Na TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeahirisha kwa mara ya pili maandamano na mikutano ya hadhara iliyopangwa kufanyika leo nchi nzima kupitia operesheni iliyopewa jina la Umoja wa Kupambana na Udikteta nchini (Ukuta) hadi hapo tarehe itakapopangwa baadaye.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya chama hicho imeamua kufanya kila jambo kwa tahadhari kubwa ili kuhakikisha usalama wa viongozi, wanachama na wananchi.
Badala yake alisema kufuatia kuondolewa kwa zuio la mikutano ya ndani ya vyama vya siasa, kamati hiyo itafanya ziara katika kanda na mikoa ya kichama ili kuendeleza harakati za Ukuta na kujenga na kuimarisha uhai wa chama hicho.
“Kamati maalumu ya Kamati Kuu inatangaza kuwa maandamano na mikutano iliyopangwa kuanza kesho (leo) sasa yatafanyika siku na tarehe itakayopangwa baadaye kwa kuzingatia hali halisi ya kisiasa itakavyokuwa nchini,” alisema Mbowe.
Alisema chama hicho kimebuni mbinu mbalimbali za kuendeleza Ukuta kwa njia za kidiplomasia ikiwa ni pamoja na ziara za nje ya nchi ambako watazieleza nchi na taasisi za kimataifa ili kujenga shinikizo la kidiplomasia katika mapambano ya kudai haki na demokrasia duniani.
“Kamati maalumu ya Kamati kuu imeelezwa kwamba, ziara iliyoongozwa na Katibu mkuu wa chama, Dk. Vincent Mashinji katika nchi za shirikisho la Ujerumani na Denmark imekuwa na mafanikio hivyo chama kimepanga kufanya ziara za aina hiyo katika nchi marafiki wa Tanzania kama Ulaya, Scandinavia, Uingereza, Marekani na Canada,” alisema Mbowe.
Alisema mbinu nyingine ni kufungua mashauri mahakamani kupinga hatua za kukandamiza demokrasia na haki za binadamu na ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.
ATANGAZA KUMTENGA LIPUMBA
Mbowe pia alizungumzia mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF) akisema Kamati Kuu ya Chadema inalaani vikali uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa kukivuruga chama hicho kwa kujaribu kumrudisha aliyekuwa Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahimu Lipumba.
“Kamati inavielekeza vyombo vyote vya chama, viongozi wa ngazi zote wanachama na wafuasi wa chama chetu wapenda demokrasia nchini kumwangalia Profesa Lipumba kama msaliti wa kudai haki na kutokumpa ushirikiano wa aina yoyote yeye pamoja na wafuasi wake,” alisema Mbowe.
Alisema wanamtangaza Jaji Mutungi kama adui wa demokrasia ya vyama vingi nchini na kuvielekeza vyombo vyote vya chama hicho kutompa ushirikiano wowote isipokuwa ule tu unaolazimishwa na matakwa ya sheria ya vyama vya siasa.
AKOSOA TWAWEZA
Mbowe pia alikosoa vikali tafiti za Twaweza akidai kuwa zimekuwa zikijaribu kufunika aibu na balaa linaloikabili nchi kufuatia hatua mbalimbali za Rais John Magufuli.
“Mifumo ya kikatiba na sheria ya uendeshaji wa nchi na Serikali imevurugwa kwa kiasi kikubwa ambapo nchi sasa inaendeshwa kwa kauli, amri na vitisho vya mtu mmoja… kwa mazingira haya ni wazi Rais anahitaji wapiga zumari kama Twaweza ili kumpamba na kumpendezesha,” alisema Mbowe.