29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waliochota mabilioni ya Libya wasakwa nchini

Na ANDREW MSECHU

TAASISI ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (Takukuru), imetangaza kuwasaka watu wanne wanaodaiwa kutoweka na zaidi ya Sh bilioni 46, ambazo ni mkopo kutoka Serikali ya Libya ili kujenga Kiwanda cha Saruji mkoani Lindi.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema fedha hizo kwa Serikali ya Tanzania na Serikali ya Libya, kama mkopo wenye riba.

Alisema kwa kuwa Serikali haifanyi biashara, fedha hizo zilikabidhiwa kwa kampuni ya MEIS Industries Ltd mwaka 2009 kwa ajili ya kujenga kiwanda hicho, lakini hadi sasa hakijawahi kuonekana na wahusika hawajulikani walipo.

“Mwaka 2009 Serikali hizi mbili zilitia saini mkataba ulioitaja kampuni ya MEIS Industrial Limited kama kampuni itakayopewa dola milioni ishirini za Marekani kwa ajili ya uwekezaji wa ujenzi wa kiwanda cha Saruji eneo la Machore mkoani Lindi.

“Fedha hizo zilitolewa kwa kampuni ya MEIS kama mkopo uliopaswa kurejeshwa kwa riba nafuu na kwa mujibu wa mkataba, mkopo huo ulipaswa kurejeshwa ndani ya miaka sita, yaani 2011 hadi 2017. Hata hivyo, hadi mwaka 2019 kampuni hiyo haijarejesha mkopo huo wala kiwanda cha saruji kilichokusudiwa kujengwa bado hakijajengwa,” alisema.

Alisema uchunguzi uliofanywa na Takukuru umebaini kuwa sehemu kubwa ya fedha hizo imetumika kwa matumizi mengine kinyume na makusudio ya Serikali jambo ambalo ni kosa.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema wahusika wa kapuni ya MEIS ambao wanatafutwa ni Islam Ally Saleh Balhabou, Merey Ally Awadh Saleh, Sabri Ameir Kuleib na Abdallah Said Abdallah bin Aliya, ambao hadi sasa hawajulikani walipo.

Alisema zipo taarifa kuwa huenda wengine walikimbilia Visiwa vya Comoro na wengine nchini Uingereza, hivyo juhudi za kuwatafuta zinaendelea.

“Tunatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa sahihi za mahali watuhumiwa hawa wanapoweza kupatikana wawasiliane nasi ili wakamatwe na kuja kujibu tuhuma hizi zinazowakabili kwa kuwa kosa hili liko chini ya kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007,” alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mikopo iliyotolewa na Serikali ya Libya kwa Tanzania, alisema Serikali ya Libya katika miaka ya 1980 iliikopesha Serikali ya Tanzania mafuta ya petrol na dizeli kiasi cha tani 200,000 za ujazo ambayo kufikia mwaka 2005 ilikuwa ikiidai Serikali ya Tanzania Dola 201,000,000.

Alisema kutokana na fedha hizo, Serikali ya Libya ilisamehe nusu ya deni ambapo Seriali hizo mbili zilikubaliana namna ya kulipa dola 101,000,000 zilizobaki.

“Katika makubaliano haya, dola milioni 61 zilitakiwa kulipwa kwa mtindo wa madeni ya kitaifa, dola milioni 20 zilipwe kwa mpango maalumu na dola 20 milioni zifanye uwekezaji nchini Tanzania na baadaye zirudishwe Libya kwa riba nafuu,” alisema.

Alieleza katika mpango huo, kampuni hiyo ya MEIS ilipopewa fedha hizo kwa ajili ya kufanya uwekezaji nchini ambao ulitakiwa uwe umeshakamilika na urejeshaji wa fedha hizo nchini Libya kwa riba nafuu uwe umeshakamilika kufikia mwaka 2017.

Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani aliliambia Mtanzania kwa njia ya simu kuwa watuhumiwa wanaotafutwa ni raia wa Tanzania ambao ni wakazi wa Kilosa mkoani Morogoro.

“Hawa wote taarifa zinaonesha kuwa ni Watanzania, ambao makazi yao ni Kilosa kkoani Morogoro. Kwa hiyo ni watu ambao taarifa zao ni rahisi kupatikana,” alisema.

Alisema fedha hizo zilitia saini na Serikali ya Libya, ambapo kwa upande wa Tanzania Wizara ya Fedha iliiwakilisha Serikali na fedha hizo ziliwekwa kwenye Benki ya Rasilimali nchini(TIB).

Watuhumiwa wengine

Katika hatua nyingine, Brigedia Jenerali Mbungo alisema Takukuru inawashikilia watu sita waliokuwa wakishirikiana kufanya utapeli, ambapo wanne kati yao walikuwa wakijifanya maofisa wa Takukuru na vyombo vingine vya dola, huku wawili wakitoka katika kampuni moja ya simu.

Alisema watuhumiwa hao walimamatwa na maofisa wa Takukuru kwa awamu kuanzia Jumatatu Juni 10 mwaka huu baada ya kupata ushirikiano kutoka kwa watoa taarifa.

Sare za jeshi

Bregedia Jenerali Mbungo alisema Takukuru opia imefanikiwa kumkamata Mohamed Abdallah, mkazi wa Kinyerezi jijini Dar es Salaam aliyekutwa akiwa na sare za jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), simu na laini za simu alizokuwa akizitumia kufanya utapeli.

Alisema Takukuru inaendelea kufanya uchunguzi wa kuwakamata watuhumiwa wengi zaidi baada ya kubaini kuwa matapeli hao wana mtandao mkubwa unaohusisha watumishi wa baadhi ya kampuni za simu.

Alisema miongoni mwa vifaa vilivyokutwa kwa matapeli hao ni sare za jeshi la Wananchi, laini za simu, simu 10 za kiganjani, funguo za kufungulia pingu, noti bandia za Sh10,000 kiasi cha Sh 100,000 na karatasi yenye namba za simu za watu kwa ajili ya kuwasiliana nao kwa utapeli.

Alisema katika mahojiaoi na Takukuru, watuhumiwa hao walikiri kuhusika na uchapaji wa noti bandia kinyume cha sheria za nchi.

Brigedia Jenerali Mbungo alisema uchunguzi wa Takukuru pia umebaini kuwa matapeli hao wana mtandao mpana unaojumuisha hadi watu kutoka maeneo ya ofisi za Serikali, ambao wamekuwa wakiwafuatilia watumishi au viongozi ambao kwa njia moja au nyingine wanaweza kuwa na tuhuma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles