22.1 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

Hotuba ya JK yawakuna wajumbe NEC

Na Khamis Mkotya, Dodoma

BAADHI ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), wameelezea kufurahishwa na hotuba iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete.
Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu mjini hapa juzi, Rais Kikwete alisema salama ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu, ni kuteua wagombea wazuri wanaokubalika kwa wananchi.
Rais Kikwete aliwaagiza viongozi wa chama hicho kuzingatia sifa na vigezo na mwisho wa siku kuteua wagombea wazuri katika ngazi zote za urais, ubunge na udiwani ili chama hicho kiweze kushinda bila jasho.
Wakizungumza na MTANZANIA nje ya ukumbi wa jengo la makao makuu ya chama hicho (White House), wajumbe hao walisema hotuba ya Rais Kikwete imetoa dira kwa chama hicho kuelekea katika uchaguzi.
Wajumbe hao walisema, hotuba ya Rais Kikwete imesimama katika uhalisia na kwamba hakuonesha mwelekeo iwapo ana mgombea wake.
Mjumbe wa Wilaya ya Musoma, Vedastus Mathayo, alisema hotuba hiyo imetoa mwelekeo kwa chama hicho na njia madhubuti kuelekea katika uchaguzi.
“Nimefurahishwa na hotuba yake, hasa pale aliposema chama kiteue mtu anayekubalika na wananchi. Tuchague mtu anayetakiwa na watu si tunayemtaka sisi viongozi.
“Utaratibu wa kuteua mtu asiyekuwa na uwezo wa kutosheleza kiu ya wananchi halafu anabebwa na chama sasa no (hapana).
“Tunahitaji ateuliwe mtu aggressive (makini) atakayekibeba chama na kukiletea ushindi, si chama kimbebe mtu, zama hizo hivi sasa hazipo,” alisema.
Balozi Karume

Mjumbe wa NEC kutoka Zanzibar, Balozi Alli Karume, alisema amefurahishwa na hotuba hiyo, kwani Rais ameonesha ukomavu wake katika medani ya siasa ndani ya chama hicho.

Balozi Karume alisema hotuba ya Rais Kikwete itatumika kukivusha chama hicho katika uchaguzi mkuu mwaka huu na uchaguzi mwingine na kuongeza anaamini hata nukuu zake zitakuwa dira ya kukiongoza chama hicho kwa siku za mbele.

Balozi Karume alisema kwa hotuba hiyo ni wazi kuwa Rais Kikwete amezungumzia mambo ya msingi na amedhihirisha anatanguliza maslahi ya chama chake na si marafiki zake.
“Ameweka wazi kwenye suala la kuchagua kiongozi kwa ajili ya kupeperusha bendera ya chama, hakuna sababu ya kutanguliza urafiki,” alisema.

Amenukuu baadhi ya maneno yaliyokuwa yakizungumzwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, lakini naamini hata hotuba yake ya leo (jana) itakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho.

“Hotuba hii ya Rais itatumika kama nukuu kwa ajili ya chaguzi na namna ya kukiendesha chama. Nimekaa nje ya nchi kwa muda mrefu, alichozungumza mwenyekiti amedhihirisha kiwango chake kwenye siasa ni cha hali ya juu,” alisema.
Alisema Rais Kikwete amezungumza na wajumbe wa NEC, lakini hakuonesha anataka nani achaguliwe, kwani hakuwa upande wowote zaidi ya kuzungumza hali halisi ya chama hicho na wakati uliopo.
“Ingekuwa wengine hapa tungeanza kupata maelekezo ya rais kuhusu nani anataka awe rais ajaye baada ya kumaliza muda wake, lakini yeye hana chaguo lake, hivyo ametaka sifa, kanuni na maadili ya chama iwe dira ya kupata viongozi,” alisema.
Raya
Mjumbe mwingine kutoka Wilaya ya Rorya, mkoani Mara, Thobias Raya, alisema hotuba hiyo imetoa suluhisho la ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao.
Alisema kwa mazingira ya sasa, kinachoangaliwa ni uwezo wa mtu na kukubalika kwake na si suala la fedha kama baadhi ya watu wanavyodhani.
“Fedha si msingi wa kumpata mgombea. Chama kinahitaji kuteua mgombea mzuri atakayekivusha chama kwa nafasi anayoomba bila kujali hali ya kiuchumi,” alisema.
Kimbita
Naye Mjumbe kutoka Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Fuya Kimbita, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa chama na kwamba kila mjumbe anapaswa kutembea na hotuba hiyo.
“Kwa kweli ni hotuba nzuri sana, binafsi nimefurahishwa, amezungumzia hali halisi ya siasa ya Tanzania kwa hivi sasa, amewafungua macho wajumbe.
“Wakati wenzetu wanaishi kwa kuzingatia fikra na hisia na kizazi cha sasa, sisi tunaishi na kizazi cha sasa lakini mipango na utaratibu wetu tunafanya kizamani, lazima tubadilike,” alisema.
Bulembo
Akizungumzia hotuba ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Alhaj Abdallah Bulembo, alisema amefurahishwa na hotuba hiyo, lakini naye alitumia nafasi hiyo kuweka wazi mgombea wa CCM lazima awe msafi asiyekuwa na kashfa chafu.
Alisema kuwa mgombea wa CCM anayetaka kugombea uongozi si yule mwenye mbwembwe na madoido mengi, bali ni mtu mwenye kujitambua. “Anayejiamini yeye ni msafi agombee, lakini kama ni mchafu ni vema akakaa kando,” alisema.

Mgeja
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja, alisema hotuba ya Rais Kikwete ni darasa tosha kwa wana-CCM, hasa kipindi hiki, kwani kwenye suala la kuchagua viongozi, ameeleza wazi umuhimu wa kuchagua viongozi kulingana na kukubalika kwao kwa wananchi.

Aliwataka wajumbe wa NEC na wana CCM kwa ujumla kuisikiliza kwa umakini hotuba hiyo ili kufahamu misingi ya chama hicho, huku akielezea kuunga mkono kauli ya Rais kuwa lazima wanachama hao wasome alama za nyakati kwa kuchagua viongozi wazuri.
“Nimesikiliza vizuri hotuba ya mwenyekiti wetu, amezungumza mambo ya msingi ambayo kwetu sisi ni darasa tosha. Lazima tusome alama za nyakati.
“Uchaguzi wa Sekali za mitaa uliofanyika mwaka jana tumeshuhudia baadhi ya mitaa imekwenda upinzani kwasababu ya viongozi kuwa na watu wao na si wale wanaotakiwa na wananchi.
“Hivyo lazima tuchague viongozi kwa kuangalia wananchi wanamtaka nani na si kiongozi anataka nani awe kiongozi,” alisema Mgeja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles