28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

UKIOA KWA WABANYANKOLE NI LAZIMA ‘UPUMZIKE’ NA MKWEO

HASSAN DAUDI NA MITANDAO


KILA kabila duniani huwa na utamaduni wao, ingawa wapo ambao hufuata tamaduni zao na wengine huzipuuza.

Utamaduni hutofautiana kutoka jamii moja na nyingine. Mfano; wakati India ikizoeleka kuona mwanamke akitoa mahari, iko tofauti hapa nchini, kwani ni wanaume ndio hufanya hivyo.

Kwa muktadha huo, si ajabu kuona jambo linalokubalika katika eneo fulani likipigwa vita na kuonekana lisilo na maana kwa jamii nyingine ingawa bado litabaki kuheshimiwa kwa watu wake.

Nchini Uganda, ambako kunaelezwa kuwa na makabila zaidi ya 35, kuna jamii ya Wabanyankole ambayo upekee wa utamaduni wake umewaduwaza wengi.

Hao wanapatikana Kusini-Magharibi mwa taifa hilo, eneo ambalo liko Mashariki mwa Ziwa Edward na watu wake huzungumza Kibantu.

Ni jamii inayokusanya makabila makubwa mawili, Bahima ambao licha ya kuwa ni wafugaji, pia ndiyo wanaoshikilia nyanja za utawala na Bairu wanaojishughulisha na kilimo.

Kinachowaacha hoi watu wa jamii zingine ni utamaduni wao wa suala la ndoa.

Pindi mtoto wa kike anapoolewa, mila na desturi zinamtaka shangazi yake kufanya mapenzi na bwanaharusi, ikielezwa kuwa yeye ndiye hupima uwezo wa kushughulika alionao mwanamume huyo.

Wakati huo huo, inaelezwa pia kuwa shangazi anatakiwa kushiriki tendo la ndoa na mkwewe kabla ya wanandoa hawajajipumzisha kwa mara ya kwanza baada ya harusi.

Katika hilo, wapo pia wazee wa kabila hilo wanaoamini kuwa si lazima shangazi afanye tendo lenyewe, bali apewe muda wa kusikiliza na kuona kinachoendelea wakati wawili hao wakiwa katika tendo la ndoa.

Kabila hilo linampa jukumu kubwa shangazi kuhakikisha binti anayeanzia umri wa miaka nane anaitunza bikra yake hadi pale anapoolewa.

Wakati watoto wa kike wenye umri huo katika makabila mengine wakiwa huru kucheza, wale wa Wabanyankore hufungiwa ndani, wakilazimishwa kula nyama, uji wa ngano na kunywa maziwa.

Shangazi huwa mkali zaidi pale binti anapoanza kuota maziwa, msisitizo mkubwa ukiwa ni kuhakikisha hajihusishi kabisa na vitendo vya ngono.

Kwa wanaume, kijana wa Banyankole huwa hatafuti mke na wala hajishughulishi kulipa mahari, kazi hiyo hufanywa na baba yake ambaye hutoa ng’ombe, mbuzi au pombe.

Inaelezwa kuwa kijana wa kiume anaruhusiwa kutumia nguvu kulazimisha kuoa au kutoka kimapenzi na msichana aliyemkataa.

Katika jamii hiyo, ndoa isiyo na watoto ni fedheha kubwa kwa mwanaume na mwanamke. Mwanamume ambaye mkewe ana tatizo la kutoshika mimba (ugumba), huruhusiwa kuoa mke wa pili lakini si zaidi ya hapo.

Kama zilivyo tamaduni nyingi, wanandoa hujivunia zaidi kupata mtoto wa kiume, wakiamini ndiye atakayeendeleza mali na kumlinda mama yake pindi mzee atakapofariki.

Kwa upande mwingine, tofauti na tamaduni nyingi, Wabanyankole hawaamini kuwa kifo ni mipango ya Mungu ikiwa aliyefariki si mzee.

Wanapofikwa na msiba, wao huuchukua mwili wa marehemu na kwenda nao kwa mganga wa kienyeji ili kujua aliyemuua. Hatua hiyo hufuata baada ya ile ya kuwaita ndugu wote ambapo asiyefika huonekana kuwa ndiye mchawi mwenyewe.

Lakini sasa, kwa aliyejinyonga huwa ni tofauti kidogo kwani wakati bado akiwa ananing’inia, watu huchimba shimo chini ya mti alioutumia.

Kisha mmoja kati ya waombolezaji hukata mti ili mwili wake utumbukie moja kwa moja bila kuguswa kwa mikono na hakuna matananga baada ya hapo, kila mtu huelekea katika mizunguko yake.

Hata hivyo, kwa mila na desturi zao, si kila mtu anapaswa kwenda kukata mti. Anayepewa nafasi ya kufanya kazi hiyo ni mwanamke aliyemaliza kuzaa. Ni kwa sababu inaaminika kuwa yeyote anayekata mti, basi naye atafariki siku chache baadaye.

Aidha, ifahamike kuwa mila za Wabanyankole zinapiga marufuku miti yote iliyokatwa kwa shughuli hiyo kutumika kama chanzo cha kuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles