Na Esther Mbusi, Dodoma
Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), amehoji uhalali wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuwa wasemaji wa waisalamu nchini.
Akiomba mwongozo wa Spika bungeni leo Jumatatu Februari 5, Bobali alisema Waislamu wana madhehebu mengi lakini taasisi pekee ndiyo inayosikilizwa na serikali ni Bakwata.
“Madhehebu mengine hayatambuliwi na hata ushiriki wa viongozi wakubwa wa kitaifa hushiriki Bakwata, hivi Bakwata ndiyo taasisi pekee iliyopewa mamlaka na serikali ya kuwasemea waislamu wa nchi hii,” alihoji Bobali.
Hata hivyo, akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alisema mwongozo huo umekosa sifa kwa mujibu wa kanuni ambapo zinamtaka muomba mwongozo kuzingatia jambo lililotokea bungeni na suala la Bakwata halijazungumzwa bungeni.