27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kibonde, Gadner watiwa mbaroni

Mtangazji maarufu wa redio nchini, Ephraim Kibonde
Mtangazji maarufu wa redio nchini, Ephraim Kibonde

NA ELIZABETH HOMBO

WATANGAZAJI maarufu wa redio nchini, Ephraim Kibonde na Gadner G. Habash, wametiwa mbaroni katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, jijini Dar es Salaam baada ya kudaiwa kusababisha ajali na kukaidi amri ya askari wa usalama barabarani.

Kibonde ambaye amejizolea umaarufu kupitia kipindi cha ‘Jahazi’ kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds Fm akiwa na mtangazaji mwenzake wa Radio Times, Gadner, walikutwa na mkasa huo jana saa 12 asubuhi katika eneo la Makumbusho.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, zilieleza kuwa Kibonde ambaye alikuwa dereva wa gari hilo aligonga kwa nyuma gari lililokuwa likiendeshwa na raia wa kigeni (mzungu).

Akizungumza na gazeti hili kupitia simu yake ya kiganjani, Kamanda Wambura alisema baada ya Kibonde kusababisha ajali hiyo, alikaidi amri ya askari wa usalama barabarani iliyomtaka asimame ili wapime na badala yake aliondoa gari kwa mwendo kasi hali iliyoashiria alikuwa amekimbia.

Alisema baada ya kukaidi amri hiyo, askari aliyekuwepo eneo la tukio naye alipanda gari jingine kwa nia ya kumfukuza na kwamba alipofika eneo la Mwenge alifanikiwa kumsimamisha na kisha kupanda katika gari lake ili warudi eneo ilikotokea ajali.

Kwa mujibu wa Wambura, baada ya askari huyo kupanda kwenye gari la Kibonde, mtangazaji huyo hakurudi kwenye eneo la tukio na badala yake aliendelea kukata mitaa mingine.

“Bahati nzuri askari wetu huyo alikuwa anawasiliana na wenzake, walipofika eneo la Ubungo Mataa wakawawekea kizuizi kilichowasaidia kuwakamata.

“…Nilipata taarifa hizo za Kibonde nikiwa kwenye kikao, ni kweli alisababisha ajali majira ya saa 12 asubuhi pale Makumbusho na alimgonga Mzungu ambaye hata hivyo sikuishika namba ya gari lake,” alisema Kamanda Wambura.

Alieleza kuwa baada ya askari wa Ubungo kufanikiwa kuwakamata, waliwafikisha katika kituo cha Polisi cha Oysterbay na walibaini kuwa watangazaji hao walikuwa wamelewa.

“Walipofikishwa kituoni na kutakiwa kupimwa ulevi waligoma… kwa sababu Kibonde alikuwa hana uwezo wa kuendesha tena gari na walikuwa wanatoa lugha chafu za matusi kwa askari wetu,” alisema.

Alipoulizwa kuwa ni sheria zipi walizozivunja, Kamanda Wambura aliyataja makosa matano, ambayo ni kusababisha ajali, kutokutii amri ya askari, kukimbia na kutoroka na askari, kutoa lugha chafu za matusi na kukataa kupimwa ulevi.

Kamanda Wambura alisema kwa sasa wanaendelea na upelelezi wa tukio hilo, na baada ya kuukamilisha watapeleka jalada kwa wakili wa serikali ili watangazaji hao washitakiwe.

Akiwazungumzia watangazaji hao, Kamanda Wambura alisema kuwa wao wanawaona kama wahalifu wa makosa ya jinai na kamwe hawatawachukulia kama watu maarufu.

“Sisi hatutajali kama watangazaji hao ni watu maarufu, na kwamba mbele ya uso wa sheria hakuna umaarufu,” alisisitiza Wambura ambaye hadi tunakwenda mitamboni jana jioni alisema watangazaji hao walikuwa bado rumande.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles