UPENDO MOSHA, MOSHI
Mgombea Ubunge Jimbo la Vunjo kwa tiketi ya Chama Cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia amesema iwapo atapata ridhaa ya kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa awamu ya pili atahakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji Safi na salama.
Mbatia ameyasema hayo katika mkutano wa adhara wa kampeni, uliofanyika kijiji cha Kiruweni, Kata Mwika kusini, ambapo alisema bado anayo nia ya dhati ya kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo ikiwemo kuboresha miundombinu mbalimbali ya maji, barabara na umeme.
Alisema pamoja na kushughulikia na kutatua kero mbalimbali Katika Jimbo hilo ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara kupitia taasisi ya maendeleo ya Vunjo ya (KDF) bado tatizo la ukosefu wa maji Katika Jimbo hilo ni changamoto.
“kuna maendeleo mengi ambayo nimeyaleta hapa kwetu Vunjo Ila Kuna baadhi ya mambo ambayo nilikuwa nayashughulikia ikiwemo la maji sijalikamilika kwa asilimia zote hivyo ndugu zangu naombeni mniamini mnipe tena ridhaa ya kuwa Mbunge wenu nitatue changamoto hii,” alisema.
Mbali na hilo Mbatia ameahidi kuendeleza utekelezaji wa miradi ya barabara katika jimbo hilo kwa lengo la kuhamasisha shughuli za maendeleo ikiwemo usafirishaji wa mazao.
Mbatia alisema iwapo wananchi hao watamuamini na kumchagua tena kuwa mbunge wao atahakikisha miradi yote ya barabara inakamilika ikiwemo uboreshaji wa sekta mbalimbali kama, afya na elimu.