FRANCISÂ GODWIN-IRINGA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa kimesema kimevumilia na kutekeleza kwa utii mkubwa agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020 wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu ambapo sasa wataanza kazi ya ujenzi wa demokrasi kama rais alivyoagiza .
Akizungumza na wanahabari jana mjini Iringa Mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa Mchungaji Peter Msigwa ambae ni mbunge wa Iringa Mjini alisema kuwa chama chake kimekuwa miongoni mwa vyama vya upinzani nchini ambavyo vilionyesha utii mkubwa wa utekelezaji wa agizo la Rais Dkt Magufuli kwa kutofanya mikutano ya hadhara kwa kipindi chote cha miaka minne sasa.
Msigwa ambaye alikuwa ameambatana na viongozi wa kanda hiyo, aliwataka viongozi wa wilaya na mikoa wa Chadema Kanda ya Nyasa kuanza kuandaa mikutano yao ya hadhara kwa kufuata taratibu zote za kuomba vibali vya mikutano hiyo ili kuendelea na ujenzi wa chama chao kuelekea Oktoba 25 siku ya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais .
” Tuliweza kutekeleza agizo la mheshimiwa Rais kwa utulivu mkubwa japo agizo hilo halikuwa sawa maana lilikuwa ni kinyume na makuzi ya demokrasia nchini, vyama vya siasa msingi wake ni siasa hivyo kuzuia mikutano kwa haikuwa sawa lakini tuliweza kutii.
“Ila jamani si alisema hakuna mikutano ya hadhara ya vyama hadi mwaka 2020 na huu ndio mwaka 2020 hivyo tunaendelea na mikutano kama kawaida ” alisema mchungaji Msigwa .
Msigwa alisema miaka minne ambayo walizuiwa kufanya mikutano ya siasa chama hicho kanda ya Nyasa walikuwa wakijijenga zaidi kuanzia ngazi za chini.
Alisema awali hawakuwahi kuwa na misingi hiyo na kwamba kwa sasa wana mtaji mkubwa kuliko hata ilivyo kuwa mwaka 2015 walivyoingia katika Uchaguzi Mkuu .
Alisema kuzuiwa kwa mikutano ya siasa ndiko kulikowapa nguvu ya kufanya vikao vyao vya ndani na kujengana zaidi.
Alisema baada ya miaka minne bila kufanya siasa ya wazi wanatoka wakiwa na mbinu na uwezo wa kushindana vikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akielezea kuhusu hali ya uchumi nchini hasa kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini alisema kila mwananchi analia tofauti na ilivyokuwa Serikali ya awamu ya tatu na ya nne.
Aidha aliishutumu Serikali kwa kushindwa kusimamia bei ya mazao pia kushindwa kutafuta masoko nje ya nchi ili kusaidia wakulima kulinda mitaji yao jambo ambalo limewaathiri wakulima hivyo kupata hasara kwa kuuza mazao kwa bei za chini.
Akitolea mfano kwa taarifa ya Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na upatikanaji wake taarifa ya mwaka 2018/2019 kuwa ilionesha jumla ya Halmashauri 46 katika mikoa 13 zilikuwa na upungufu wa chakula, miongoni mwa Halmashauri hizo ni Halmashauri ya Iringa Vijijini ambayo ipo kwenye orodha ya kanda zinazozalisha chakula kwa wingi.
Kuhusu wafanyakazi wa umma, Mchungaji Msigwa hawajaongezewa mishahara yao kwa miaka minne sasa kinyume na sheria huku gharama za maisha zikiongezeka siku hadi siku.
Pia alisema wafanyaakazi wa umma hawajapandishwa madaraja kinyume na sheria kwa takribani miaka minne sasa tangu utawala huu wa wanyonge uingie madarakani .
“Wafanyakazi waliostaafu ambao walitoa mchango mkubwa kwa Taifa hadi sasa malipo ya pesheni zao yamekuwa yakisua sua sana huku Serikali ikijinadi fedha zipo na tumeshuhudia awamu hii ya tano wafanyakazi wengi wa sekta binafsi wamefutwa kazi kutokana na mazingira magumu katika sekta binafsi.”
Mchungaji Msigwa alisema hali ya afya kwa mwaka 211 katika maadhimisho ya siku ya wazee duniani iliyofanyika mjini Morogoro serikali ya CCM ilitangaza kutoa matibabu bure kwa wazee jambo ambalo takribani miaka 9 sasa wameshindwa kulitekeleza.
Aidha kuhusu elimu alitaja sababu sita ambazo zinafanya wanafunzi kuhangaika ikiwemo ya mabadiliko ya mara kwa mara ya sera ya elimu ya msingi, suala la mikopo ya elimu ya juu na sababu nyingine ambazo wao wamekuja na majibu .