25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mbio urais CCM

Khamis Mkotya na Debora Sanja, Dodoma

HATIMAYE mbio za urais, ubunge, udiwani na uwakilishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza rasmi, baada ya chama hicho kutangaza ratiba ya kuchukua na kurejesha fomu.
Ratiba hiyo inaonyesha fomu za wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zitaanza kutolewa Juni 3 na kurejeshwa Julai 2, mwaka huu, saa kumi jioni.
Kuhusu nafasi ya ubunge, udiwani na uwakilishi, wagombea wa nafasi hiyo wanatakiwa kuchukua fomu kuanzia Julai 15 hadi 19, mwaka huu.
Wagombea wataanza kufanya kampeni Julai 20 hadi 31, mwaka huu na kura ya maoni itafanyika Agosti mosi, mwaka huu, ambapo wanachama wote wa CCM watapiga kura kuchagua wagombea hao.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye, alisema ratiba hiyo imekamilika baada ya kujadiliwa na kupitishwa na Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC).
Kuhusu gharama za fomu, Nape alisema fomu ya urais itauzwa Sh milioni 1, ubunge 100,000, wakati kwa nafasi ya udiwani fomu itauzwa Sh 50,000.

Urais
Kwa nafasi ya urais, Nape alisema kuanzia Juni 3 na Julai 2, wagombea watapata muda wa kuzunguka mikoani kwa ajili ya kutafuta wadhamini.
Alisema utaratibu wa mwaka huu wagombea urais wanatakiwa kutafuta wadhamini 450 katika mikoa 15, tofauti na uchaguzi wa mwaka 2010 nyuma, ambapo wadhamini walikuwa 250.
Alisema ongezeko la wadhamini limetokana na ongezeko la mikoa na wanachama wa CCM.
“Tumesema kati ya mikoa hiyo, walau mikoa mitatu iwe ni Zanzibar na kati ya hiyo, mitatu angalau mkoa mmoja Unguja na mmoja Pemba.
“Katika uchaguzi wa mwaka 2005 na 2010, mgombea urais alitakiwa kutafuta wadhamini kutoka mikoa 10, kati ya hiyo angalau mikoa miwili itoke Zanzibar,” alisema.

Masharti

Nape alisema wagombea urais hawatakiwi kudhaminiwa na mjumbe yeyote wa Mkutano Mkuu wa CCM, mjumbe wa NEC, Kamati Kuu (CC) wala wenyeviti wa CCM wa mikoa na wilaya.
Alisema hali hiyo inatokana na kwamba wajumbe hao ndio watakaoshiriki mchakato wa uteuzi wa kumpata mgombea huyo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Alisema wagombea hao watalazimika kudhaminiwa na wanachama wa kawaida, ambapo mwanachama haruhusiwi kumdhamini mgombea urais zaidi ya mmoja ambaye atakuwa amethibitishwa na katibu wa wilaya kwamba ni mwanachama.
Kwa mujibu wa Nape, vikao vya mchujo wa nafasi hiyo vitaanza Julai 8, ambapo Kamati ya Usalama na Maadili itakutana.
“Julai 9, mwaka huu Kamati Kuu (CC) itakutana na Julai 10, Halmashauri Kuu itakutana kwa ajili ya mchujo wa nafasi hiyo, ambayo pia itampitisha mgombea wa urais wa Zanzibar,” alisema.

Zanzibar

Kwa upande wa Zanzibar, mgombea urais muda wa kuchukua fomu ni Juni 3 hadi Julai 2, mwaka huu na kwamba katika kipindi hicho, mgombea atatakiwa kutafuta wadhamini.
“Kwa upande wa mgombea wa Zanzibar, atatakiwa kutafuta wadhamini 250 kutoka mikoa mitatu, kati ya hiyo angalau mkoa mmoja utoke Unguja na mkoa mmoja kutoka Pemba,” alisema Nape.
Alisema vikao vya mchujo kwa mgombea urais wa Zanzibar vitaanza Julai 4 mwaka huu, ambapo Kamati ya Usalama na Maadili ya Zanzibar itakutana.
“Kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Zanzibar itakutana Julai 5, mwaka huu, Julai 8, mwaka huu itakutana Kamati ya Usalama na Maadili ya Taifa na Julai 9 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa itakutana.
“Julai 10, mwaka huu NEC itakutana ambapo kikao hicho ndicho cha mwisho kitakachompata mgombea urais wa Zanzibar. Mkutano mkuu utafanyika Julai 11 na 12 kwa ajili ya kuchagua mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Ubunge

Kuhusu nafasi ya ubunge, udiwani na uwakilishi, Nape alisema baada ya fomu kurejeshwa Julai 19, kampeni katika matawi kwa ajili ya kuomba kura zitaanza Julai 20 hadi 31, mwaka huu, wakati siku ya kupiga kura za maoni nchi nzima, itakuwa Agosti mosi, mwaka huu.
Nape alisema baada ya hapo vikao vya mchujo vitafuata. “Kwa nafasi za uwakilishi na ubunge wa viti maalumu, ratiba ni ile ile kama ya ubunge na udiwani.
“Bara kutakuwa na masanduku mawili, ubunge na udiwani, wakati upande wa Zanzibar kutakuwa na masanduku matatu, ambayo ni ubunge, uwakilishi na usheha,” alisema.
Viti maalumu ubunge
Alisema katika mchakato wa kuwapata wagombea wa viti maalumu katika makundi yote utaratibu ni ule ule, isipokuwa kwa kundi la vijana, kura za mwisho zitapigwa katika mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Umoja wa Wanawake (UWT), tofauti na uchaguzi uliopita ambapo walipigiwa na Jumuiya ya Vijana (UVCCM).
Hata hivyo, Nape alisema chama hicho kimefanya maboresho, kwani mbali na makundi mengine maalumu, safari hii Jumuiya ya Wazazi itakuwa na viti viwili.
Kura ya maoni

Akizungumzia mchakato wa kura za maoni, alisema CCM imeweka mfumo wa udhibiti wanachama feki ili kuzuia matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2010.
Alisema wanachama watakaokwenda kupiga kura za maoni watatakiwa kuwa na kadi mbili, ambazo ni kadi ya CCM na kadi ya kupigia kura ili kudhibiti wanachama feki.
Kuhusu daftari la wanachama, Nape alisema NEC imepitisha pendekezo kwamba Julai 15, mwaka huu, itakuwa ukomo wa kuingiza wanachama wapya na baada ya hapo daftari litafungwa.
Aliwataka wagombea wote, wakiwemo wa urais kufuata kanuni za chama katika mchakato huo.
“Hatutaki sherehe wala mbwembwe wakati wa kuchukua na kurudisha fomu wala wakati wa kwenda kutafuta wadhamini, wagombea wasome kanuni na wazifuate, kosa moja goli moja,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles