Na TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM
KUMEKUWAPO na dhana kwamba baadhi ya shule binafsi zinafanya udanganyifu katika matokeo ya mitihani ya Taifa.
Dhana hii inatokana na ukweli kwamba wamiliki wa shule hizi ni wafanyabiashara hivyo hulazimika kuzitangaza shule zao kwa kuonesha zinafanya vizuri katika mitihani ya Taifa.
Baadhi ya shule zimekuwa zikifanya udanganyifu huu kutokana na ukweli kwamba hawakuwa na maandalizi ya kutosha sambamba na kutokuwa na mitihani ya kujipima kabla ya mtihani ya kuhitimu.
Interschool examination ni mradi ulioandaliwa na taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia masuala ya elimu ya Teacher’s Junction ambayo iliandaa mitihani kwa shule binafsi za mikoa ya Arusha na Dar es Salaam.
Ofisa Mradi wa Interschool exam, Njama Salum anasema huo ni mradi shirikishi uliobuniwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wa shule binafsi.
Anasema shule nyingi binafsi zimejikita katika ushindani huku wakitupilia mbali ubora wa taaluma wanazotoa.
“Baadhi zimefikia hata kufanya udanganyifu katika mitihani ya Taifa ili waonekane wanafundisha zaidi bila kujali taaluma wanazowapa wanafunzi.
Anasema kwa kuliona hilo wao wameamua kubuni mradi wa kuwapima wanafunzi wa shule za msingi binafsi kabla ya mitihani ya Taifa.
Njama anasema walimu wa shule husika hutunga mitihani kwa masomo yote kwa darasa la saba na nne kisha kuikabidhi kwao ili kuiboresha.
“Tunapoipokea mitihani hii, tunaichuja na kuandaa mtihani wa pamoja ambao hufanywa na shule zote kwa siku moja, ambapo hufanywa kwa usimamizi mkubwa.
“Hii inawasaidia wanafunzi kujipima na kuwajengea hali ya kujiamini katika ufanyaji wa mitihani, pia kuwaondoa hofu,” anasema Njama.
Anasema faida za mitihani hii ni pamoja na kuwasaidia walimu kutambua upungufu unayopatikana katika ufundishaji wao.
“Inawasaidia walimu kujua uwezo wa uelewa wa wanafunzi walionao ili waweze kuangalia mbinu mpya za kufundisha,” anasema.
Anasema baada ya mitihani huandaa ripoti ya mitihani na kuzipeleka katika shule zilizoshiriki.
“Timu ya Interschool exam wakiongozana na shule zilizofanya vizuri huzitembelea shule ambazo hazijafanya vizuri na kuwapa ushauri,” anasema Njama.
Kwa upande wake Mkuu wa shule mstaafu, Athman Ahmed anasema mitihani hiyo itawajengea wanafunzi kujiamini zaidi katika kufanya mitihani na hivyo kuinua taaluma nchini.
“Nitoe rai kwa wazazi kutoa ushirikiano kwa walimu na wamiliki wa shule katika kukuza taaluma ya watoto wetu,” anasema Ahmed.
Anasema hizi ni juhudi binafsi zilizoanzishwa mahususi kuinua elimu hivyo ni vema kuziunga mkono.
“Niwapongeze walioanzisha wazo hili kwa kuwa ni juhudi za dhati kuinua taaluma inayotolewa na shule binafsi,” anasema Ahmed.
Mwanafunzi wa darasa la nne aliyefanya vizuri na kutunukiwa, Hanspoppe Jeremia kutoka shule ya msingi Sakana, anasema juhudi binafsi zimemsaidia kufika hapo alipo.
“Huwa najisomea usiku ninapokuwa nyumbani, hii hunisaidia kukumbuka ninapokuwa katika mitihani,” anasema Hanspoppe.
Naye mshindi wa jumla kwa darasa la saba kutoka katika shule ya Green Acre, Nakiye Mwinuka anasema amefurahishwa na mashindano ya mitihani hiyo kwani itamsaidia kujiimarisha kwa mtihani wa taifa wa darasa la saba.
“Ninafuraha kushinda katika mitihani hii, naamini itaniongezea hali ya kujiamini katika mitihani ya mwisho,” anasema Nakiye.
Anawaomba wanafunzi wenzake kujituma na kutumia muda wao vizuri ili waweze kufikia malengo wanayoyataka.
Mkuu wa shule ya msingi ya Sakana ambayo alitokea mshindi wa jumla kwa darasa la nne, Johansen Rwebugisa anasema amefarijika kutoa mwanafunzi bora kwa mikoa miwili.
“Lengo la walioanzisha Interschool ni zuri kwa kuwa tunaweza kuinua kiwango cha elimu kwa kuongeza ushindani kwa shule zetu,” anasema.
Akizumgumzia maisha ya shule ya mwanafunzi aliyefanya vizuri, Hanspoppe Jeremia anasema ni kijana anayejituma.
“Hanspoppe ni kijana anayejituma na anapenda kutunza muda na mwanafunzi mwenye nidhamu ya hali ya juu,” anasema Rwebugisa.
Naye Gracian Mbelwa ambaye ni mmiliki wa shule ya Mothers’ of Mercy anasema amefurahishwa na tukio hilo ambalo litawawezesha kutambua uwezo wa wanafunzi walionao.
“Tukiendelea na utaratibu huu tunaweza kuinua kiwano cha elimu kwa shule zetu kwani kwa sasa ushindani utaongezeka,” anasema Mbelwa.
Anatoa wito kwa shule nyingi kuingia katika mitihani hiyo ili kuongeza ushindani kwa wanafunzi.
Katika mitihani hiyo jumla ya shule 13 zilishiriki na kupata washindi wa kila shule na washndi wa jumla.
Shule hizo Dar es Salaam ni Sakana, mothers of Mercy, Green Acre Mabibo, Green Acre Mbezi, Bright View,Emmy na Grace.
Kwa Arusha shule zilizofanya mitihani hiyo ni Tumaini,Upendo friends, Kilimanjaro, Dominion, Mecson na Marian.