31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mama Pinda: Wanawake wote tunataka amani

Mke wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mama Tunu Pinda
Mke wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mama Tunu Pinda

NA MWANDISHI WETU, SEOUL

MKE wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mama Tunu Pinda, amesema wanawake wote duniani wanalilia amani na hawapendi vita wala machafuko kwani husababisha amani kutoweka.

Mama Pinda alitoa wito huo jana wakati akitoa mada kama mzungumzaji mkuu kwenye mkutano wa dunia wa siku tano ulioanza Seoul, Korea Kusini jana.

Mkutano huo ambao umeandaliwa na Taasisi ya Universal Peace Federation (UPF) ambayo inatoa ushauri kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya uchumi na jamii, unajadili masuala ya amani, usalama na maendeleo.

Akiwasilisha mada yake kuhusu usalama, amani na maendeleo barani Afrika, Mama Tunu Pinda alisema:

“Ninaiomba jamii ya kimataifa duniani kote tusimamie amani na usalama kwani kinyume na hapo ni kuleta machafuko na vita.

“Wanawake hatupendi vita wala machafuko kwa sababu tukiruhusu machafuko, wanawake na watoto watapoteza maisha kwa wingi jambo ambalo wanawake wote duniani hatutaki litokee.”

Pamoja na hayo, aliwataka washiriki wa mkutano huo wasimame katika nafasi zao kama baba na mama, kaka na dada na wahakikishe dunia inakuwa ni mahali pazuri pa kuishi.

“Ninawasihi tuendeleze maono ya muumba wetu, tuweke utu mbele kwa kuwajali wengine na tuache kutanguliza masilahi yetu binafsi,” alisema.

Awali akiwakaribisha wajumbe zaidi ya 500 kutoka nchi 68 wanaoshiriki mkutano huo, Rais wa UPF, Dk. Thomas Walsh, alisema taasisi hiyo inasimamia misingi ya amani, usalama na maendeleo ya jamii kwa nia ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa mataifa mbalimbali.

Alisema ana tumaini uwepo wa wakuu wa nchi mbalimbali na viongozi mashuhuri katika mkutano huo, utasaidia kupata majibu ya changamoto zinazoikabili dunia juu ya upatikanaji wa amani ya kudumu.

Naye Mfalme Letsie Mswati III kutoka Lesotho, alisema dunia inakabiliwa na changamoto nyingi za ukosefu wa amani ikiwamo uharibifu wa mazingira.

Aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanahimiza utunzaji wa mazingira kama njia ya kupunguza matatizo yanayojitokeza kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Alionya kwamba kuna haja ya kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha dunia haiendelei kuwa na matukio ya ugaidi na matumizi ya silaha za maangamizi.

“Kama tutakubali vita viendelee kutokea na migogoro isiyokwisha barani Afrika na nchi za Uarabuni ni lazima tukubali kuwa hakutakuwa na maendeleo katika mabara haya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles