Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MBUNGE wa Ulanga, Goodluck Mlinga (CCM), amegeuka mbogo kwa kudai walimu wa shule za msingi wamekuwa wakiwafundisha wanafunzi kwa kutumia ramli kutokana na kutokuwa na mitaala ya kufundishia.
Kwa sababu hiyo, alimwomba Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, awatoe bungeni Waziri wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia na naibu wake hadi watakapokuwa na majibu ya kuridhisha ni kwanini hakuna mitaala ya kufundishia pamoja na vitabu.
Akiomba mwongozo huo bungeni jana, Mlinga alidai linapozungumziwa suala la elimu ya sekondari na vyuo, msingi wake ni elimu ya msingi.
“Lakini mheshimiwa mwenyekiti mpaka hivi sasa ninapozungumza, darasa la nne hawana mitaala wala hawana vitabu, kwa maana hiyo hawasomi.
“Walimu wamekuwa wakiwafundisha kwa kupiga ramli na wanafanya mtihani mwezi wa 11, lakini mpaka sasa hawana mitaala wala vitabu.
“Na cha kusikitisha, hapa ndani namwona waziri na naibu waziri, wala hawatikisiki… nilikuwa naomba mwongozo wako kwa kuwa Bunge kazi yake ni kuisimamia Serikali na si kuiangalia.
Mlinga ambaye hujenga hoja zenye utata alisema: “Naomba kwa kutumia mamlaka yako, utoe maagizo naibu waziri na waziri wasiingie humu ndani mpaka waje na majibu.”
Akijibu mwongozo huo, Chenge alisema suala hilo ni nyeti na linatakiwa liangaliwe na kutolewa ufafanuzi na Serikali.
“Suala la Mlinga ameliweka kwa utani, lakini Serikali muone namna gani mnaweza kulitolea ufafanuzi, naamini mmemwelewa vizuri,” alisema Chenge.
Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William ole Nasha, alisema kwa sasa hakuna ukosefu wa mitaala na kwamba wizara inaendelea na taratibu za kuboresha iliyopo.
“Niseme tu kwamba madai yake kwa sasa hatuna mtaala ambao umekosekana, hata hivyo wizara inaendelea na taratibu ya kuboresha mitaala iliyopo.
Kuhusu vitabu, ole Nasha alisema vitabu vilichelewa lakini kwa sasa vimeanza kugawiwa shuleni.
“Vitabu ambavyo vilikuwa vimechelewa kwenda shuleni ni vitabu vya darasa la nne, naomba nimuhakishie mheshimiwa mbunge na Bunge lako tukufu, kwamba vile vitabu ambavyo vilichelewa kwa sasa vimeanza kugaiwa shuleni.
“Na tunaamini ndani ya wiki nne vitakuwa vimesambaa nchi nzima na tayari tumegawa katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na bado utaratibu unaendelea wa kuvigawa katika maeneo mengine,” alisema ole Nasha.
Wakati huo huo, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma (CCM), aliomba mwongozo bungeni jana akiitaka Serikali ibadilishe muhula wa masomo uwe mara tatu kwa mwaka.
Akiomba mwongozo huo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Musukuma alihoji ni kwanini Wizara ya Eimu isirudishe utaratibu wa zamani wa mihula mitatu.
Akijibu mwongozo huo, Chenge alisema suala hilo anaiachia Serikali kama itaona linafaa.
Katika majibu yake, Naibu Waziri ole Nasha, alisema Serikali haiwezi kufanya hivyo kwa sababu hayo ni mabadiliko ya tabianchi.