Na PETER FABIAN-RORYA
MBUNGE wa Jimbo la Rorya, Lameck Airo (CCM) Mkoa wa Mara, amejitolea kugharimia mafunzo kwa madiwani wote wa jimbo lake ili wajifunze namna ya kusimamia miradi ya maendeleo kulingana na thamani ya fedha iliyotolewa na Taasisi ya Governance Links Tanzania.
Airo amefikia uamuzi huo baada ya kubaini kuwepo kwa madiwani ambao hawajawahi kupata semina ya kuwajengea uwezo wa namna ya kusimamia fedha za miradi ya maendeleo kupitia bajeti ya halmashauri hiyo, hivyo kumtumia mtaalamu Donald Kasongi wa Taasisi ya Governance Links Tanzania kuwapatia mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo.
Akizungumza katika semina ya siku moja iliyofanyika wilayani Rorya juzi, Mbunge Airo aliwakumbusha madiwani wajibu wao wa kushirikiana naye kusimamia miradi ya maendeleo ikiwemo suala la mapato na matumizi ya fedha za mapato kwa kuhakikisha zinatekeleza yaliyokusudiwa na kuacha kuingia mitego ya kuihujumu halmashauri kwa kushirikiana na wataalamu.
“Madiwani hapa hakuna cha diwani wa chama fulani ni wajibu wetu wote kuungana kuijenga Rorya yetu hii ndiyo kaulimbiu yetu toka kuanzishwa kwa halmashauri hii miaka tisa iliyopita, hivyo vyama vyetu tuweke pembeni na tuwe na mshikamano wa kusimamia kwa dhati maendeleo ili huduma za jamii zipatikane,”alisisitiza.
Mbunge huyo aliwakumbusha madiwani wote bila kujali itikadi za kisiasa kuwa uamuzi huo wa kupatiwa semina zamani ulikuwa ukitolewa na serikali kupitia TAMISEMI, hivyo gharama hizo za semina hiyo atazitoa ili madiwani wawe na jukumu moja la kusimamia fedha na miradi ya maendeleo kwa weledi.
Naye mtaalamu mwezeshaji akitoa elimu kwa madiwani hao alisema ni wajibu wa madiwani kuiangalia Rorya kwa miaka 20 ijayo na ufatiliaji wa miradi siyo lazima kuwa mnachukua majukumu ya wataalam bali ni wajibu wa kusimamia miradi na maendeleo ya vijiji na kata kufikia lengo halisi na tija.
“Ni lazima kuwa na umahiri wa kutambua na kuzielewa taarifa za wataalam juu ya kutekeleza ujenzi wa miradi kwa kuhakikisha utekelezaji wake unaendana na BQ ambazo ni muhimu kwa madiwani kuomba ili kusaidia kufuatwa kwa ujenzi wa miradi ya maendeleo katika sekta zote za utolewaji huduma ili kuondoa uchakachuliwaji wa miradi hiyo na kujengwa chini ya kiwango,”alisema.