekuwa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari, Absalom Kibanda alisema kukithiri kwa unyanyasaji na vipigo kwa waandishi wa habari bila kuchukuliwa hatua stahiki ni pigo kwa tasnia nzima.
“Hatua ya kufungia vyombo vya habari siyo tu vinawaathiri waandishi ambao ni waajiriwa wa vyombo hivyo bali hata wananchi ambao walitegemea kupata habari kupitia vyombo hivyo,” alisema Kibanda.