27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAMFUKUZA NCHINI BOSI UN

* Aondolewa ndani ya saa 24, adaiwa kuja na malengo tofauti


Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SERIKALI imemwondoa nchini Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Awa Dabo.

Mkurugenzi huyo raia wa Gambia, aliyeletwa nchini na Umoja wa Mataifa (UN) Agosti 2015, aliondolewa wiki iliyopita ndani ya saa 24 kwa agizo la Serikali, huku akiwa chini ya ulinzi.

Hadi sasa haijaelezwa sababu za kuondolewa.

MTANZANIA ilipomtafuta Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi Kasiga ili kupata ufafanuzi wa kina wa tukio hilo, alijibu kwa kifupi kuwa anayepaswa kuzungumzia hilo ni UNDP na si Serikali.

“Ninakuomba watafute UNDP wenyewe ndio wanaweza kuzungumzia hilo kwa sasa,” alisema Mindi.

Ulipotafutwa uongozi wa UNDP, Mtaalamu wa Mawasiliano wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu, alithibitisha kuondolewa nchini kwa mkurugenzi huyo.

“Ni kweli mkurugenzi wetu ameondolewa nchini ila kwa maelezo zaidi wasiliana na upande wa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa au mtafute Mindi (Msemaji wa Wizara),” alisema Hoyce.

MTANZANIA lilipomtafuta tena Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mindi ili kuzungumzia sababu za kuondolewa kwa kiongozi huyo, hakuwa tayari kuzungumza suala hilo ila alithibitisha kuondolewa kwake.

“Ni kweli (Mkurugenzi wa UNDP) ameondolewa nchini, ila sasa sababu mimi binafsi sijazijua, anayetakiwa kuzieleza ni Katibu Mkuu, hivyo kama atasema tutauleza umma,” alisema Mindi.

Alipotafutwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Suzan Kolimba kwa simu, alisema kwa sasa hajui lolote kuhusu suala hilo.

“Sina taarifa hizo, nipo bungeni labda kwanza nifanye ‘follow up’ kisha ndiyo nikwambie, au nitamwagiza mkurugenzi atakupatia taarifa tu usijali,” alisema Dk. Suzan

 

Akizungumzia kuondolewa kwa kiongozi huyo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Aziz Mlima, alisema kuwa kulitokana na kuibuka kwa mgogoro kati yake na wafanyakazi wa UNDP waliopo nchini.

Dk. Mlima alisema baada ya kuibuka kwa mgogoro huo, Serikali iliamua kuandika barua Umoja wa Mataifa ikitaka kuondolewa kwa mkurugenzi huyo.

“Unajua unapokuwa na kiongozi kama huyo ana kinga ya ubalozi, ni lazima ufuate taratibu na si vinginevyo, hivyo baada ya tukio hilo tuliandika barua kati ya Aprili 6 au 7 na kuomba kuondolewa kwa kiongozi huyo.

“Na kikubwa unapokuja katika nchi kama yetu ni lazima ushirikiane na Serikali iliyopo na si vinginevyo na kwenda kinyume ni sawa na ukwamishaji wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2020. Na UNDP ni mbin mkubwa wa maendeleo kwa nchi yetu, ila kama unakuja tofauti na maelengo na kazi za UNDP, huku ni kuleta mgogoro,” alisema Dk. Malima.

Alisema mara nyingi Serikali imekuwa ikitoa heshima zote kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa ikiwamo UNDP, lakini pindi inapobainika yanakwenda kinyume na malengo ya kazi, katu Serikali haiwezi kuruhusu hali hiyo.

 

TAARIFA ZA NDANI

Chanzo cha kuaminika kiliiambia MTANZANIA kuwa sababu ya kuondolewa kwa mkurugenzi huyo ni pamoja na hatua yake ya kuingilia baadhi ya mambo katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, mwaka 2015 pamoja na ule wa marudio wa Machi 20, mwaka jana.

Hatua hiyo inaelezwa kutowafurahisha baadhi ya viongozi wa Serikali.

“Kuondolewa kwa mkurugenzi huyo kumechangiwa pia na alichoandika katika ripoti yake kwenye Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu utata wa uchaguzi huo ambao Maalim Seif Sharif Hamad, aliulalamikia na kudai yeye ndiye mshindi.

“Si hilo tu, pia inaelezwa kuwa yapo baadhi ya matukio ambayo anatajwa nayo moja kwa moja ikiwemo kuwasikiliza baadhi ya viongozi walioshiriki uchaguzi na kushindwa, ikiwemo kuwapa mbinu za namna ya kuwasililisha malalamiko yao kwa vyombo vya kimataifa.

“Je, hata kama ungekuwa wewe unaingiliwa mambo yako ya ndani na mtu ambaye si raia wa nchi yako, unaweza kuvumilia? Jibu jepesi hapana,” kilisema chanzo hicho.

Agosti 2016, Maalim Seif alifanya ziara kimataifa katika nchi za Marekani, Ulaya, Canada na Umoja wa Mataifa kulalamikia uvurugaji wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Kutokana na malalamiko yake, taasisi ya kimataifa ya Umoja wa Wanaliberali – Liberal International (LI) imeliandikia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) kutaka kutolewa kwa vikwazo dhidi ya Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taarifa iliyopatikana kwenye tovuti ya LI, taasisi hiyo imetaka baraza hilo lenye jukumu la kulinda misingi ya haki za binadamu kwenye mataifa yote wanachama wa UN, kuchukua hatua kali ili kukomesha ilichokiita uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu na ukandamizaji wa haki za kisiasa na kiraia visiwani Zanzibar.

Katika tamko walilolitoa na kufikishwa mbele ya mkutano wa 33 wa baraza hilo uliofanyika Septemba mosi mwaka huu, Liberal International imetaka jumuiya ya kimataifa kufikiria kuweka vikwazo vya kusafiri na kuzuia mali za watu wote walioshiriki kuidhinisha vitendo vya utesaji wanasiasa wa upinzani na wafuasi wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles