23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mbowe, Kinana wakutana kwa siri Dar

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe

AZIZA MASOUD NA AGATHA CHARLES

IMEDHIHIRIKA kuwa viongozi waandamizi wa vyama vikubwa vya siasa vilivyo na uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba, wanapanga njama za kulivunja bunge hilo baada ya kushindwa kufikia maridhiano ya muundo wa serikali.

Kuvuja kwa taarifa hizi kumekuja ikiwa ni siku chache baada ya kufanyika vikao kadhaa vilivyowashirikisha viongozi wa vyama vikilenga kutafuta maridhiano ya muundo wa serikali unaopaswa kuandikwa katika Katiba mpya.

Taarifa zilizolifikia MTANZANIA Jumapili kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya vyama vya CCM, Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi, zimeeleza kuwepo kwa mikutano ya siri ya viongozi wakuu wa vyama hivyo inayojadili mwenendo wa Bunge la Katiba na hatima ya upatikanaji wa Katiba mpya.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, mwelekeo wa vikao vya viongozi hao unaonyesha mchakato wa kufanikisha upatikanaji Katiba mpya utafanywa na rais wa awamu ya tano atakayeingia madarakani kwa kutumia Katiba ya sasa ambayo itafanyiwa marekebisho.

MTANZANIA Jumapili limedokezwa kuwa vikao hivyo vinafanyika katika hali ya usiri mkubwa na kuhudhuriwa na wenyekiti watatu wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanaotajwa kuwa ni Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF, James Mbatia wa NCCR-Mageuzi na Freeman Mbowe wa Chadema huku CCM ikiwakilishwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana.

Imeelezwa kuwa ili kuweka hali ya usiri wa mazungumzo na makubaliano yatakayofikiwa katika vikao hivyo, wasaidizi wa wanasiasa hao na hata watendaji wengine wanaofanya nao kazi kwa karibu, wamezuiwa kuhudhuria.

Taarifa zilizopatikana kutoka Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, zimeeleza kuwa katika kikao cha kwanza kilichofanyikia Dodoma, Kinana aliondoka Dar es Salaam kwa ndege hadi mkoani humo Alhamisi wiki iliyopita kwa ajili ya kiwafuata Mbowe, Lipumba na Mbatia.

Kwamba katika kikao hicho cha kwanza, ajenda mama ilikuwa kupata suluhu ya kutatua mgogoro wa kikatiba unaoendelea baina ya vyama.

Taarifa zinadai, makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na Kinana kwenda kuongea na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta ili kumtaka asitishe shughuli za bunge hilo mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.

Makubaliano mengine ni kuitaka serikali ipeleke muswada wa marekebisho madogo ya Katiba ya Jamhuri katika mkutano wa bunge unaotarajiwa kuketi mwezi Novemba yatakayohusu Katiba kumtambua mgombea binafsi, kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi na kuanzishwa kwa mahakama ya juu (supreme court) itayosikiliza mashauri ya kupinga matokeo ya urais mahakamani.

Muswada huo ambao utaandaliwa na tume ya Makatibu wakuu wa vyama vya siasa na kuwekwa katika lugha ya kisheria na utaratibu wa kiserikali pia utaeleza umuhimu wa ajenda ya Katiba Mpya kujadiliwa baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Novemba 2015.

Alipotafutwa Kinana kupitia simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia kuwepo kwa vikao hivyo alilitaka gazeti hili kuzungumza na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliyeeleza kuwa ndiye mzungumzaji w mambo yote yanayohusiana na Ukawa.

“Mpigie Nape, tafuta ufafanuzi kutoka kwa Nape wa majibu yeyote unayoyataka,” alisema Kinana.

Naye Mbatia alipopigiwa simu alisema ameshitushwa na taarifa za kuwa mmoja wa wajumbe kwenye kikao hicho na kudai kuwa si za kweli.

“Sio kweli kwamba mimi nilishiriki kikao wala sijasikia kikao chochote, ndio kwanza nakusikia wewe,” alisema Mbatia.

Gazeti hili lilipomtafuta pia Profesa Lipumba lakini simu yake ya kiganjani iliita bila majibu na hata alipotumiwa ujembe mfupi wa maneno hakujibu.

Hata hivyo, hoja za kuvunjwa kwa Bunge la Katiba hivi karibuni zilionekana kupata nguvu kutokana na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na ile ya Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) katika kikao na Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti wa Halmashauri za Miji na Wilaya nchini mjini Tanga waliokaririwa wakisema akisema uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kutegemea hatma ya mchakato wa Katiba mpya.

Kwa upande mwingine, ALAT mbali na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika mwezi Oktoba, pia Aprili mwaka huu ilitoa tamko kuwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vinavyoendelea mjini Dodoma ni batili.

ALAT ilisisitiza kuwa vikao hivyo ni batili kutokana na kuwatenga wawakilishi wa wananchi wengi ambao ni jumuiya hiyo.

Uamuzi huo wa ALAT kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika kama ulivyopangwa mwezi Oktoba, unaipa nguvu hoja ya kuvunjwa kwa Bunge la Katiba ili kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano kuketi kwa ajili ya marekebisho ya sheria za uchaguzi.

Kwa mujibu wa mwenendo wa taratibu za uchaguzi, maboresho yanayofanywa na Tume ya Uchaguzi katika daftari la kudumu la wapiga kura, yanatoa hitaji la kufanyika kwa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi.

Kutoka na kuwepo kwa hitaji hilo la kisheria, Bunge la Jamhuri litalazimika kuketi ili kufanya marekebisho ya sheria hiyo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa, Oktoba, mwaka huu.

Mabingwa wa shughuli za kibunge wanaeleza kuwa Bunge la Jamhuri litakapoketi litalazimisha kusitishwa kwa shughuli za Bunge Maalumu la Katiba na ikiwa kinyume chake, uchaguzi wa Serikali za Mitaa hautafanyika kama ulivyopangwa.

Katika mwelekeo wa kukazia hoja ya kuvunjika kwa Bunge hilo, mapendekezo yaliyotolewa katika kikao kinachodaiwa kukaliwa na viongozi wakuu wa vyama vya siasa vikubwa nchini, pia yametolewa na chama cha ACT-Tanzania ambacho kimetaka Bunge hilo kuvunjwa.

Akizungumza jana katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Hoteli ya JB Belmont jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa ACT, Samson Mwigamba, alisema  moja ya mapendekezo yao ni kuona Tume ya Uchaguzi inakuwa huru na ionekane wazi.

Mwigamba pia alisema Katiba ya sasa inapaswa kuruhusu mgombea binafsi na wabunge ‘kukatisha kapeti’ (kuhama chama kimoja na kwenda kingine bila kupoteza ubunge) kwa madai ya kudhibiti ubabe wa vyama vya siasa.

“Pia kushusha umri wa mgombea urais ili kuwapa vijana haki na fursa ya kugombea katika nafasi hii muhimu, hasa ukizingatia kwamba karibu theluthi mbili (65%) ya wapiga kura wote Tanzania wapo chini ya umri wa miaka 40, na ukweli kwamba takwimu za Tume ya Marekebisho ya Katiba zinaonyesha kuwa wananchi walio wengi (53.7%) waliotoa maoni kuhusu umri wa mgombea urais, walitaka umri huo ushushwe,” alisema Mwigamba.

Alisema ATC inapendekeza pia kuwepo kwa masharti kwamba ili mgombea atangazwe kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, lazima apate angalau asilimia 50 ya kura zilizo halali.

Na kwamba kuwe na msingi wa kikatiba kuwa wagombea hao wa urais wafanye midahalo takribani mitatu katika kipindi cha kampeni.

“Kuondoa suala la mafuta na gesi katika mambo ya Muungano ili kuruhusu Zanzibar kuendelea na utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa uhuru na bila kuingiliwa na Tanzania bara, huku ikiruhusiwa kuwa na ushirikiano wa kimataifa  kwa faida za maendeleo yake,” alisema.

Mbali na masuala hayo ya Zanzibar, Mwigamba alisema kuwe na mipaka ya mashitaka ya kesi za rushwa ili kuruhusu TAKUKURU kufanya uchunguzi na kuendesha kesi, hususani zinazohusu ufisadi wa mali za umma pasipo kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka.

Sambamba na hilo, alisema kuwepo na msingi wa kisheria wa tangazo la mali na madeni ya viongozi kuwa wazi kwa umma, na uthibitisho wa uhalali wa mali ambazo mtu anamiliki uwe upande wa mtuhumiwa.

Pia alitaka marekebisho hayo kuweka misingi ya kikatiba kwa uhuru wa kupata habari kwa wananchi na kupiga marufuku vyombo vya habari kufungiwa isipokuwa kwa amri ya mahakama.

Mbali na hayo, lakini pia hoja ya theluthi mbili bado haifikiwi katika Bunge hilo la Katiba linaloendelea na vikao vyake Dodoma.

Hofu ya kupatikana kwa theluthi mbili iliibuliwa pia na mjumbe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.

Mwigulu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,  aliungwa mkono na baadhi ya wabunge wa CCM alipotaka Bunge Maalumu la Katiba lijitathmini kama lina ulazima wa kuendelea wakati hakuna uhakika wa kupatikana kwa theluthi mbili.

Hali hiyo ya kukosekana kwa theluthi mbili, ilijitokeza pia hivi karibuni wakati wa Bunge hili kwa kamati namba mbili inayoongozwa na  Shamsi Vuai Nahodha kukosa idadi hiyo katika ibara 19 na 22 zinazohusu maadili na miiko ya uongozi na utumishi wa umma.

Na kwamba ili theluthi mbili ipatikane katika Bunge hilo, wanahitajika wajumbe 16 kutoka upande wa Zanzibar.

Viongozi wa juu wa  Ukawa pamoja na wale wa CCM  walishakutana zaidi ya mara mbili wakiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa lengo la kutafuta maridhiano bila mafanikio.

Katika vikao walivyofanya na Jaji Mutungi ambavyo havikuzaa matunda, cha mwisho kilifanyika Agosti mosi katika Hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao pia waliwahi kuitwa  na wajumbe wa Kamati ya Maridhiano ya Bunge Maalumu la Katiba, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta jijini Dar es Salaam, lakini wajumbe wa Ukawa waligoma kufika katika mkutano huo.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuikutanisha kamati hiyo pamoja na wajumbe hao kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mvutano uliotokea katika Bunge hilo lililopita ambapo Ukawa walitoka nje.

Kamati hiyo iliyoteuliwa na Sitta kabla ya kuanza kwa awamu ya pili ya mjadala wa Katiba Agosti 5 kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mvutano huo, ilijumuisha wajumbe kutoka vyama, taasisi na mashirika yote yaliyowakilishwa katika Bunge hilo.

Hata hivyo, katika mkutano huo, wajumbe waliohudhuria takribani wote ni viongozi, hasa mawaziri na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo walioko kwenye kamati hiyo kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na taasisi mbalimbali, huku vyama vya upinzani aliyehudhuria ni Peter Mzirai kutoka chama cha APPT-Maendeleo.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

  1. pamoja na tume huru ya uchaguzi, lakini pia muswada huo uhusishe uhuishai wa daftari la Wapiga kura na kuwa wazi,halikadhalika mfumo mzima wa usimamizi wa uchaguzi lazzima ubadilishwe kwani sasa hivi wakuu wa Wilaya na wakurugenzi ndiyo wasimamizi wakuu, na mwisho ni uthibiti wa vyombo vya ulinzi yaani polisi na usalama wa taifa wasihusike katika kusimamia uchaguzi, wao walinde usalama katika vituo. Mkirekebishe hayo basi kweli tutakuwa na uchaguzi huru na halali. TUme huru ikishawekwa ndiyo itakayoandaa uchaguzi na makando kando yake. ifike mahali sasa Tza ianze kuwa na demokrasia ya kweli na siyo kuzuga zuga na usanii halafu matokeo yake ni malalamiko kila wakati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles