26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

MCHAWI WA FILAMU ZA BONGO HAYUPO KARIAKOO

Na FESTO POLEA


BAADHI ya wasanii wa filamu za Bongo wameandamana maeneo ya Kariakoo wakiamini ndiko alipo mchawi anayeroga kazi zao zisiuzike.

Awali Bongo Fleva walikuwa wakipata shida kubwa walipokuwa wakipambana na muziki wa Genge uliokuwa maarufu nchini Kenya ambao ladha na mwonekano wa muziki huo ni kama wa Bongo Fleva, lakini hawakuandamana kwenda Kariakoo kupinga nyimbo zao kupakuliwa ama kutopakuliwa, walikaa chini wakijiuliza na kumgundua mchawi wao, wakamfanyia kazi kwa sasa ndiyo wanaoongoza soko Afrika Mashariki.

Bongo Fleva waligundua vitu vingi ikiwemo uwekezaji kuanzia studio na video, lakini pia walihakikisha wanachokiimba kina mantiki kwa jamii na pia wanawekeza kwenye usambazaji.

Bongo Fleva waliliona hilo wakaamua kufanya uwekezaji mkubwa hadi leo wanaongoza Afrika Mashariki kwa ubora wa kazi zao na namna wanavyopata shoo nyingi ndani na nje ya nchi hizo, lakini kilichosababisha ni kumgundua mchawi wako na kurekebisha mapungufu yako kwa kasi ya juu.

Leo hii uwekezaji unaofanywa kwenye wimbo mmoja wa msanii wa Bongo Fleva, ni mkubwa ingawa kwenye audio unaweza kuwa bure kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wenye studio, alitaka kujitangaza kupitia msanii mwenye jina lakini inapokuja kwenye video uwekezaji wake huwa mkubwa.

Kama Diamond, Ali Kiba, Vanessa, Chege Chigunda, Ay, mwana FA na wengine wengi wanawekeza kwenye video za nyimbo zao za dakika tatu hadi tano kiasi cha zaidi ya milioni 50 na washiriki katika wimbo huo wanaweza kuwa wawili, watatu au sita, inashindikanaje kwa nyie Bongo Movie ambao mkiwekeza sana ni milioni 30 tena kwa hesabu hewa.

Filamu nyingi mlizotaja zimegharimu zaidi ya milioni 30 hakuna hata moja iliyoingia mtaani hadi leo, kama msanii wa Bongo Fleva anatumia hadi milioni 50 kwa video ya dakika tano (5), inakuwaje kwa nyie mnaoandaa video ya dakika 60 (saa moja) au filamu zenye sehemu ya I, II, III na IV mkatumia milioni 10, huku mkiwa na idadi kubwa ya washiriki kwenye filamu husika, hapo kutakuwa na ubora wa filamu kweli?

Huo ndio uchawi na si kuandamana Kariakoo, igeni wasanii wa Bongo Fleva wanavyofanya mtafika mbali kimabadiliko na hamtoandamana tena Kariakoo kudai mnachokidai, huku wengi wakiwashangaa.

Boresheni filamu zenu kuanzia ubora wake, hadithi zenye uhalisia wa maisha ya mnachoigiza, uhalisia wa mandhari mnazoigizia na hata wasanii mnaowatumia katika maigizo yenu wawe na uhalisia wa anachokiigiza.

Mtakapoboresha filamu zenu mtaondokana na aibu nyingi ikiwemo wakati mnaposhiriki matamasha mbalimbali ya uonyeshaji na kushindanisha filamu zenu kama mlivyoshiriki kwenye tamasha la Kimataifa la Filamu za Nchi za Majahazi (ZIFF) filamu zenu huwa zinashindwa kuendana na kinachoandaliwa kwenye tamasha hilo, lakini hilo mmeshindwa kulifanyia kazi kila mwaka mnarudia makosa yake yale.

Wakati wateja wenu wakilalamika kupata kitu kisichoendana na fedha zao wanazotumia kununua kazi zenu, anatokea mtu mwingine anatafasiri sinema ya Kikorea, Kimarekani, Kijapani, Kifilipino na kwingineko tena kwa lugha ya Kiswahili ingawa si vyote anapatia, lakini anaeleweka kwanini huyu mtu asikimbilie kununua sinema, tamthilia hiyo yenye sehemu 20 tena kwa gharama isiyozidi Sh 2000.

Rudisheni imani iliyopotea kwa waliokuwa mashabiki na wateja wenu wa zamani warudi kuzinunua filamu hizo, wengi wa wateja wenu walifurahia mlichokuwa mkikifanya kipindi hicho cha marehemu Kanumba na kwa kuwa mnatumia Kiswahili mashabiki wenu waliongezeka wakaachana na soko la filamu za Nigeria, Ghana na Afrika Kusini.

Nina hakika kama kazi za Bongo Movie zingekuwa na ubora unaotakiwa, hadithi nzuri zenye ubora wa picha na waigizaji wake wakatambua wanachokifanya, msambazaji angeweza kusambaza kazi zote nzuri za Bongo Movie na kila mmoja angepata anachostahili, lakini hakuna filamu bora kwa sasa ndiyo maana wanamtafuta mchawi Kariakoo.

Soko la filamu lilipotanuka na wasambazaji waliongezeka kwa sababu kulikuwa na ushindani wa kutoa kazi bora nzuri na zenye kueleweka hasa kipindi alichokuwepo Kanumba, lakini baada ya kufariki ubora wa kazi hizo umeyumba ndiyo maana na soko limeyumba na hata wasambazaji hawataki kazi mbovu kwa kuwa haziuziki huko mitaani.

Pia mkumbuke kwa sasa huwezi kuzuia ukuaji wa teknolojia, hata mkiandamana Kariakoo halitabadilika na mkiendeleza mazoea ya kutegemea majina yenu ndiyo yafikishe mbali tasnia yenu, maandamano yenu hayataishia Kariakoo bali mtayaendeleza sehemu nyingine ambazo filamu zenu zilikuwa zikiuzika kwa wingi ikiwemo Zambia, Rwanda na Kongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles