24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

MCHENZO MCHAFU TENA BANDARINI

*Majaliwa akuta trela 44 zilizotaka kutolewa kwa jina lake kukwepa kodi

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


BAADHI ya wafanyabiashara wameonekana kutaka kurudisha mchezo wa kukwepa kodi katika bandari ya Dar es Salaam.

Hilo limebainika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuagiza polisi kuwakamata watu wawili kwa tuhuma za kuingiza nchini trela 44 za malori mwaka 2015 na kutaka kuzitoa bandarini bila kuzilipia kodi, wakitumia jina la mtendaji huyo mkuu wa Serikali.

Wakati Majaliwa akitoa agizo hilo jana, hivi karibuni Rais Dk. John Magufuli, alitembelea bandari hiyo na kukuta magari 50 ya wagonjwa yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kwa jina la Ofisi ya Rais, huku yakiwa si mali ya ofisi hiyo.

Magufuli alimtaka mtu aliyeingiza magari hayo kujitokeza kwani anamfahamu.

Hali hii inajitokeza sasa ikiwa ni miaka miwili tangu Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani na kukemea uozo kwenye bandari hiyo.

Ziara za kushtukiza za Rais Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa, ziliibua madudu na mapato ya sekta hiyo kupanda baada ya udhibiti wa mianya ya kukwepa kodi katika bandari hiyo.

Juni mwaka jana, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata, alisema baada ya mianya ya ukwepaji kodi kuzibwa bandarini, makusanyo yamepanda.

Alisema walikuwa wakikusanya Sh bilioni 200 hadi 300 kwa mwezi kutoka katika bandari hiyo, lakini baada ya kudhibiti mianya ya uingizaji mizigo, Aprili walikusanya Sh bilioni 458 na Juni Sh bilioni 517.

 

MAJALIWA NA TRELA

Katika ziara yake aliyofanya katika bandari hiyo jana, Majaliwa aliamuru kukamatwa kwa watu wawili aliowataja kwa jina moja moja; Bahman wa Kampuni ya NAS na Samwel ambaye ni wakala wa Kampuni ya Wallmark.

Majaliwa aliitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu serikalini.

“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dk. John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Majaliwa.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu jana, ilisema kuwa Majaliwa alifanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara Bahman kutaka kutapeli uongozi wa TPA ili atoe trela hizo zilizoingizwa nchini mwaka 2015 zikitokea Uturuki.

 

Taarifa hiyo ilisema kuwa Bahman alitaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwamba amewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.

Ilisema kuwa Majaliwa amesema Serikali inataka watu wafuate sheria na taratibu za nchi, ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubughudhiwa.

Taarifa hiyo ilisema kuwa Majaliwa amewataka wafanyabiashara kufuata sheria za nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao.

“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading), inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana hajafanya hivyo,” ilisema taarifa hiyo.

Majaliwa alisema kitendo cha kusajili trela hizo bila ya kuwa na nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza bidhaa hizo kutolipwa malipo yaliyobaki.

Alisema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Uturuki na kwamba kampuni iliyouza tela hizo, imeshawasilisha malalamiko katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini.

“Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania, sasa huu ujanja ujanja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi, unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria, nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja,” ilisema taarifa hiyo ya Majaliwa.

Pia Majaliwa ametoa wito kwa TRA kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko, alimweleza Majaliwa kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, wao walisimamia sheria na taratibu.

 

NOVEMBA 27, 2015

Majaliwa alifanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam na kuwasimamisha kazi maofisa watano wa bandari na watumishi watatu wa TRA kutokana na upotevu wa makontena 349 yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 80.

 

FEBRUARI 11, 2016

Majaliwa alimtaka mtendaji mkuu wa wakala wa vipimo Tanzania, kumpa maelezo kwa maandishi ya sababu za kuzuia utumiwaji wa mita za kupima kiwango cha mafuta kinachopakuliwa bandarini kutoka melini (flow meter) kwa kipindi cha miaka mitano, jambo lililosababisha Serikali kupata hasara ya mamilioni ya shilingi, huku mita hizo zikianza kufanya kazi siku moja tu kabla ya kufanya ziara hiyo bandarini hapo.

 

SEPTEMBA 26, 2016

Rais Magufuli aliagiza TPA kukutana na kampuni ya upakuaji wa makontena bandarini – TICTS ili kupitia upya mkataba baina yao. Pia amebaini baadhi mashine za kukagulia makontena (scaner) bandarini hapo zina kasoro na kuagiza kununuliwa nne mpya ndani ya miezi miwili.

 

MACHI 23, 2017

Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini, ikiwamo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.

Katika ziara hiyo, alishuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo Kanda ya Ziwa, ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2, 2017.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles