JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA
NI ni simulizi ya kweli na aina yake, ambayo kwa sanamu, filamu zimetengenezwa na vitabu kuandikwa kuhusu mbwa huyu wa Kijapan aina ya Akita – Hachiko au maarufu kwa jina la Hachi.
Simulizi hii ya miongo mingi iliyopita, inamfanya Hachi ahesabiwe kuwa mbwa mwenye upendo na mwaminifu kuliko wote duniani.
Mbwa huyu, ambaye simulizi zake iwe kitabuni au kwenye filamu huwatoa wengi machozi, alizaliwa huko Ōdate nchini Japan Novemba 10, 1923, miezi miwili tu baada ya lile tetemeko kubwa la ardhi la Kanto.
Katika umri wa miezi miwili aliasiliwa na Professa Hidesaburō Ueno (1872-1925) mjini Tokyo na hivyo Januari 14, 1924 Hachi akaondoka kwao Ōdate na kuwasili Stesheni ya Reli ya Shibuya baada ya safari ya treni ya saa 20.
Kwa vile Professa Ueno alikuwa mpenzi mkubwa wa mbwa na tayari alikuwa na mbwa wengine wawili – John na S. John, haikushangaza alipomchukua dogo Hachi.
Wakati akiwa mdogo mara nyingi Hachi aliugua hasa maradhi ya tumbo na homa. Ueno anasemekana alimuuguza usiku kucha kitandani mwake, akimwangalia kwa karibu kana kwamba yu mtoto mchanga.
Ijapokuwa yeye na mkewe Yaeko waliasili binti, hawakufanikiwa kuzaa mtoto.
Hachi haikuchukua muda akaanza kuongozana na Ueno kwenda Stesheni ya Shibuya asubuhi na kurudi nyumbani baada ya kumsindikiza bwana wake huyo na jioni alifika stesheni hapo kumpokea Ueno arudipo kutoka kazini.
Hata hivyo, Hachi hakuwa pekee, mbwa wengine John na S – mara nyingi waliambatana naye.
Kila alipopanda gari moshi na kuagana na mbwa wake hao katika Stesheni ya Shibuya, aliwapatia biskuti, akiwasemesha na kuwapiga piga nao walimrukia rukia. Hakujali kuchafuka nguo!
Pia aliwahi kwenda nao hadi getini mwa Idara ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Tokyo, ambako Profesa Ueno alifanya kazi.
Siku moja ya huzuni Mei 21, 1925 ilifika, ni mwaka mmoja na miezi minne tangu Hachi awe sehemu ya maisha ya Ueno.
Profesa Ueno alianguka ghafla wakati akitoa mhadhara darasani na kufariki dunia papo hapo kwa shambulio la moyo akiwa na umri wa miaka 53.
Jioni ya siku hiyo, Hachi akiwa hana hili wala lile kama kawaida alienda kumpokea Ueno lakini bila mafanikio.
Kwa mujibu ya simulizi za mke wa marehemu, Yaeko Ueno, Hachi alilala katika kapu lenye nguo alizovaa Ueno mara ya mwisho na aligoma kula kwa siku tatu.
Usiku mmoja wakati wa kumwombea Ueno, Hachi, alikuwa akizurura bustanini akiwa na huzuni na ghafla alifungua mlango na kuingia chumbani walimokuwa wakifanyia maombolezo.
Alijilaza chini ya meza, ambayo jeneza lenye mwili wa Ueno liliwekwa. Alinyoosha miguu na kutuliza kichwa chake katika miguu hiyo na alikaa hapo kwa usiku mzima. Kwa kuona namna Hachi alivyokuwa karibu na Ueno, kila mmoja chumbani alimwaga machozi.
Kwa sababu ya kukataliwa na familia ya Ueno, kwani Professa Ueno na mkewe Yaeko walikuwa hawajaoana rasmi. Hivyo, Yaeko hakuwa na haki ya kisheria na mali za Ueno baada ya kifo chake na hivyo hakupaswa kuishi katika makazi ya Ueno.
Ilibidi aondoke na mbwa huyo kwenda naye katika nyumba ya kupanga.
Dogo Hachi aliishi na Yaeko kwa kuhama hama; akianzia Nihombashi, kisha Asakusa. Wakati nyumba yake mpya ilipokuwa tayari Yaeko alirudi na Hachi kitongoji cha Setagaya, kilomita tano tu kutoka yalipokuwa makazi ya Ueno.
Haikuchukua muda Hachi akaanza kwenda Stesheni ya Shibuya mara mbili kwa siku asubuhi na jioni, akifuata ule utaratibu wakati akimsindikiza na kwenda kumpokea Ueno huku akipita kwenye makazi ya Ueno. Pamoja na juhudi za Yaeko kumzuia, Hachi kamwe hakuacha hija yake hiyo ya kila siku.
Yaeko alihofia uchovu wa kutembea umbali mrefu wa jumla ya zaidi ya kilomita 20 kila siku utamwathiri Hachi kiafya, hivyo ili kumuokoa na hali hiyo, akatafuta mtu stahili anayeishi karibu na stesheni ili asisumbuke umbali mrefu kutoka Setagaya hadi stesheni hapo. Hii ilikuwa karibu miaka miwili tangu kifo cha Ueno.
Mtu huyo aliyepewa kazi ya kukaa naye alikuwa Kikusaburō Kobayashi, ambaye alikuwa akifanya kibarua cha kukata miti na michongoma katika makazi ya Ueno.
Wakati alipokuwa akijaribu kujiimarisha kibiashara ni Ueno aliyemsaidia Kobayashi. Hivyo, Kobayashi alihisi ana deni kubwa kwa Ueno.
Akiishi jirani na stesheni hiyo, ni yeye aliyempokea Hachi Stesheni wakati alipowasili kutoka Odate, Januari 14, 1924.
Hivyo, Yaeko hakukosea kumwamini Kobayashi, alikuwa mtu sahihi kwani alimjua vyema Hachi na hivyo alimtunza na kumlisha vyema.
Nyuma ya nyumba ya Kobayashi, kulikuwa na bucha iliyoendeshwa na wenzi wawili, ambao hawakubarikiwa watoto, na walimpenda Hachi.
Hachi mara nyingi alionekana akitembea na watoto wa nyumba jirani kwenda ‘viwanja.’
Hata hivyo, licha ya maisha mazuri aliyoishi, hayakumzuia kuendelea na hija yake katika Stesheni ya Shibuya mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni kwa muda ule ule, ambao Professa Ueno alizoea kuondoka na kurudi.
Siku, wiki na miaka ikapita. Si wote walikuwa wema kwa Hachi. Siku moja alikamatwa na kutupwa katika ‘jela’ ya mbwa wazuraraji, lakini aliachiwa baada ya Konstebo mmoja wa polisi kumgundua.
Kwa mujibu wa rekodi, Hachi hakuwahi kumshambulia mtu hata pale alipotendewa ukatili.
Ni Hirokichi Saitō, aliyeishi miaka 1899-1964 aliyekuwa chanzo kikuu cha umaarufu wa Hachi nchini humo na katika ulimwengu wa filamu.
Mwanakampeni huyo wa matunzo ya mbwa wa Kijapan aliyeanzisha Chama cha Kutunza Mbwa wa Kijapan mwaka 1928 baada ya kumwona Hachi na kusikia habari zake, akamwendea Kobayashi kumtaka amwachie aishi naye.
Hata hivyo, Kobayashi alikataa, akisema marehemu Professa Ueno alimpenda mno Hachi kiasi kwamba aliacha wosia kuwa azikwe kando yake iwapo atafariki. Saitō akamwandika Hachi mara mbili katika jarida la chama chake.
Kwa mujibu wa Saito, Hachi alikuwa mbwa mpenda haki na amani. “Wakati mbwa wawili walipoanza kupigana, Hachi daima alijiweka katikati ya mapigano hayo ili kuyazuia.
Iwapo mbwa mmoja atasisitiza kushambulia, Hachi aliingilia kati ili asitoke mshindi.
Akiwa anazeeka na dhaifu huku jicho moja likiwa na jeraha na matatizo ya kuona, Hachi hakukoma kwenda stesheni ya Shibuya kumsubiri bwana wake mpendwa.
Makala inayosimulia mbwa anayemsubiri bwana wake katika stesheni ya gari moshi ikapata umaarufu mkubwa katika magazeti makubwa kama Asahi Shimbun, ambalo lilitoa makala Oktoba 4, 1932.
Nyendo zake hizo ziligusa kila kiumbe kilichomwona stesheni hapo wakiwamo watu waliofunga safari za mbali kuja kumwona, wengi walimwaga machozi.
Umaarufu wa Hachi uliifanya Shesheni ya Shibuye iamue Hachi mzee aishi ndani ya jengo usiku.
Ofisa mmoja aliajiriwa kumtunza na kumlinda Hachi, ambaye ameonekana katika filamu kama The Boss of Alps na miaka ya karibuni karibuni filamu nyingi zikiwamo za Hollywood zimemwangazia.
Mnamo Februari 6, 1934 aliugua, wengi wakiwamo watoto walimiminika stesheni kuchangia fedha za matibabu yake huku maombi yakifanyika ili apone. Kwa furaha ya kila mtu, alipona kimiujiza.
Machi 10, 1934, tukio la kuchangisha fedha lilifanyika kwa ajili ya kumtengenezea sanamu. Hachi, Mjane wa Ueno na Saitō ambaye ndiye aliyemfanya Hachi ajulikane walikuwepo katika tukio hilo lililovuta watu 3,000.
April 21, 1934, sanamu ya shaba ya Hachi ilizinduliwa, akiwa bado hai. Saa 12 asubuhi ya Machi 8, 1935, Hachi alikutwa akiwa amefariki dunia katika upenu wa duka moja la vileo.
Ni mkabala na stesheni ya Shibuya nyuma ya njia ya reli ambayo kwa kawaida Hachi akifahamu si salama, hakuthubutu kuitumia.
Wataalamu wa wanyama wa mbwa wanasema inawezekana Hachi aliamua kwa makusudi kuendana na msemo ‘mbwa hawapendi kuchafua mazingira ya familia zao kwa miili yao mfu.’
Eneo ilipo sanamu ya Hachiko nje ya Stesheni ya Shibuya, kwa sasa kwa heshima wake limegeuka mahali ambako kila siku watu huenda kuwasubiri marafiki au wapendwa wao, kama alivyofanya Hashi wakati wa uhai wake.
Chuo Kikuu cha Tokyo alichofanya kazi Professa Ueno pia kina sanamu na kumbukumbu zao.