ARIZONA, MAREKANI
SENETA John McCain wa Marekani amevikingia kifua vyombo vya habari baada ya shambulizi la karibuni kutoka kwa Rais Donald Trump, akionya kuwa udikteta huanza kwa namna hiyo.
“Rais wa Marekani ameendelea kuvishambulia vyombo vya habari na wanahabari akisema kupitia akaunti yake ya tweeter kuwa ni maadui wa watu wa Marekani.hii haikubaliki,” alioonya.
Aidha hivi karibuni, Trump aliuambia umati mjini Florida ‘wanataka kuzungumza nanyi bila kuchuja taarifa za uongo.”
Trump aliongeza: “Wamekuwa sehemu kubwa ya tatizo. Ni sehemu ya mfumo wa kifisadi,” alisema.
Lakini Seneta McCain, mgombea urais wa zamani kupitia Chama cha Republican, alisema “uhuru wa habari ni muhimu na tunapaswa kuulinda”.
Mkosoaji huyo wa muda mrefu wa Trump, alikiri binafsi kuvichukia vyombo vya habari, lakini alisema bila wanahabari, ukombozi wa watu wengi utapotea.
Na alionya: ‘hii ndiyo namna udikiteta unavyoanza.”
McCain alisema haamini kama Trump anataka kuwa dikteta, lakini alisema ‘tunahitaji kujifunza kutokana na historia.’
McCain, ambaye aligombea na kushindwa urais na Barack Obama mwaka 2008, alisema: “madikteta walianza kwa kukandamiza uhuru wa habari. Kwa maneno mengine, kujidhatiti madarakani.”
“Wakati ukiangalia historia, kitu cha kwanza madikteta walichofanya ni kuvifunga vyombo vya habari. Hii ni hatari,” alisema katika mahojiano na televisheni ya NBC.