EWURA YATANGAZA BEI KIKOMO ZA BIDHAA ZA MAFUTA YA PETROLI

0
601

Na Faraja Masinde

Mamlka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini zitakazoanza kutumika rasmi leo Julai mosi huku ikitoa onyo kwa wafanyabiashara wanaoficha mafuta.

Kauli hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Mhandisi Gogwin Samweli, ambapo alisema kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya aina zote petroli, dizeli na mafuta ya taa zimepungua ikilinganishwa na toleo lililopita la Juni 7 mwaka huu.

Alisema kwa mwezi Julai mwaka huu bei za mafuta ya petroli zitashuka kwa shilingi 37 kwa lita, dizeli shilingi 14 kwa lita na mafuta ya taa kwa Sh 0.73 kwa lita.

“Bei hii imeshuka kutokana na mfumo wa uingizwaji mafuta katika soko la Dunia na mafuta haya tutakayoanza kuyatumia kesho, yalinunuliwa Mei mwaka huu wakati ambapo kulikuwa na ushindani mzuri ambapo vile vigezo vya kununulia mafuta vilifanya mafuta haya yapatikane kwa bei ya chini.

“Mfumo huu wa uingizaji mafuta pamoja huwa ni kushindania faida hivyo huu unasaidia kuelewa bei halisi na kiwango cha mafuta yanayoingia tofauti na awali ambapo mafuta mengine yalikuwa yakiingiziwa bandari ya Bagamoyo,” alisisitiza Samweli

Aliongeza kuwa bei za jumla na rejareja kwa mafuta ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa shilingi 43 kwa lita na shilingi 4 kwa lita upande wa dizeli, katika Mkoa wa Tanga ikilinganishwa na toleo lililopita la Juni 7 mwaka huu.

“Pia bei za jumla za petroli na dizeli kwa Mkoa wa Tanga zimepungua kwa shilingi 43.07 kwa lita na shilingi 3.81 kwa lita, ongezeko hili kwa Tanga linatokana na mabadiliko ya bei za mafuta katika soko la dunia kwa mzigo mpya uliopokelewa katika bandari ya Tanga Juni mwaka huu ikilinganishwa na bei za mzigo wa mwisho kupokelewa Aprili mwaka huu,” alisema Samweli.

Alisema kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu isizidi bei kikomo.

Aliongeza kuwa kwa Dar es Salaam bei ya mafuta ya petroli imeshuka kufikia Sh 2,014 kwa lita, dizeli Sh 1,874 kwa lita na mafuta ya taa kwa Sh 1,806 kwa lita.

Pia aliwataka wafanya biashara wanaoficha mafuta kuacha mara moja mchezo huo kwani ni sawa na kuhujumu uchumi.

“Mtu unayehodhi mafuta bila kuuza wewe ni sawa na mhujumu uchumi, hivyo ukibainika unamafuta alafu hauuzi adhabu yake ni shilingi milioni 7 hadi 20,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here