25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mbunge wa Ukawa kubanwa tena bungeni

Goodluck MilingaNa Arodia Peter, Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum, Anatropia Theonest (Chadema) yuko hatarini kuadhibiwa tena endapo itathibitika kuwa alimvua kofia ya balagashia, Mbunge wa Ulanga, Goodluck Milinga (CCM) ndani ya ukumbi wa Bunge.

Wiki iliyopita, Bunge lilimpa adhabu ya kutohudhuria vikao vitatu mfululizo  na kukatwa mshahara   na posho zote anazozipata katika siku hizo ambazo hatahudhuria vikao vya Bunge, kuanzia Juni 17 hadi 22 mwaka huu.

Hali hiyo ilijitokeza siku ambayo mbunge huyo alikuwa anamaliza adhabu yake aliyopewa na Bunge baada ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumtia hatiani kwa kusema uongo dhidi ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Jana, Milinga aliomba mwongozo kwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson  baada ya kipindi cha maswali na majibu akimlalamikia  Anatropia kuwa alimvua kofia hiyo  akiwa bungeni na kumsababishia usumbufu.

Alisisitiza kuwa kama asingepata mtu wa kumuazima kofia nyingine ya aina hiyo angekosa sifa ya kuendelea kubaki bungeni kwa mujibu wa kanuni za Bunge  na aina ya vazi alilokuwa amevaa.

Akitumia Kanuni ya 67(8), aliomba mwongozo huo huku akitoa maelezo marefu kuhalalisha hoja yake.

“Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wabunge wa kambi ya upinzani wakitoka nje, kundi la wabunge wa Chadema likiongozwa na  Anatropia Theonest walifika mezani kwangu naye akanivua balagashea yangu kama hii niliyovaa ambayo nimepewa na msamaria mwema nje   niweze kuhudhuria kikao hiki cha Bunge,” alieleza Mlinga.

Alisema  Anatropia alitokomea kusikojulikana akiwa na kofia hiyo.

Mbunge huyo  alichambua athari zilizotokana na kitendo hicho kuwa ni pamoja na kumfanya akose sifa za kuwa bungeni wa mujibu wa kanuni kwa kuwa inatakiwa mbunge akivaa kanzu ahakikishe amevaa vazi rasmi ambalo ni kanzu na kofia ya aina hiyo.

Alitaja athari ya pili aliyoipata kuwa ni kuwakosesha kwa muda, wananchi wa Ulanga uwakilishi bungeni kwa vile  kitendo chake hicho kilimsababishia mtikisiko wa mawazo na hadi  wakati akizungumza bungeni  hakuwa akifahamu nia yake ilikuwa ni nini.

“Kitendo hiki ni kukosea heshima vazi langu hilo kwa sababu kwa mujibu wa utamaduni wa vazi hili tu pekee mwenye mamlaka ya kumvua mwanaume kofia hiyo ni mke wake wa ndoa, kwa kitendo alichofanya Atropia amemkosea mke wangu, Mama Glory.

“Kwa hiyo mbunge huyo aliingia kwenye himaya ya mke wangu  bila ridhaa yake na amevunja amri ya tano kati ya amri 10 za Mungu  inayozuia mtu kutamani mali, mke au mume wa mtu mwingine.

“Athari ya sita iliyosababishwa na mbunge huyo ni kuvunja msimamo wa chama chake wa kutowakaribia wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Mheshimiwa Naibu Spika naomba mwaongozo wako kwamba je, vitendo hivi vinaruhusiwa kwenye Bunge lako tukufu?” alimaliza.

Dk. Tulia wakati akijibu mwongozo huo alimuuliza Mlinga kama tukio hilo lilifanyika ndani ya Ukumbi wa Bunge au nje na Milinga alijibu kuwa ni ndani ya ukumbi huo.

Naibu Spika  alisema tukio hilo hajaliona na atakwenda kulifanyia kazi na kulitolea uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles