27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mwandishi  atuhumiwa kwa ugaidi Rwanda

KIGALI, Rwanda

MWANDISHI wa  habari wa kujitegemea, Phocus Ndayizera ameonyeshwa mbele ya vyombo vya habari na polisi wa upelelezi nchini hapa  wiki moja baada ya kutoweka huku akidaiwa kujihususha na vitendo vya ugaidi.

Msemaji wa idara ya polisi ya upelelezi nchini hapa alisema juzi kwamba  mwandishi huyo anatuhumiwa makosa ya ugaidi na  alikuwa akifuatiliwa.

Mwandishi huyo ambaye amewahi kufanyia kazi vyombo vya habari mbalimbali na mara kwa mara amekuwa akiripoti pia katika Shirika la Utangazaji la Uingereza  (BBC),  Idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi,   alisema kwamba hajui kwa nini anashikiliwa.

Mwandishi wa BBC   mjini hapa, Yves Bucyana, alisema    Ndayizera  alipoonekana mbele ya waandishi wa habari   makao makuu ya idara ya polisi inayohusika na upelelezi, alikuwa amefungwa  pingu na hali yake ilionyesha uchovu.

Alisema, mwandishi huyo alifahamika katika vyombo vya habari mbalimbali na mara kwa mara aliifanyia kazi BBC idhaa ya Kinyarwanda na Kirundi kama mwandishi wa kujitegemea.

Alisema   mara ya mwisho kwa  Ndayizera   kuiripotia BBC ilikuwa   Juni mwaka huu.

Alipotakiwa na polisi kuwambia waandishi wa habari tuhuma dhidi yake, Ndayizera alisema   hana habari yoyote kuhusu mashitaka dhidi yake.

Ndayizera alisema   alikamatwa katika mtaa wa Nyamirambo jijini hapa  alipokwenda kumuona jamaa yake na kupelekwa sehemu isiyojulikana kabla ya kujikuta katika mahabusu ya polisi Kituo cha Remera.

Msemaji wa Idara ya Upelelezi, Modeste Mbabazi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi.

Polisi wa upelelezi wamekiri kuwa ndiyo waliokuwa wanamshikilia mwandishi huyo kwa wiki nzima.

Msemaji huyo wa Idara ya Upelelezi,  Mbabazi aliwaambia waandishi wa habari kwamba Ndayizera anatuhumiwa kwa kujihusha na ugaidi.

Kwa mujibu wa msemaji huyo, walikuwa na taarifa za mipango ya watuhumiwa   kuhatarisha usalama wa   Rwanda.

Msemaji wa Polisi alisema walisubiri siku kadhaa kutangaza kumshikilia mwandishi huyo kwa sababu  makosa ya ugaidi yanafuatiliwa kwa njia ya  pekee tofauti na makosa mengine.

Haijafahamika ni lini mwandishi huyo na wengine wanaotuhumiwa   watafikishwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles