NA SAIMON MGHENDI, SHINYANGA
JESHI la polisi mkoani Shinyanga linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuuza madini ya dhahabu njee ya masoko ya dhahabu, masoko ambayo yalioanzishwa na serekali kwa lengo la wachimbaji wadogo waweze kunufaika pamoja na serekali iweze kupata mapato.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, kamishina Joseph Paul akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake alisema tukio hilo lilitokea Julai 14 mwaka huu saa moja usiku katika machimbo ya Mwakitolyo Wilaya ya Shinyanga vijijini.
Kamanda huyo wa jeshi la Polisi mkoani humo alisema jeshi la polisi kwa kushirikiana na tume ya madini Mkoa wa Shinyanga, liliwakamata watu watano wakiwa na gramu 11.4 za dhahabu wakiwa wanafanya biashara nje ya soko la madini jambo ambalo ni kukiuka sheria za madini na kuifanya Serikali ipoteze mapato.
Aidha aliwaeleza waandishi wa Habari kuwa watu hao watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliwataka wafanyabiashara kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali ili kuweza kunufaika na raslimali hizo na siyo kukwepa ama kutorosha madini hayo kwani masoko yamefunguliwa kila mahali.
Kwa upande wake Ofisa Madini Mkoa wa Shinyanga, Joseph Kumburu alisema ofisi ya madini Shinyanga ilipata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa kuna baadhi ya watu wanaendelea kufanya biashara ya ununuzi wa madini ya dhahabu nje ya utaratibu wa masoko.
Kumburu alisema watu hao wametenda kosa kwa kukiuka kifungu cha 6 cha kanuni za masoko za mwaka 2019, na kuongeza kuwa baada ya kupata taarifa hizo, tume ya madini ilishirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ambapo Julai 14waliweka mtego katika operesheni hiyo iliyofanyika eneo la mwakitolyo.
“Katika operesheni hiyo tulifanikisha kuwakamata watuhumiwa saba katika eneo la Mwakitolyo namba 1, 2 na 3. Ambapo watuhumiwa hao walikutwa wakinunua dhahabu nje ya soko huku mmoja akikamatwa akiwa na gramu 6 na mtuhumiwa mwingine gramu 2.6,” alisema Kumburu.
Kumburu aliwataja watuhumiwa kuwa ni Matingwa Matembe (56), Magida Magida (38) Makomba Maduhu (40) Malugu Nzemi (45) Kija Ndakile (44) Daud Soni (32) pamoja na Singu Legele (37).
Alisema tukio hilo ni la pili ambapo awali vijana sita walikamatwa ambao baadaye walikiri makosa yao na kulipa kodi zote za Serikali kwa hiari yao wenyewe.