– Kutumia siku tatu ndani ya majimbo 9
NA BAKARI KIMWANGA, GEITA
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, leo ataanza mikutano ya kampeni jijini Dar es Salaam.
Dk. Magufuli atawasili jijini humo baada ya kukamilisha mikutano ya kampeni ya kuomba kuchaguliwa katika nafasi hiyo kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Akiwa jijini Dar es Salaam, atafanya mikutano katika majimbo yote ambayo alikuwa hajahutubia, huku akiwanadi
wagombea ubunge wa majimbo hayo.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), katika siku tatu jijini humo, Dk. Magufuli atafanya
mikutano katika majimbo ya Kigamboni, Mbagala, Temeke, Ilala, Segerea, Ubungo, Kibamba, Kinondoni na Kawe.
Mgombea urais huyo ambaye alizindua kampeni zake Agosti 23, mwaka huu katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, anatarajia kufungia jijini Mwanza Oktoba 24.
Katika mikutano yake, mgombea huyo mara kadhaa amekuwa akieleza mikakati yake kama atachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni kupambana na rushwa na ufisadi kwa kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kero hizo. Pamoja na hayo, amekuwa pia akifafanua nia ya mabadiliko ya kweli ya Serikali yake, huku akipinga suala la mabadiliko kwa kukiondoa chama tawala madarakani.
FAMILIA NA URAIS WAKE
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geita, jana, baba mdogo wa Dk. Magufuli, Albert Marco (70), alisema familia yao inaona faraja kwa mtoto wao kuweza kuaminiwa na Watanzania.
Alisema nyota ya mgombea huyo wa CCM, ilionekana tangu akiwa mtoto kwani alipokuwa shule aliaminiwa na wanafunzi wenzake na kuchaguliwa kuwa kiongozi wa darasa.
“John (Magufuli), ni mtoto wa kaka yangu mkubwa ambaye alikuwa wa tatu kuzaliwa kwa baba yetu. Malezi ya kaka
yalikuwa mema na sasa kila Mtanzania anamjua John. “Ni kijana mwenye msimamo sana wakati wote, hata sisi katika familia huwa tunajisikia faraja sana kwa michango yake mizuri.
“Leo amefika hapa kwa kuaminiwa na CCM, na sisi tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe nguvu katika
jukumu zito atakalokabidhiwa na Watanzania Oktoba 25,” alisema Albert.
Albert ambaye ndiye kiongozi wa familia ya Magufuli, alisema familia yao ni ya kawaida licha ya baadhi ya watoto wao kushika nafasi mbalimbali serikalini.
“Maisha yetu ni ya kawaida kama mnavyomuona John, ni mtu wa kawaida hana majivuno na suala la uaminifu kwake si la ukubwani ni tangu utotoni.
“Ukimtuma anatumika, siyo jeuri na ni mtu ambaye wakati wote ana heshima kwa wakubwa na wadogo, anajua wajibu wake katika familia na hata kazini.
“Alipokuwa shule, John muda wote alikuwa ni mtu wa kupenda kusoma na kushirikiana na wanafunzi wenzake,
ninamwombea Mungu amjalie kijana wetu,” alisema.
Wakati huo huo, Dk. Magufuli alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Busorwa, Wilaya ya NyanghwaleNmkoani Geita, alitaka uongozi wa wilaya hiyo, uache mpango wa kukopa Sh milioni 700 kutoka Benki ya CRDB ili kuwalipa fidia wananchi wanaotakiwa kupisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya wilaya hiyo.
Dk. Magufuli, alisema mpango huo haufai kwa sababu utawaumiza wananchi.
“Ni sawa kuwafidia wananchi, lakini baada ya muda, halmashauri itachukua muda mrefu kulipa deni na kusababisha
baadhi ya huduma kusimama.
“Hivyo nitaiagiza Mamlaka ya Ujenzi wa Nyumba za Serikali iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi ninayoiongoza, wafike hapa ili kuanza kufanya utaratibu wa kuratibu eneo la ujenzi,” alisema. Dk. Magufuli alisema ili mpango huo ukamilike, aliwataka wananchi hao wamchague kuwa rais wa awamu ya tano, aweze kutafuta fedha za kuwalipa fidia
haraka.
Akiwa Sengerema, Dk. Magufuli aliwaambia wananchi katika viwanja vya Mnadani kuwa wakimchagua atakamilisha mradi wa maji ulioanza kutekelezwa na Serikali wilayani humo.
Pia, alisema atajenga barabara ya kutoka Buyagu kupitia Kijiji cha Ngoma hadi Busorwa yenye urefu wa kilomita 35.
“Hata barabara ya kutoka Sengerema kuelekea Nyehunge hadi Buchosa yenye urefu wa kilomita 65 hadi Nkome Geita, itajengwa kwa kiwango cha lami.
“Nitateua pia timu ya wataalamu wa kuandaa mchoro wa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujenga daraja la kisasa katika Kivuko cha Busisi na Kigongo ili vivuko vilivyopo vitumiwe kuvusha wananchi katika maeneo mengine,” alisema.
Awali, mgombea ubunge Jimbo la Sengerema, William Ngeleja (CCM), alimwomba Dk. Magufuli atekeleze ujenzi
wa barabara ya Kamanga hadi Katunguru kwa kiwango cha lami kama inavyoelekezwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM.