MBUNGE wa Viti Maalum, Anatropia Theonest (Chadema) yuko hatarini kuadhibiwa tena endapo itathibitika kuwa alimvua kofia ya balagashia, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Milinga (CCM) ndani ya ukumbi wa Bunge.
Wiki iliyopita, Bunge lilimpa adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu mfululizo na kukatwa mshahara na posho zote anazozipata katika siku hizo ambazo hatahudhuria vikao vya Bunge, kuanzia Juni 17 hadi 22 mwaka huu.
Hali hiyo ilijitokeza siku ambayo mbunge huyo alikuwa anamaliza adhabu yake aliyopewa na Bunge baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtia hatiani kwa kusema uongo dhidi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Jana, Milinga aliomba mwongozo kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson baada ya kipindi cha maswali na majibu akimlalamikia Anatropia kuwa alimvua kofia hiyo akiwa bungeni na kumsababishia usumbufu.
Alisisitiza kuwa kama asingepata mtu wa kumuazima kofia nyingine ya aina hiyo angekosa sifa ya kuendelea kubaki bungeni kwa mujibu wa kanuni za Bunge na aina ya vazi alilokuwa amevaa.
Akitumia Kanuni ya 67(8), aliomba mwongozo huo huku akitoa maelezo marefu kuhalalisha hoja yake.
“Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wabunge wa kambi ya upinzani wakitoka nje, kundi la wabunge wa Chadema likiongozwa na Anatropia Theonest walifika mezani kwangu naye akanivua balagashea yangu kama hii niliyovaa ambayo nimepewa na msamaria mwema nje niweze kuhudhuria kikao hiki cha Bunge,” alieleza Mlinga.
Alisema Anatropia alitokomea kusikojulikana akiwa na kofia hiyo.
Mbunge huyo alichambua athari zilizotokana na kitendo hicho kuwa ni pamoja na kumfanya akose sifa za kuwa bungeni wa mujibu wa kanuni kwa kuwa inatakiwa mbunge akivaa kanzu ahakikishe amevaa vazi rasmi ambalo ni kanzu na kofia ya aina hiyo.
Alitaja athari ya pili aliyoipata kuwa ni kuwakosesha kwa muda, wananchi wa Ulanga uwakilishi bungeni kwa vile kitendo chake hicho kilimsababishia mtikisiko wa mawazo na hadi wakati akizungumza bungeni hakuwa akifahamu nia yake ilikuwa ni nini.
“Kitendo hiki ni kukosea heshima vazi langu hilo kwa sababu kwa mujibu wa utamaduni wa vazi hili tu pekee mwenye mamlaka ya kumvua mwanaume kofia hiyo ni mke wake wa ndoa, kwa kitendo alichofanya Atropia amemkosea mke wangu, Mama Glory.
“Kwa hiyo mbunge huyo aliingia kwenye himaya ya mke wangu bila ridhaa yake na amevunja amri ya tano kati ya amri 10 za Mungu inayozuia mtu kutamani mali, mke au mume wa mtu mwingine.
“Athari ya sita iliyosababishwa na mbunge huyo ni kuvunja msimamo wa chama chake wa kutowakaribia wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mheshimiwa Naibu Spika naomba mwaongozo wako kwamba je, vitendo hivi vinaruhusiwa kwenye Bunge lako tukufu?” alimaliza.
Dk. Tulia wakati akijibu mwongozo huo alimuuliza Mlinga kama tukio hilo lilifanyika ndani ya Ukumbi wa Bunge au nje na Milinga alijibu kuwa ni ndani ya ukumbi huo.
Naibu Spika alisema tukio hilo hajaliona na atakwenda kulifanyia kazi na kulitolea uamuzi.