JESHI la polisi mkoani Simiyu linamshikilia Kimola Salulu (30) wa Kijiji cha Mwakiloba katika Kata ya Lamadi wilayani Busega kwa tuhuma za kukutwa na meno mawili yanayodhaniwa kuwa ya tembo, anaripoti Derick Milton.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Simiyu, Jonathan Shana alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa kijijini hapo Machi 19 mwaka huu na polisi waliokuwa kwenye doria maalum ya kupambana na ujangili ndani ya hifadhi.
Alisema katika operesheni hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na polisi kwa kushirikiana na askari wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, nyara hizo zilikamatwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.