33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mbaroni kwa kutaka kumuua mtoto kwa imani za kishirikina

Na AMON MTEGA-SONGEA

WATU nane wakiwa na mtoto mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi tisa, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma za kukutwa wakifanya ramli chonganishi pamoja na vitendo vya ushirikina juu ya kilele cha mlima Mgwijima katika Wilaya ya Namtumbo.

Tukio hilo limetokea ikiwa imepita miezi michache tangu kuibuka matukio mengine ya watoto wenye umri kati ya miaka miwili hadi sita kuchinjwa na kukatwa koromeo, sehemu za siri, masikio na ulimi katika Mkoa wa Njombe.

Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ACP Simon Maigwa alisema tukio hilo lilitokea Juni 17 mwaka huu katika eneo la kilele cha mlima Mgwijima uliopo Namtumbo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Fredrick Ngalibhenaye (44), Oliva Kaduma (33), Beatus Lutenge (53), na Samola Raphael (32) ambao wote ni wakazi wa Makambako katika Mkoa wa Njombe.

Watuhumiwa wengine ni Rajab Yasini (38), Nasibu Issa (25), Omary Salumu (50) na Faraji Panjapi (41) ambaye ni mganga wa jadi pia ni wakazi wa kijiji cha Minazini Wilaya ya Namtumbo.

Alisema kuwa watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mbuzi mweusi, kuku mweusi, kuku mweupe, kigoda cheusi, vitambaa vyeusi na vyeupe vikiwa na shanga pamoja na mikuki minne ambavyo vitu hivyo viliandaliwa kwa ajili ya kufanyia vitendo hivyo vinavyodaiwa ni vya kishirikina.

Kamanda Maigwa alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu hao ambao wengine wametokea Mkoa wa Njombe na wengine Mkoa wa Ruvuma kutokana na kupambana na vitendo viovu ambavyo hivi karibuni vilikuwa vikijitokeza katika mkoa wa Njombe hasa vya kuwauwa watoto wadogo.

“Jeshi la Polisi tunatilia shaka kutokana na watuhumiwa hao kuwa na mtoto mdogo, kisha kwenda kufanya vitendo hivyo vya kishirikina jambo ambalo lingeweza kusababishia madhara kwa mtoto huyo kwa vitendo hivyo,”alisema.

Kwa upande wake mmoja wa watuhumiwa hao, Oliva Kaduma ambaye ni mama wa mtoto huyo alisema kuwa yeye alioteshwa njozi kuwa akafanye matambiko katika chimbuko walikotokea wazazi wake katika mlima huo ili aweze kutatua matatizo yake.

Januari 27 mwaka huu,watoto 10 wenye umri kati ya miaka miwili hadi sita wamechinjwa na kukatwa koromeo, sehemu za siri, masikio na ulimi wilayani Njombe mwezi huu.

Kutokana na matukio hayo yanayodaiwa kuhusishwa na imani za kishirikina, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri alitoa kwa wazazi na walezi kuwapeleka na kuwafuata shule watoto wao.

Pia, aliagiza watoto wote wilayani humo kuhakikisha kuwa wanatembelea kwa makundi.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema watoto sita wamefanyiwa ukatili huo katika Halmashauri ya Mji wa Njombe na wanne wanatoka Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

“(Kati ya) sita waliookotwa (wakiwa wamekufa) Halmashauri ya mji Njombe, wawili walipotea na kuokotwa wakiwa wameuawa misituni, wawili wameokotwa maeneo tofauti wakiwa wamekufa na hawakutambulika, wamezikwa na halmashauri,” alisema.

Mbali na matukio hayo kutokea Njombe, Oktoba mwaka jana na Februari mwaka huu matukio kama hayo yaliibuka mkoani Simiyu ambapo Mtoto Susan Shija (9), mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mwabasabi ndiye aliuawa na maiti kutelekezwa ndani ya nyumba ambayo ujenzi wake haujakamilika.

Vilevile Desemba 13 mwaka jana  mwili wa mtoto mwingine, Milembe Maduhu (12) ulikutwa akiwa ameuawa na kutelekezwa nyumba ya aina hiyo eneo la Lamadi mkoani Simiyu, kabla ya tukio lingine la karibuni la Februari 8 la mwili wa mtoto Joyce Joseph (8), mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Lukungu kukutwa ameuawa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles