26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe: Taratibu zikikiukwa tutakataa matokeo

DSC_4901SHABANI MATUTU NA MAULI MUYENJWA, DAR ES SALAAM

MWENYEKITI mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe, amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hakitakubali matokeo ya uchaguzi mkuu kama kutakuwa na ukiukwaji wa taratibu.

Alitoa msimamo huo jana jijini Dar es Salaam wakati wa shughuli ya kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti

mwenza wa Ukawa, Dk. Emmanuel Makaidi, aliyefariki dunia mwanzoni mwa wiki mkoani Lindi.

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, alisema hayo alipokuwa akijibu swali la mwandishi wa habari aliyetaka kujua msimamo wa Chadema kuhusu matokeo ya urais baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

“Kabla ya kukubali matokeo, tutachunguza namna mchakato mzima ulivyoendeshwa, na kama itabainika haukuwa huru, haki na wazi, tukisema tutakubali, tutakuwa tunajidanganya,” alisema Mbowe.

Pamoja na hayo, alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanalinda kura zao kwa kukaa nje ya kituo umbali wa mita 200 kwa sababu sheria inaruhusu kufanya hivyo.

MBATIA

Akimwelezea Dk. Makaidi, Mwenyekiti mwenza mwingine wa Ukawa, JamesMbatia, alisema alikuwa mstari wa mbele katika kuleta mageuzi na mabadiliko pasipo kuyumbishwa na mtu wala kujali udogo wa chama chake
cha NLD.

“Lilipofikia suala la kuunganisha Ukawa kwenye Bunge Maalum la Katiba, Dk. Makaidi alikuwa mtu wa kwanza kuunga mkono juhudi hizo, ikiwa ni pamoja na kuchangia kiasi kikubwa cha fedha wakati chama chake kikiwa hakina ruzuku.

“Hata baada ya Ukawa kuamua kutoka nje ya Bunge Maalumu la Katiba Aprili 16 mwaka jana, Dk. Makaidi
aliungana na wajumbe wengine kuacha posho ya shilingi 300,000 kwa siku bila kujali kama chama chake
hakina ruzuku.

“Kwahiyo, huyu alikuwa ni mpenda mageuzi wa kweli, alikuwa na msimamo usioyumba na alikuwa akijiamini zaidi,” alisema Mbatia.

Akiwazungumzia wanasiasa wanaotumia muda wao kuwatakia wenzao vifo, aliwataka kutofanya hivyo kwa sababu kila mmoja ni mpitaji duniani.

“Leo wanasiasa wamekuwa wakiwaombea wenzao vifo kwenye majukwaa, wakisahau kwamba hapa duniani tunapita. Sote tunatakiwa kujua kwamba kila mmoja anatakiwa kumwombea mwenzake mambo mema,
tusiombeane mabaya,” alishauri Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi.

Akizungumzia kuhusu uvumilivu, alisema kipimo chake ni mgombea urais wa Ukawa, ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye pamoja na kutukanwa kuliko mwingine yeyote, hajamjibu mtu.

“Lowassa ndiye aliyetuagiza tumzike Dk. Makaidi kwa heshima anayostahili, na uamuzi huo umechangia kutukutanisha viongozi wote wakubwa wa Ukawa.

“Kutokana na jinsi tulivyokuwa tukimheshimu Dk. Makaidi na kutokana na jinsi tunavyoheshimiana, tulikubaliana kusimamisha shughuli za kampeni kwa muda wa saa 24,” alisema.

JAJI MUTUNGI

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji mstaafu, Francis Mutungi, alimwelezea Dk. Makaidi kama mwanasiasa aliyefanikiwa kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwamo Mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Vyama
vya Siasa lililoanzishwa mwaka 2009.

“Dk. Makaidi amesaidia kuleta mabadiliko ya siasa, hivyo tumuenzi kwa kufanya uchaguzi wa amani,” alisema
Jaji Mutungi.

PETER MZIRAY

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, Peter Mziray, alimlilia Dk. Makaidi na kusema amefariki wakati busara zake zikiwa bado zinahitajika katika uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kuwa mgumu.

MAKAMU MWENYEKITI NLD

Naye Makamu Mwenyekiti wa NLD, Mfaume Khamis, alisema itakuwa vigumu kwa chama hicho kupata kiongozi aliyekuwa akijitolea kama alivyokuwa akifanya Dk. Makaidi.

MAKABURINI

Marehemu Dk. Makaidi, alizikwa jana katika makaburi ya Sinza, Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, akiwamo mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Lowassa.

Baada ya shughuli za maziko kukamilika, wanafamilia na waombolezaji walirudi nyumbani kwa marehemu maeneo ya Sinza Madukani. Wakati huo huo, wafuasi wa Ukawa waliohudhuria mazishi hayo, walishindwa kuvumilia na kuanza kumshangilia Lowassa wakimuita rais.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles