23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mbwana Samatta aipeleka Mazembe fainali Afrika

samattaNA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

MABAO mawili yaliyopachikwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, yalichangia ushindi wa 3-0 na kuipeleka Klabu ya TP Mazembe kwenye fainali ya Klabu Bingwa Afrika.

TP Mazembe ikicheza kwenye uwanja wake wa nyumbani jijini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, iliifunga El Merreikh ya Sudan katika mchezo wa pili wa nusu fainali iliyochezwa jana.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa jijini Khartoum, TP Mazembe ililala 2-1 huku bao la pekee likifungwa na Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu, kabla ya kuzinduka jana katika mchezo wa marudiano na kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2.

Mazembe ina kibarua kizito kwenye fainali kwani itakutana na timu bora kutoka Algeria USM Alger, iliyotinga fainali kwa kuitoa timu nyingine ya Sudan, Al Hilal, kwa jumla ya mabao 2-1.

Mchezo wa kwanza wa fainali umepangwa kufanyika kati ya Oktoba 30 na Novemba Mosi mwaka huu jijini Algiers na marudiano kuchezwa jijini Lubumbashi kati ya Novemba 6 na 8 mwaka huu.

Hii ni mara ya kwanza kwa wachezaji wa Kitanzania kucheza fainali ya michuano hiyo mikubwa tangu ibadilishwe na kuanza kutumia mfumo mpya mwaka 1997.

Samatta aliyekuwa kwenye kiwango bora katika mchezo wa jana alifunga mabao hayo dakika ya 53 na 69 huku bao lingine likipachikwa na mshambuliaji Roger Assale.

Chachu ya ushindi wa TP Mazembe ni mabadiliko yaliyofanywa kipindi cha pili kuwaingiza Assale na Ulimwengu ambao waliongeza kasi kwa timu hiyo.

Mara ya mwisho TP Mazembe kutinga fainali ya Klabu Bingwa Afrika ni mwaka 2010 walipotwaa taji hilo na kisha kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kucheza hatua ya fainali michuano ya Klabu Bingwa Dunia na kufungwa na miamba ya Italia, Inter Milan, 3-0.

Samatta anazidi kuipaisha jina lake katika soka la Afrika kwani ‘hat-trick’ (mabao matatu) yake iliiwezesha TP Mazembe kuichapa Moghreb Tetouan ya Morocco mabao 5-0.

Vitu vinavyofanywa na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ni sawa na kuanza kuijibu kwa vitendo kauli yake aliyoiambia MTANZANIA Septemba 17 mwaka huu, kuwa anachoangalia hivi sasa ni kuiachia taji la michuano hiyo TP Mazembe kabla ya kutimkia Ulaya mwakani atakapomaliza mkataba wake.

“Mimi kiukweli ningependa niiachie TP Mazembe kombe la haya mashindano makubwa Afrika kwa ngazi za klabu, nitahakikisha nashirikiana na wachezaji wengine kutimiza hilo,” alisema.

Wakati mkataba wake ukiwa ukingoni, tayari mshambuliaji huyo ameweka wazi kuwa hataongeza mkataba mwingine TP Mazembe huku akiwa na mipango ya kutimkia barani Ulaya, anapowaniwa na baadhi ya timu kutoka ligi kuu za Ufaransa, Ubelgiji na Ureno.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles