Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, hawezi kuongoza tena chama hicho kwa muhula mwingine hata kama uchaguzi utaitishwa sasa na kiongozi huyo akashinda.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kusema chama hicho kilikiuka katiba yake kilipobadilisha kipengele cha katiba kilichoondoa ukomo wa uongozi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema mabadiliko hayo yalitakiwa kupitishwa na mkutano mkuu.
“Suala hilo (mabadiliko) halikujadiliwa kwenye Mkutano Mkuu … itambulike kuwa marekebisho yoyote yanaweza kufanywa na mkutano mkuu peke yake.
“Kwa maana hiyo kwa sasa kiongozi yeyote wa Chadema ambaye ameongoza chama hicho kwa vipindi viwili, hawezi kugombea tena na hata akigombea na kushinda, sisi hatutamtambua na tutahesabu kama nafasi yake ipo wazi,” alisema Nyahoza.
Alisema kama chama hicho kinataka kuendelea na kipengele hicho, lazima kifanye Mkutano Mkuu ambao utajadili na kuridhia kupitishwa kifungu hicho.
Nyahoza, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, alikitaka chama hicho kuitisha mkutano mkuu kwa ajili ya kufanya uchaguzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali.
Alisema kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, kiongozi ambaye ameongoza kwa miaka 10 anapaswa kuachia madaraka na kupisha wengine.
Mpaka sasa, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ameongoza kwa vipindi viwili, hivyo anapaswa kutoka na nafasi yake ichukuliwe na mtu mwingine.
“Kama kuna kiongozi ambaye amekaa kwa vipindi viwili anapaswa kuachia madaraka na kupisha wengine waweze kuongoza chama hicho,”alisema Nyahoza.
Msajili huyo Msaidizi, alisisitiza haja ya Chadema kuitisha Mkutano Mkuu uchague viongozi wengine jambo linalotakiwa kutekelezwa ifikapo Januari mwakani.
Alisema kama viongozi hao watashindwa kufanya hivyo, ofisi yake itachukua hatua ikiwa ni pamoja na kuwaandikia barua ya kutoutambua uongozi utakaokuwa madarakani.
Chama hicho kinapaswa kufuata utaratibu kiliojiwekea katika katiba kiweze kuongozwa kwa njia ya demokrasia, alisema.
Alisema mwishoni mwa mwaka jana, ofisi hiyo ilipata barua kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na wenzake, wakidai kuwa uongozi wa chama hicho ulibadilisha kinyemela kipengele cha katiba kilichohusu ukomo wa uongozi.
Baada ya kupata barua hiyo ofisi hiyo ilikiandikia barua Chadema kuhoji suala hilo na kukitaka kiwasilishe katiba yake iweze kupitiwa na kuangaliwa kipengele hicho, alisema.
Alisema baada ya kusoma katiba hiyo, ofisi ya msajili ilibaini kuwa ilikuwa ikionyesha kwamba ukomo wa uongozi ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano.
“Baada ya Mwigamba na wenzake kuwasilisha barua ya malalamiko kuhusu kubadilishwa kinyemela kipengele cha ukomo wa uongozi, tulilazimika kuwaandikia barua ya kutaka kuthibitisha hilo na wakatuletea katiba yao.
Tuliisoma na kujiridhisha, lakini pia tumewataka kuitisha mkutano mkuu wa chama hicho waweze kufanya uchaguzi kwa kufuata katiba ya chama chao,”alisema.
Alisema ofisi ya msajili inafanya kazi kwa kufuata sheria za vyama vya siasa nchini, hivyo kila chama kinapaswa kuendesha shughuli zake kwa kufuata katiba yake ili kuendeleza demokrasia ndani ya vyama.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, toleo la 2006, kifungu cha 6.3.2 (C) kinachohusu muda wa uongozi, kinasema, “(c) Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi.”
Lakini pia Katiba ya Chadema ya mwaka 2004 kipengele 5.3.2 (c) kinasema, “Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi kwa muda usiozidi vipindi viwili katika cheo kimoja kwa ngazi moja.”
Hata hivyo Msajili anasema: “Sisi katiba ya Chema tuliyonayo ni ya mwaka 2006 ambayo inaonyesha ukomo wa uongozi ni vipindi viwili.”
Alisema baada ya Mwigamba kuwasilisha barua ya malalamiko kuhusu kipengele hicho cha katiba, ofisi yake ilifanya uchunguzi na kubaini kuwa hakuna mkutano wa chama hicho uliobariki kuondolewa kipengele hicho cha ukomo wa uongozi.
Mbowe alipotafutwa na Mtanzania kuzungumzia suala hilo alijibu kwa kifupi kuwa, “tutatoa taarifa rasmi juu ya suala hilo”.
Oktoba 29, mwaka 2013 Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alilipokuwa akitoa ufafanuzi wa kuvuliwa uongozi kwa waliokuwa wanachama wa chama hicho, Samson Mwigamba na Dk. Kitila Mkumbo, alisema madai ya kwamba wakati mabadiliko ya katiba ya mwaka 2006 yakifanywa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka 10 kiliondolewa kinyemela, siyo kweli.
Alisema hayakufanyika marekebisho ya Katiba bali kilichofanyika ni kuandikwa upya Katiba ya chama kutoka ile ya mwaka 2004.
“Kwa ninavyokumbuka hicho kinachoitwa ‘kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano’ hakijawahi kuingizwa kwenye katiba mpya ya Chadema.
“Baada ya timu zote kufanya kazi yake; rasimu ya katiba ilipita katika vikao vyote vya katiba yaani sekretariati, kamati kuu, baraza kuu na hatimaye mkutano mkuu.
“Katika vikao vyote hivyo, iwapo kipengele hicho kingekuwa kimeondolewa ‘kinyemela’ kama inavyodaiwa, mwandishi wa tuhuma hiyo angehoji kutoka Agosti 2006,” alisema Makene.