30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

JPM awasha moto Dar

 FARAJA MASINDE Na NORA DAMIAN– DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameanza kuliangalia Jiji la Dar es Salaam kwa namna nyingine, baada ya kumwagiza Mkuu wa Mkoa, Aboubakar Kunenge abadilike na kuachana na upole.

Amemtaka mkuu huyo wa mkoa awe mkali kwa lengo la kuhakikisha miradi ya jiji hilo inaenda vizuri, huku akiagiza kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani huko Mbezi Luis.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana Dar es Salaam akizungumza na wakazi wa jiji hilo wakati wa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi.

Ametaka ujenzi wa kituo hicho wenye gharama ya Sh bilioni 71, ambao umekamilika kwa asilimia 85, ukamilike rasmi mwezi ujao.

Aidha Rais Magufuli alimwagiza waziri mwenye dhamana ya ujenzi kufuatilia kwa karibu sababu za mkandarasi wa mradi huo uliotakiwa kukamilika Julai mwaka huu kuuchelewesha na kutaka aukabidhi Februari mwakani, ikiwezekana aanze kukatwa gharama za kuchelewesha mradi huo baada ya Novemba.

“Lakini pia wahandisi wa mkoa na wilaya hamieni hapa msimamie huu mradi ili ukamilike Novemba. 

“Kwa hiyo uongozi wa mkoa, ninajua mkuu wa mkoa wewe ni mgeni hapa, lakini badilika uwe mkali usiwe sheikh au askofu, ni lazima watu watimize wajibu wao, muondoe ‘damage’ ambayo iko kwenye mkataba,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaaam, Spora Liana, kuhakikisha mradi huo unakamilika kabla ya Novemba huku akiagiza mkandarasi kuanza kukatwa pesa zake kwa sababu ameuchelewesha.

“Mimi nataka wafanye mpaka wawe wanafia hapa na corona, jengo limalizike haraka, kwa sababu saa nyingine mkataba huu ni wa Sh bilioni 71, ulikuwa umalizike Julai, leo ni Oktoba na waziri alikuwa anazungumza hapa kuwa walitakiwa kukabidhi Januari, hii siyo sawa, sababu kuanzia Julai mpaka Januari ni miezi minne, palitakiwa watu wawe wanafanya kazi hapa wanaingiza pesa. 

“Palitakiwa hizo ajira za watu 10 iwe hapa katika kipindi cha hiyo miezi 10 nani atayezilipa hizo fedha na kuzifidia? Ndiyo maana nalisema hili, mradi ni mzuri lakini utekelezaji wake ni mbovu.

“Haiwezekani watu watafute visingizio vya corona, mkandarasi alitakiwa awe hapa, kwa hiyo waziri, huyu mkandarasi aanze kukatwa pesa za kuchelewa kukabidhi mradi na fedha hizo zitatumika kuwasaidia Watanzania wanyonge,” alisema Rais Magufuli.

Alisema iwapo miradi mingi itaendeshwa kwa mfumo huo basi itachelewa na hivyo kuzorotesha maendeleo. 

“Haiwezekani hawa wakandarasi ifike mahali viongozi wa Dar es Salaam mlielewe hili, hizi ni fedha za Watanzania masikini, wamewekeza hapa ili wapate faida ya mradi huu, kwa hiyo haiwezekani mnasema corona, baadaye mtasema mvua, baadaye matope, baadaye jua, haiwezekani. 

“Mkurugenzi wa Jiji wewe ndiyo ulisaini mkataba huu, nataka kabla ya mwezi wa 11 mradi huu uwe umemalizika, wafanye kazi usiku na mchana, umeme upo, maji yapo, fedha zipo, hakuna sababu ya kusingizia corona, mbona hawajavaa barakoa hapa,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli aliwaomba watendaji wake, akiwamo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa haraka.

“Hapa palitakiwa leo kuwe na mama lishe hapa, wanafanya biashara, dereva taksi wanafanya kazi zao hapa, Bodi ya Wakandarasi na Bodi ya Wahandisi muanze kuangalia huu mradi kwa kuufuatilia kikamilifu. 

“Mhandisi Mshauri (Chuo cha Ardhi) inawezekana mnataka mkae kwenye eneo la mradi ili mlipwe, tumewapa hii kazi ili mumbane mkandarasi na siyo kuwa sehemu ya mkandarasi, hakikisha mnambana sawasawa mkandarasi huyu, huyu ni kibarua wetu, fedha za Watanzania.

“Nataka niwaeleze, huu mradi nitaufuatilia vizuri mimi alafu kama hamtatapika kama kuna hela zozote mlizozimeza,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ameangalia mradi huo kila mahali na kwamba fedha za mradi huo Sh bilioni 71 ni nyingi. 

“Sh 71 bilioni? Kwa sababu nataka niseme wazi, fedha nilizohidhinisha mimi baada ya mgogoro, kuanza kuupata huu mradi kulikuwa na mgogoro mkubwa, walikuwa wanagombana baadhi ya watendaji wakiwamo madiwani, tukahidhinisha Sh bilioni 51, leo ninaambiwa ni Sh bilioni 71, tayari imeshatokea ongezeko.

“Inawezekana hiyo kazi iliyoongezeka ni muhimu, nimeambiwa na waziri kuna daraja, sasa daraja la kugharimu Sh bilioni 21 nitaliangalia na lenyewe nilione hilo daraja, sababu kwa bahati nzuri kwenye sekta ya ujenzi nimekaa karibu miaka 20 ninajua, lakini nimeona hili lizungumze wazi ili watendaji waanze kujipanga vizuri kwanza kwa ajili ya thamani ya pesa na muda,” alisema Dk. Magufuli.

Aliwataka mkandarasi na mshauri kushinda kwenye eneo hilo la mradi na kwamba baada ya Novemba wataanza kukatwa sehemu ya pesa.

Alisema kituo hicho kitakuwa kikubwa katika Jiji la Dar es Salaam linalokadiriwa kuwa na wakazi milioni sita.

“Hili pia litahusisha nchi mbalimbali ndani ya SADC (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika) ikiwa ni pamoja na ndugu zetu wa Malawi ambao ni ndugu zetu, na ninataka katika jengo hili kuwapo na ofisi ya Uhamiaji, pia mabasi ya nje ya nchi yawe na sehemu zao, ya ndani, teksi, mamalishe hivyo hivyo, hii italeta faida ya fedha za Watanzania,” alisema Rais Magufuli huku akiwaonya watendaji wa Serikali kuacha kushirikiana na wakandarasi.

Rais Magufuli aliweka jiwe hilo pamoja na Rais wa Malawi, Dk. Lazarus Chakwera ambaye alikuwa nchini kwa ziara ya siku mbili.

Kituo hicho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kubeba mabasi 1,000 na teksi 280 kwa siku, pia kutakuwa na maeneo ya bodaboda na bajaji na eneo la mamalishe na babalishe.

Mradi huo umegharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 22 sawa na Sh bilioni 71 ambao ukikamilika utasaidia kupunguza msongamano wa mabasi yaendayo mikoani kwa kiasi kikubwa.

Mapema jana, Rais Magufuli akiwa na mkewe Janeth Magufuli alikagua kazi za ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya Ubungo (Ubungo Flyover).

Rais Magufuli alipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale.

Alisema kuwa kwa Jiji la Dar es Salaam wametumia Sh bilioni 660 kwenye miundombinu tu na kwamba tangu uhuru jiji hilo la kibiashara halijawahi kuwa na miundombinu bora ya barabra kama ilivyo hivi sasa.

Pia aliwasihi Watanzania kuendelea kulinda amani kwakuwa ndiyo msingi wa haya yote yanayoendelea kufanyika na kuwataka kudumisha amani hiyo hata baada ya Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28.

 KUENDELEA NA KAMPENI DAR 

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli leo atafanya mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Mkapa akijikita kueleza mafanikio ya utekelezaji ilani iliyopita na yale yatakayotekelezwa miaka mitano ijayo.

Rais Magufuli ambaye alifanya mkutano wa mwisho Oktoba 3 visiwani Zanzibar alipumzika kwa muda kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa.

Akizungumza jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema Rais Magufuli ataeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na matarajio kwa miaka mitano ijayo.

“Kesho (leo) Dar es Salaam inakwenda kusimama, utakuwa ni mkutano mkubwa wa kampeni. Magufuli atatuongoza kuomba kura kwa Watanzania waishio Dar es Salaam watupe dhamana ya uongozi wa nchi hii ili kazi tuliyoianza akaiendeleze katika muhula wake wa pili wa miaka mitano,” alisema Polepole.

Dar es Salaam unakuwa mkoa wa 14 kufanya kampeni tangu chama hicho kilipozindua kampeni zake Agosti 29 jijini Dodoma.

Mikoa mingine ambayo Dk. Magufuli ameshafanya kampeni ni Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Kigoma, Njombe, Iringa, Mbeya na Songwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles