Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imeamua mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuendelea kama kawaida baada ya Jaji Edwin Kakolaki wa mahakama hiyo kusema hakuna suala la dharura la kusitisha uchaguzi huo kwa sasa.
Mgombea aliyeenguliwa katika uchaguzi wa TFF uliopangwa kufanyika Agosti 7, mwaka huu kwa kutokidhi vigezo vya kikanuni, Ally Saleh alifungua kesi mahakama kuu kupinga kanuni na muundo wa TFF.
Kesi hiyo ilisikilizwa leo Ijumaa chini ya Jaji Kakolaki ambaye aliwasikiliza mawakili wa pande zote mbili, TFF ikiwakilishwa na mawakili wanne.
Jaji Kakolaki amesema kesi ndogo ya kusitishwa kwa mchakato wa uchaguzi wa TFF na ile ya msingi zitasikilizwa Julai 9, 2021.
Akizungumza baada ya kutoka mahakamani, Ally Saleh, amesema wanaheshimu uamuzi wa Jaji, lakini bado kuna jambo la msingi katika kesi yao kubwa lakini wanasubiri.