CAROLINA KASKAZINI, MAREKANI
MCHUNGAJI Billy Graham, mmoja wa wainjilisti wa Kikristo maarufu zaidi duniani, amefariki dunia juzi asubuhi akiwa na umri wa miaka 99.
Mbali ya kuwa mhubiri wa kimataifa aliyetembelea nchi zaidi ya 150, Graham pia alikuwa mshauri wa kiroho wa marais wa Marekani kuanzia Rais wa 33, Harry Truman.
Kwa mujibu wa Mark DeMoss ambaye ni msemaji wa familia, Graham alifariki dunia akiwa nyumbani kwake katika Jimbo la Carolina Kaskazini.
DeMoss alisema Graham alifariki akiwa usingizini bila uwapo wa mwanafamilia yeyote zaidi ya muuguzi pekee.
Katika mkutano na wanahabari juzi, DeMoss alisema Graham, ambaye alifanya mkutano wake wa mwisho wa hadhara mwaka 2005 jijini New York, akiwa na umri wa miaka 86, mwili wake kwa sasa uko katika nyumba ya mazishi ya Morris huko Asheville jimboni hapa.
Kuhusu taratibu za msiba na mazishi, alisema wanafamilia watamfanyia maombi maalumu kesho na kuanzia Jumatatu ijayo mwili wake utakuwa katika nyumba ya familia kwa utoaji wa heshima za mwisho kabla ya kuzikwa Ijumaa.
Mtoto wake, Franklin Graham, ambaye amekabidhiwa na baba yake huyo huduma ya kimataifa ya injili, anatarajia kuongoza familia yake katika mazishi hayo ya dakika 90.
Mwili wa Graham utapumzishwa katika kaburi la matofari lenye umbo la msalaba upande wa kaskazini mashariki mwa Maktaba ya Bill Graham, kandoni mwa alimozikwa mkewe Ruth mwaka 2007.
Jeneza lililobeba mwili wake limetengenezwa na wafungwa wa Gereza la Louisiana State Penitentiary nchini Angola.
Akifahamika kama ‘Mchungaji wa Amerika’, Graham alikuwa mtu muhimu wa uamsho wa vuguvugu la Kikristo la Kiinjili Marekani.
Mhubiri huyu alianza kufanya mikutano ya uamsho katika miaka ya 1940 kisha akaenda kuwa mshauri wa marais kadhaa wa Marekani.
Katika mikutano yake ya kimataifa aliyoanzia kuhubiri jijini London, Uingereza mwaka 1954, alikuwa akikusanya maelfu ya watu kila alipofanya mikutano yake ya hadhara ya injili.
Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Graham aliwahi kuhubiri nchini Tanzania miaka 55 iliyopita, wakati nchi ikijulikana kama Tanganyika, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Afrika katika miaka ya 1960.
Kwa mujibu wa mtandao wa shirika lake, takriban watu 40,000 walihudhuria mkutano huo wa siku moja, Februari 28, 1960.
Kwa zaidi ya miaka 60 ya huduma yake, inakadiriwa kuwa amewahubiria jumla ya watu milioni 210.
Wakati wa harakati za mashirika ya kupigania haki za binadamu, Graham aliibuka kuwa mkasoaji mkubwa wa ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Ni mhubiri aliyeepuka kashfa mbalimbali zilizowazonga wahubiri wengi waliotumia runinga kusambaza injili.
Rais Donald Trump amemwelezea Graham kama ‘mwanaume wa kipekee’.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Trump alisema: “Mhubiri maarufu wa Injili Billy Graham. Hakuna aliyekuwa kama yeye! Atakumbukwa na Wakristo na watu wa dini zote. Mwanamume wa kipekee kabisa.”