26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

JAJI DAMIAN LUBUVA: TUME YA UCHAGUZI YA TAIFA IKO HURU

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI mstaafu wa Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva amesema tume hiyo   ni huru isipokuwa ni maono ya watu kwa kutokuwapo neno ‘huru’.

Amesema hata nchi ambazo tume zao  zina neno huru,  kwa uhalisia si huru kwa sababu uchaguzi wao umekuwa ni wa vurugu.

Jaji Lubuva ambaye alipata kuwa Mwanasheria wa Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar na baadaye Tanzania Bara, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Oysterbay,   Dar es Salaam juzi.

“Nisingependa sana kulizungumzia hili kwa sasa kwa sababu wenzangu wapo wangelizungumzia.

“Lakini hata hivyo ni kweli mwenyekiti na makamishna wote wa tume wanateuliwa na rais, lakini tangu iliponzishwa mwaka 1992 tume ilikuwa ikifanya kazi zake kwa uhuru.

“Haikuwahi kuingiliwa na mtu yeyote, ni huru na inasimamia uchaguzi kwa uhuru bila kuelekezwa na mtu yeyote aliyeko madarakani, hiyo ndiyo maana ya tume huru.

“Iko hoja usipoandika tume huru kama ya Kenya, unaweza kuona kwamba pamoja na kutajwa kwenye sheria ni huru kumbe haziko huru hata kidogo.

“Kilichopo ni maono ya watu, kwenye fikra zao wanafikiria kwamba mwenyekiti, wakurugenzi na makamishna wa tume wote wanateuliwa na rais hivyo wanadhani kwamba watapendelea mtu fulani.

“Lakini kwa ukweli tume yetu ni huru pengine kuliko za nchi nyingine …na Kenya mlishuhudia ilivyokuwa ingawa tume yao ina neno huru,”alisema Jaji Lubuva.

Mwanasheria huyo nguli alisema kama ni kubadilishwa ni suala la kuangalia muda muafaka kwa sababu inahusu katiba.

“Sasa kama ni kubadilishwa ni suala la kuangalia muda muafaka kwa sababu ni suala la katiba, lakini jinsi katiba na sheria zilivyo nasema kwa nguvu zote kuwa tume yetu ni huru.

“Tumekaa miaka minne na JK (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete), lakini hajawahi kuniita hata siku moja akanipa maelekezo yoyote kuwa pendelea fulani.  Bila hata neno huru tume iko huru kabisa,”alisisitiza  Jaji Lubuva.

Aprili 12, mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai alitupilia mbali hoja ya Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), kuhusiana na marekebisho ya masuala yanayohusu Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza bungeni   baada ya kumalizika  kipindi cha maswali na majibu, alisema anaikataa taarifa ya mbunge huyo na akajipange upya.

“Kwa hiyo taarifa yako Mheshimiwa Kubenea naikataa kwa hiyo kajipange tena, kama bado una nia, uje katika utaratibu unaotakiwa kama hatukukuelewa tutatafuta muda  tueleweshane zaidi ila sisi tumeelewa hivyo.

“Mheshimiwa Saed Kubenea ameleta kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka Bunge lifanye marekebisho ya masuala yanayohusiana na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

“Ili ikidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi   nchini sasa kwa kuwa Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa na Katiba katika ibara ya 74 marekebisho yote juu ya tume hiyo yanatakiwa kuletwa kwa kupitia muswada wa marekebisho ya Katiba na siyo hoja binafsi ya mbunge,” alisema.

Alisema  alichokisema Kubenea ni jambo linalohusu Katiba hivyo    upo utaratibu wa kuafuata   kuendana na mabadiliko hayo ya katiba ya nchi.

Spika Ndugai, alisema wabunge wamekuwa wakipata shida ya jinsi ya kuwasilisha hoja binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles