25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI AJIUZULU, AJIUNGA NA WAASI SUDAN KUSINI

JUBA, SUDAN KUSINI


WAZIRI wa Kazi nchini Sudan Kusini, Luteni Gabriel Duop Lam, amejiuzulu na kujiunga na kundi la waasi wa nchi hiyo.

Katika barua aliyomtumia Rais Salva Kiir, Luteni Lam alisema ameungana na kundi la waasi linaloongozwa na aliyekuwa Makamu wa Rais Riek Machar.

“Nakiri uaminifu na kujitoa kwangu kuhudumu chini ya uongozi wa hekima wa Mheshimiwa Dk. Riek Machar,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo, ambayo vyombo vya habari vya hapa na kigeni viliiona.

Waziri huyu ni ofisa wa pili wa ngazi ya juu kujiuzulu kutoka serikali ya taifa hili lenye utajiri mkubwa wa mafuta, ambalo linashuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka minne.

Vita hiyo inayofuata mkondo wa kikabila iliyoanza Desemba 2013, imesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni moja na kukosesha makazi wengine zaidi ya milioni tatu.

Ilitokea baada ya Rais Kiir anayetoka kabila la Dinka kumfuta kazi Machar, aliyekuwa makamu wake, ambaye anatokea kabila la Nuer.

Desemba 2016 Umoja wa Mataifa (UN) ulionya kuwa kinachoendelea hapa huenda kikageuka kuwa mauaji ya halaiki.

Msemaji wa Serikali, Michael Makuei Lueth alithibitisha kujiuzulu kwa Lam siku ya Ijumaa.

Siku sita zilizopita Luteni Jenerali Thomas Cirillo Swaka, ambaye alikuwa naibu msimamizi wa idara ya uchukuzi jeshini, ajiuzulu wadhifa huo.

Hata hivyo, hakusema iwapo anajiunga na kundi la waasi linaloongozwa na Dk. Machar.

Swaka alieleza kuchukizwa na visa vya ukiukaji wa haki za binadamu katika jeshi la Sudan Kusini.

Aliongeza Rais Kiir amekuwa akiteua watu kutoka kabila lake la Dinka kushikilia nyadhifa kubwa katika jeshi hilo.

Wakati huo huo, makamanda zaidi wa jeshi wamejiuzulu nchini Sudan Kusini juzi.

Makamanda hao wamejiondoa serikalini wakimlaumu Rais Kiir kuhusika katika uhalifu wa kivita na mauaji yanayolenga kabila fulani.

Brigedia Henry Oyay Nyago, anamshutumu Rais, ambaye anatoka katika kabila la Dinka, kwa kuamuru kuuawa kwa watu wasiotoka katika kabila hilo.

Kanali Khalid Ono Loki, pia anamlaumu liongozi mkuu wa jeshi kwa mauaji ya kimbari, kukamatwa na kuwafunga watu kiholela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles