26 C
Dar es Salaam
Friday, November 29, 2024

Contact us: [email protected]

MBOWE, MDEE WAFICHUA WALICHOHOJIWA KWA SAA MBILI

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (kushoto), akihojiwa
mbele ya ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa amri ya Spika Job Ndugai ya
kumtaka afike mbele ya kamati hiyo kujibu tuhuma zinazomkabili za kuingilia haki, uhuru na
madaraka ya Bunge kutokana na matamshi yasiyo na staha mapema wiki hii bungeni Dodoma.

Na Waandishi Wetu – Dodoma

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), jana wamehojiwa na Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa muda wa saa mbili – saa moja kila mmoja.

Wamehojiwa na kamati hiyo baada ya saa 48 tangu Spika wa Bunge, Job Ndugai, atoe agizo la kumtaka Mdee afike bungeni ndani ya saa 24 vinginevyo akamatwe na polisi.

Kuhojiwa kwa wanasiasa hao, kulithibitishwa na Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya.

Hata hivyo, Owen alisema hawezi kuzungumza yaliyojiri ndani ya kikao hicho kwa kuwa hakuingia.

Kwa upande wake, Mbowe alipohojiwa na MTANZANIA Jumapili jana, alisema kamati hiyo ilimuhoji juu ya kauli nne alizotoa usiku wa Jumanne ya wiki hii mbele ya waandishi wa habari, baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), ambao wagombea wawili wa Chadema, Lawrence Masha na Ezekia Wenje, walipigiwa kura za hapana.

Mbowe alisema kauli hizo ni pamoja na aliyosema Ndugai amevunja kanuni na sheria hazikufuatwa katika uchaguzi huo, mchakato wa uchaguzi huo ulikuwa ni mkakati wa Serikali na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikuwa anajua, wagombea Chadema walikuwa wazuri lakini kupigwa kura ya hapana ilikuwa ni mkakati wa CCM na ya nne uchaguzi ulikuwa batili.

 “Walinihoji kwamba Aprili 4, mwaka huu baada ya kufanyika uchaguzi wa EALA, nikiwa nje ya ukumbi wa Bunge nilidhalilisha mamlaka ya Spika na Bunge.

“Sasa katika maelekezo yangu niliwaambia kwamba kauli hizo nilizitoa baada ya mabishano marefu mle ndani (ndani ya ukumbi wa Bunge) na kwamba mimi ni kiongozi, lakini leo (jana) sijajua kwanini wagombea wetu walikataliwa. Je, hawana elimu au hawajui Kiingereza?

“Niliwaambia sikudharau Bunge wala kiti cha Spika, mimi ni mbunge wa muda mrefu, ninajua utaratibu wa Bunge. Nikawaambia kauli yangu haikulenga mtu binafsi bali nililalamikia uchaguzi, lakini wanadhani nilimlenga mtu binafsi, nimeomba radhi, lakini bado msimamo wangu uko palepale,” alisema.

Naye Mdee alisema alihojiwa juu ya tuhuma zilizotolewa na Ndugai kwamba alitoa kauli za matusi bungeni na suala la pili ni kuzungumza bungeni bila kupewa ruhusa ya Spika.

“Nimehojiwa kwa mambo mawili; kwanza ni kuhusu yale aliyoyasema spika juzi, pili ni kuzungumza bila kupewa kibali na Spika. Wamemaliza kazi yao, kinachofuata ni hatua ya kupelekwa kwa Spika,” alisema.

Alhamisi wiki hii, baada ya kipindi cha maswali na majibu, Ndugai aliombwa miongozo na wabunge juu ya kauli ya Mbowe aliyoitoa kutokana na matokeo ya uchaguzi wa EALA na alinukuliwa akisema: “Naendelea kusema tena kwa mara nyingine, safari hii tuko hapa kwa muda mrefu, tuko hapa karibu miezi mitatu na kila mnachokifanya hapa tunamwona mmoja mmoja wenu. Kwa tabia zenu na mwenendo na nimeshasema na tuko tayari kuleta nidhamu ndani ya Bunge. Mnapozungumza ninyi wenzenu wanawasikiliza, wanapozungumza wenzenu kazi yenu kuzomea, kila mmoja tunampata nataka niwahakikishieni tutachukua hatua.”

Ndugai alisema hatochoka kuwaambia wabunge hao kuwa atashughulika na kila mtu anayejifanya yeye ana vurugu na kwamba anaanza na Mdee.

“Sasa naanza na Halima Mdee ambaye yeye alimtukana Spika. Watanzania wengi wamesikitishwa na jambo hili, wamenipigia simu, wameniandikia ujumbe wa message.

“Huu si utaratibu mwema, si utamaduni mwema na hii si mara ya kwanza kwa Halima na nilivumilia nikasema Mungu anisaidie,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles