27.7 C
Dar es Salaam
Saturday, June 15, 2024

Contact us: [email protected]

‘ASILIMIA KUBWA YA WANASIASA WACHUMIA TUMBO’

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, John Shibuda amesema asilimia 99 ya wanasiasa wana njaa na ni ‘wachumia tumbo’.

Amesema wengi wao wamekuwa wakifanya siasa za unafiki badala ya kujadili masuala mazito ya  taifa.

Kauli hiyo aliitoa jana katika mdahalo ulioandaliwa na Twaweza  kujadili mada ya ‘demokrasia yetu’ na kuongozwa na Mkurugenzi wa Taasisi hiyo, Aidan Eyakuze.

Akijibu maswali ya washiriki wa mdahalo huo ambao wengi wao walihoji kuhusu nafasi ya wanasiasa katika kusimamia mabadiliko ya Katiba Mpya,  Shibuda alisema wanasiasa hao wamekuwa si wakweli na   vipaumbele vyao ni njaa.

“Ugonjwa mkubwa sana Tanzania ni njaa zetu hata kama ni kwenda Mbinguni kupitia siasa, asilimia 99 tunakwenda motoni kwa sababu vipaumbele vyetu ni matumbo,” alisema Shibuda.

Hata hivyo hoja hiyo ya Shibuda ilipingwa na Katibu Mkuu wa Chama cha Siasa cha Wakulima Tanzania (Alliance Farmers Party -AFP), Rashid Rai kwa kumtaka Shibuda aseme baadhi tu ya wanasiasa na si wote.

“Napenda niweke sawa kuhusu hoja ya mwenyekiti wangu aliposema wanasiasa ni wanafiki na waongo, hapa si wote ni baadhi yao tu,” alisema Rai.

Kauli hiyo ya Rai  ilijibiwa na Shibuda papo hapo akisema  “Samaki mmoja akioza wote wanaoza”.

Kwa sababu hiyo, Shibuda  aliwataka wanasiasa kuanza kufikiria masilahi ya taifa kwanza badala ya kutanguliza masilahi binafsi.

“Ni lazima mjifikirishe na kujiuliza kuwa mtashinda vipi vita ya kudai masilahi ya matumbo ndipo muweze kudai masilahi ya nchi?” alisema Shibuda.

Alisema wanasiasa wa Tanzania wanahitaji kupewa elimu ya uraia   waweze kukutana katika ndoto ya kufikiria ndoto ya Tanzania wanayoitaka.

“Tanzania vyama vyote 19 vya siasa hawajui maana ya siasa, hawana elimu ya uraia hawajui vyama vyao vina dira gani, ndoto gani,” alisema Shibuda.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliitaka serikali kuimarisha mifumo ya kutoa taarifa kwa kuzijengea uwezo taasisi zake.

Alisema serikali inatakiwa kuboresha sheria  kuongeza uwazi na uwajibikaji wa viongozi katika rasilimali za taifa.

“Mapambano dhidi ya rushwa yanaonekana lakini inapaswa kujiendesha kwa uwazi na kuruhusu taasisi zake kuwajibika katika ununuzi na matumizi ya fedha za umma,” alisema Zitto.

Alisema jambo linaloisaidia serikali kukabiliana na ufisadi ni uwazi na uhuru wa maoni uliotolewa na awamu ya nne ya serikali kwa sababu wananchi waliweza kutoa taarifa na ndizo zinazofanyiwa kazi kwa sasa.

“Usiri uliopo sasa katika serikali unawanyima wananchi haki ya kupata taarifa muhimu za miradi mbalimbali ya maendeleo  katika maeneo yao jambo ambalo linaweza kusababisha kuwapo na ufisadi huko,” alisema Zitto.

Alisema sababu kuu ya kuibuka hoja mbalimbali zikiwamo za Epa, Richmond na Meremeta ni kwa vile  serikali ya awamu ya nne iliimarisha taasisi zake kuwa za uwazi na uwajibikaji.

Akichangia katika madahalo huo, Mbunge wa Tarime vijijini, John Heche (Chadema),  alisema ni lazima watu wasimame na kudai demokrasia ya nchi badala ya kukaa na kusubiri mtu mmoja aamue kila jambo kwa Watanzania.

“Kwa hili la demokrasia kwa sasa nasema hapana, hakuna kabisa maana, haiwezekani mtu mmoja anaamua mambo ya Watanzania. Kwa hili binafsi ninalipinga na sikubaliani nalo waache na wenzako waseme.

“Mfano mdogo kule Mbozi katika uchaguzi huu wa madiwani mgombea aliyeshindwa ndiye anatangazwa mshindi! Hili hapana!” alisema

Alisema yeye kama mjumbe wa  Kamati Kuu ya Chadema, amepokea hoja ya kuunganisha nguvu na hivyo ataipeleka katika chama chake ili kudai demokrasia.

“Tutaendelea kupambana mpaka wananchi wa nchi hii watakapokuwa huru kutoa maoni yao ya namna ya kuendesha nchi na kuheshimika na viongozi wao,” alisema Heche.

Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Paschal Mayalla, alisema akili za watu wa CCM ni kutawala milele jambo ambalo linasababisha kuuminya upinzani na kuwanyima demokrasia.

“Rais anakanyaga Katiba na analindwa na Katiba hiyo kwa kuwa hairuhusu kumshtaki, lakini vyama vya upinzani hawamwambii wala kumshtaki.

“Kwa nini wapinzani badala ya kulalamika, nendeni mkafungue kesi ili mahakama kama chombo cha kutafsiri sheria kiseme,” alisema Mayala.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles